Monday, April 23, 2012

WAKAZI WA VINGUNGUTI WAITAKA UONGOZAI WA KATA KUACHIA NGAZI

 
BAADHI ya wakazi wa Vingunguti wilayani Ilala wameutaka uongozi wa Kata hiyo kuachia ngazi kutokana na ufisadi unaofanyika katika mradi wa maji.
 
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa masharti ya kutotajwa majina katika ukurasa huu jijini Dar es Salaam leo , wakazi hao walisema Kata hiyo ina visima vipatavyo 200 lakini fedha zinazo kusanywa kutokana na mradi huo hazijulikani zinakokwenda.
 
Walisema wameutaka uongozi wa Kata hiyo, akiwamo diwani ambaye  amedaiwa kuwa ndio anayewalinda watendaji hao wabovu na wafujaji wa mradi huo wa maji.
 
Wakazi hao walitanabaisha kuwa mradi huo ambao umekuwa ukiingiza fedha nyingi umekuwa haufahamiki mapato yake ya mwezi wala haifahamiki katika akaunti yake kuna shilingi ngapi.
Walisema watendaji hao imekuwa ni kawaida kwao kukataa kuitisha mikutano  kila baada ya miezi mitatu (3), ya kuwasomea wananchi wakata hiyo mapato na matumizi ya mradi huo.
 
Akitoa ufafanunuzi kuhusiana na madai hayo diwani wa Kata hiyo, Assaa Haroun alisema taarifa hizo hazina ukweli kwani kata hiyo haina visima 200 ambapo mradi huo una visima visivyopungua tisa (9).
 
Alisema watu hao wanaopitapita kueneza taarifa hizo za uongo ni wale walionguliwa katika usimamizi kutokana na historia yao mbaya ya kuua miradi kila walipopita.
Haroun alisema akiwa msimamizi wa miradi mbalimbali anahakikisha hatakubali kuona miradi ya wananchi inachezewa na baadhi ya watu wenye nia mbaya.
 
Alisema ataisimamia kwa nguvu zake zote miradi hiyo ili mradi inakuwa yenye manufaa kwa wananchi ambapo kuzembea kwake kutamfanya ajekubeba lawama kuliko mtu yeyote mwingine.

No comments: