Thursday, April 12, 2012

Watendaji wa vijiji na kata wilaya ya Longido watafutiwa dawa

Mbunge wa Jimbo la Longido, Lekule Laizer
Na.ashura Mohamed,Arusha

Kutokana na watendaji wa kata na vijiji kukithiri kwa ubadirifu wa fedha za serikali na wananchi, halmashauri ya wilaya ya longido imejipanga kukabiliana na tatizo hilo ili kuokoa fedha ambazo zimekuwa zikipotea bila kuleta maendeleo yoyote katika kata na vijiji husika.

Akizungumza katika baraza la madiwani diwani wa kata ya Tinga Tinga,Sabore Moimollet alisema kuwa wakati umefika sasa kwa halmashauri hiyo kupitia idara ya utumishi kuwafukuza kazi watendaji wa kata na vijiji ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua kali za kisheria.

Alisema kuwa watendaji wengi ni walevi na wamekuwa wakitumia fedha hizo vibaya kwa kuwa wanafahamu kuwa hakuna mkaguzi yeyote anayefuatilia akaunti hizo hali inayosababisha kuzorota kwa maendeleo ya vijiji,kata kutokana na fedha hizo kutoelekezwa katika kutatua kero mbalimbali zinazoikabili jamii.
Aidha alisema kuwa idara ya utumishi sasa ilifanyie  kazi swala hilo na kuhakikisha kuwa wakaguzi wanafuatilia akaunti hizo mara kwa mara ili kuhakikisha fedha hizo hazipotei bila sababu ya msingi na pindi ubadirifu unapojitokeza hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Longido, Lekule Laizer alisema kuwa ili kukabiliana na tatizo hilo madiwani wa halmashauri hiyo waorodheshe majina ya vijana waliomaliza elimu ya kidatp cha nne na sita wenye uwezo ili wakapitiwe mafunzo maalum ya uongozi na utawala ili wajengewe uwezo na kuweza kusaidia vijiji na kata zinazoizunguka halmashauri hiyo.

Alisema kuwa pindi vijana hao watakapopatiwa mafunzo hayo itawasaidia katika kufanya kazi kwa uadilifu hali ambayo itachangia kwa kiwango kikubwa maendeleo ya vijiji na kata hali ambayo itawasaidia halmashauri hiyo kupata maendeleo na hatimaye kutumia vizuri fedha hizo na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa vijiji na kata zilizopo katika wilaya hizo.

No comments: