Wachezaji wa Azam
Na Prince Akbar
MICHUANO ya Kombe la Urafiki, inayoandaliwa na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), inatarajiwa kuendelea leo kwa mchezo kati ya Super Falcon na Jamhuri ya Pemba kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Mechi nyingine ya kundi hilo, B ingekuwa kati ya Yanga na Zanzibar All Stars, lakini ZFA imeiengua Yanga kwenye michuano hiyo kwa kupeleka timu B, badala ya timu A.
Mechi za Kundi A zitaendelea kesho, kwa Azam kujaribu kusaka ushindi wa kwanza kwenye michuano hiyo mbele ya Mafunzo, baada ya kucheza mechi mbili za awali bila kushinda.
Mabingwa wa Tanzania Bara, Simba SC wao watakuwa mikononi mwa timu ambayo ni tishio kwenye michuano hiyo, Karume Boys. Mechi hizo za kesho ndizo zitaamua timu za kuingia Nusu Fainali kwenye Kundi hilo.
Karume ina pointi sawa na Simba SC, nne kila moja lakini inazidiwa bao moja la kufunga na Wekundu hao wa Msimbazi.
Katika mechi za Kundi A jana, Simba SC walishindwa kuwafunga Azam FC licha ya kucheza pungufu, baada ya kutoka sare ya 1-1.
Simba ilitangulia kupata bao dakika ya 35 kupitia kwa mshambuliaji wake iliyemsajili kutoka Dong Tam Long An ya Vietnam, Danny Mrwanda, lakini Azam ilisawazisha kupitia kwa George Odhiambo ‘Blackberry’ dakika ya 45.
Katika mechi hiyo, iliyokuwa kali nay a kusisimua, Abdulhalim Humud alipewa kadi ya pili ya njano na kuwa nyekundu dakika ya 52 na kutolewa nje, hivyo Azam kubaki pungufu ya mchezaji mmoja uwanjani.
Katika mechi yake ya kwanza, Simba SC ilianza vyema baada ya kuifunga Mafunzo mabao 2-1, wakati Azam ililazimishwa sare ya 1-1 na U23, Karume Boys.
Simba sasa inaongoza kundi hilo kwa pointi zake nne, mabao matatu ya kufunga na mawili ya kufungwa, wakati Mafunzo ni ya pili kwa pointi zake nne, mabao mawili ya kufunga na moja la kufungwa na Azam FC ni ya tatu kwa pointi zake mbili, wakati Mafunzo inashika mkia baada ya kufungwa mechi zote mbili.
No comments:
Post a Comment