Sunday, December 9, 2012

Umoja Wa Mataifa Wa Laumiwa Kwakushindwa Kuchukua Hatua Stahiki Kuzuia Mgogoro Wa Congo

UMOJA wa Mataifa (UN) umelaumiwa kwa kushindwa kuchukua hatua stahiki kuzuia na kumaliza kabisa mgogoro unaoendelea katika mji wa Goma,Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Shutuma hizo zimetolewa jana jijini Dar es Salaam na Rais Yoweri Museveni, ambaye pia ni mwenyekiti wa sekretarieti ya nchi za maziwa makuu,wakati wa mkutano wa Umoja wa Jumuiya za Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) uliojikita kuzungumzia migogoro ya Zimbabwe, Madagascar na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Rais Museveni alisema kuwa kitendo cha wanajeshi wa umoja wa mataifa wanaofikia 17,500 wa kulinda amani DRC Kongo kuwepo huko bila kuwa na uwezo wa kukabiliana na waasi wa M23 wanaoendesha operesheni zao katika mji wa Goma ambao wameuteka mji huo majuma mawili yaliyopita ni sawa na utalii wa kijeshi.
Akitoa historia ya mgogoro huo Museveni alisema kuwa ulianza toka wakati wa Rais wa zamani wa nchi hiyo wakati ikiitwa Zaire, hayati Mobutu Sseseko, na kueleza kuwa kwasasa unaendeshwa na vikundi alivyoviita vya kigaidi.
Museveni alisema kuwa mgogoro huo utaweza kutatuliwa kwa kutumwa kikosi cha pamoja cha nchi wananchama wa SADC na nchi za maziwa makuu kitakachokuwa na amri ya kukabiliana na uasi wowote katika eneo hilo.
Akifungua mkutano huo Rais Jakaya kikwete,ameziomba nchi jumuiya za SADC kukomesha migogoro iliyozikumba baadhi ya nchi hizo ili kuepusha maafa yanayoendelea kuwakumba wananchi.
Akizungumzia mgogoro wa Kongo, kikwete alisema kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi wanachama wa SADC pamoja na nchi nyingine ili kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

No comments: