Sunday, April 22, 2012

NANI WA KUINUSURU CCM

Jahazi La CCM Lazidi Kuzama ( Gazeti Mwananchi)

UPEPO wa wanachama wa CCM kujiunga na Chadema umezidi kushika kasi baada ya viongozi zaidi wa chama hicho na mamia wanachama kuhamia Chadema.  Viongozi wa CCM waliohamia Chadema  ni Wilaya ya Monduli, Wilaya za Sengerema, na Kikundi cha Kwaya cha Uhamasishaji wa chama hicho Wilaya ya Magu na mamia ya wachama kutoka katika maeneo hayo. 

Akizungumza na Mwananchi Jumapili kwa njia ya simu jana, Mwenyekiti wa Chadema, Wilaya ya Monduli, Amani Ole Selenga amesema chama chake kimepokea jumla ya wanachama 300 wa CCM katika kata mbili za Makuyuni na Mto wa mbu wilayani Monduli.  

Aliongeza kuwa wengi wa wanachama hao ni wajumbe wa serikali za vijiji na wajumbe wa nyumba kumi.
Kwa mujibu wa Ole Selenga, taarifa za wanachama hao kukimbilia Chadema zilimshtua Mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa na kudai kuwa mbunge huyo alipanga kurejea jimboni kuzima moto huo.
 
Mkoa wa Mwanza Katika hatua nyingine zaidi ya wanachama 95 wa CCM kutoka Wilaya za Magu na Sengerema wamerudisha kadi za CCM na kujiunga na Chadema jana.
 
Wanachama hao ambao kati yao, 45 ni wanakwaya maarufu ya uhamasishaji ya Ngómbe ya Magu ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikitumiwa katika kampeni kuhamasisha wananchi kuchagua CCM.
Akitangaza kujiunga wanakwaya hao, Katibu wa Chadema Magu, Bahati Simon alisema jana kuwa wamechukua uamuzi huo baada ya kuona CCM haijawaletea maendeleo wananchi wala wao wenyewe.
 
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana mjini Sengerema na kuhutubiwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa, wanachama 50 wa CCM walihama na kujiunga na Chadema.
Katika mkutano huo, diwani wa CCM Kata ya Lugata kutoka Wilaya ya Sengerema Adrian Tizeba, alitangaza kujiunga na Chadema.  Diwani huyo ambaye ni ndugu wa Mbunge wa Buchosa (CCM), Dk Charles Tizeba, alisema ameamua kuhamia Chadema kwa hiari yake mwenyewe  Diwani mwingine aliyehama CCM na kuingia Chadema ni Hamis Mwagao wa Kata ya Nyampulukano ambaye pia  Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya UVCCM, Wilaya ya Sengerema John Tungu.   Viongozi CCM Arusha waita Dar
 
Wakati hali ikiendelea kuwa tete, ndani ya CCM viongozi wa ngazi ya juu wa CCM Mkoa wa Arusha wameitwa makao makuu ya chama jijini Dar kueleza kinachoendelea mkoani humo.   Habari za uhakika kutoka ndani ya viongozi wa CCM, zimeeleza kuwa Katibu wa UVCCM Mkoa wa Arusha, Abdalah Mpokwa na Katibu wa Itikadi mkoani humo, Loota Sanare  Jumatano wiki hii, waliitwa ghafla makao makuu ya CCM na walitarajia kurejea jana jioni kwa ndege. 

 “Ni kweli kuna viongozi wameitwa haraka Dar es Salaam nadhani wametakiwa  ili kueleza kinachotokea Arusha,” alisema Kiongozi mmoja wa CCM ambaye jina lake linahifadhiwa.  Wakati viongozi hao wakiwa wameitwa Dar es Salaam, viongozi wengine wa CCM wa ngazi ya mkoa na wilaya, kuanzia juzi walikuwa katika wilaya za Ngorongoro katika kata za Enduleni, Longido na Monduli kufuatilia taarifa za viongozi na wanachama wao kuhamia Chadema.  

Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM, Mkoa wa Arusha, Sanare alikiri jana kuwa alikwenda jijini Dar es Salaam ghafla muda mfupi baada ya kurejea safari yake binafsi Nairobi, Kenya. Hata hivyo alikanusha kuitwa na viongozi wa juu wa CCM.  “Ni kweli nipo Dar es Salaam, lakini sipo kwa mambo ya CCM nina mambo yangu, haya mambo ya kuhama watu ni haki yao ila vyombo vya habari mnayakuza sana,” alisema Sanare.  Soma zaidi: http://www.mwananchi.co.tz

No comments: