Tuesday, September 17, 2013

KILA MBINU ITUMIKE KUONDOA JANGA HILI LA MADAWA YA KULEVYA, NI AIBU KWA TAIFA

KWANZA nimshukuru Mungu kwa kunipa afya siku hii ya leo na kunifanya niandike haya nitakayoyaandika nikiamini kwamba yatasaidia taifa langu.
Madawa ya kulevya.
Kila kukicha takwimu zinaonyesha kumekuwa kuna  wimbi kubwa la Watanzania wanaojiingiza katika biashara ya madawa ya kulevya ndani na nje ya nchi, na kwamba katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, jumla ya watuhumiwa zaidi ya elfu kumi wamekamatwa kwa kujihusisha na biashara hii haramu ya dawa hizo.
Naamini hicho ndicho kimeifanya serikali kuandaa sheria mpya ya madawa ya kulevya ili kuwabana wafanyabiashara hiyo haramu ambapo Waziri wa Nchi, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi wiki iliyopita alikutana na waandishi wa habari na kueleza mengi  na hasa kuhusu serikali kupitia Tume ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini, kwamba imeanza kutafuta muarobaini wa kumaliza sakata la usafirishaji wa madawa ya kulevya baada ya kuwaomba wadau mbalimbali kushiriki uchangiaji wa maoni ya kuboresha sheria mpya.
Mbali na hilo, Lukuvi alisema kuna mapendekezo ya kuunda chombo maalumu na kuanzisha mahakama maalumu ya kuendesha kesi za madawa ya kulevya ili kukomesha biashara hiyo nchini. Hili wazo ni zuri na niliwahi kupendekeza kupitia safu hii.
Inanihuzunisha na kunitia uchungu ninapoona kuwa katika kipindi cha miaka mitano, Watanzania 240 walikamatwa katika nchi za Brazil, Pakistani pamoja na Afrika Kusini wakihusishwa na madawa hayo, hali ambayo inafedhehesha na inaharibu kabisa taswira ya nchi na kusababisha Watanzania wasio na hatia kupata masharti magumu wanapotaka kusafiri kwenda nchi za nje kufanya kazi za ujenzi wa taifa.
Kinachonisikitisha zaidi ni kuona kuwa biashara hiyo haramu inashika kasi ya kutisha na sasa tunasikia hata wasichana wadogo wanaingizwa katika tanuri hilo la biashara ya madawa ya kulevya. Tulisikia jinsi  wasichana wawili Agnes Jerald
(25) pamoja na Melisa Edward
(24), ambao ni Watanzania wadogo walivyokamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo uliopo eneo la Kempton Park, Afrika Kusini wakiwa na dawa za kulevya aina ya Crystal Methamphetamine.
Kama vile hilo halitoshi, Watanzania wengine wawili walikamatwa huko Hong Kong wakiwa na dawa za kulevya aina ya cocaine na heroine zenye thamani ya Shilingi bilioni 7.6 akiwemo mmoja aliyekamatwa akitokea Dar es Salaam kupitia Dubai.
Inasikitisha kuona nchi yetu sasa imegeuzwa kuwa njia ya kusafirishia madawa ya kulevya kwenda nchi mbalimbali duniani, na kwa namna hali ya kushamiri kwa biashara hiyo kunavyoonekana, wanaofanikisha mikakati ya kupitisha mihadarati hiyo ni Watanzania wenyewe. Hapo nakumbuka usemi wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliposema kuwa mvunja nchi ni mwananchi.
Hii inadhihirika kwa kuwa kuna ushahidi kwamba wengi wao wanaokamatwa katika viwanja vya ndege huko ughaibuni ni Watanzania au baadhi yao walitokea hapa nchini.
Watanzania wengi wanaofanya biashara halali ya kwenda China, wanaonekana kuwa wanakwenda huko kubeba bidhaa za kibiashara, na nina uhakika kuwa wengi wao hawathubutu kuingia nchini China na madawa za kulevya kwa sababu wanafahamu adhabu zinazochukuliwa dhidi ya watuhumiwa wa biashara hiyo haramu ambayo ni kunyongwa mara moja kwa kupigwa risasi ya kisogoni.
China haina muda wa kumchunguza anayekamatwa na madawa ya kulevya ‘red handed’, bila kujali mtuhumiwa anatokea nchi gani ndiyo maana nasema ipo haja ya kurekebisha sheria ili adhabu ziwe kali na mizizi ipatikane.
Naungana na Waziri Lukuvi kusema kwamba adhabu zilizopo kwenye sheria ya sasa haziwaogopeshi wafanyabiashara ndiyo sababu ya kuongezeka kwa biashara ya madawa ya kulevya.
Nitakuwa sijatenda haki kama sitachukua japo nafasi kidogo kumsifu Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, kwa kazi yake nzuri kuhusu vita hii ambayo hakika ni ya Watanzania wote, mimi na wewe bila kujali una wadhifa gani katika nchi hii.
Dk.  Mwakyembe alionyesha njia pale katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere baada ya kuwataja maofisa usalama wanne wanaodaiwa kuhusika katika njama za kupitisha madawa ya kulevya. Pamoja na kuwataja wahusika hao, akaiagiza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) wafukuzwe kazi, wakamatwe na kufunguliwa mashtaka mahakamani.
Ki ukweli wote hao wangekuwa China, wakathibitika kuwa walijihusisha wangejikuta wakipigwa risasi ya kisogoni mara moja! Dk. Mwakyembe amefanya alichokifanya kwa ujasiri mkubwa  jambo linaloonekana kuwa  gumu kwa baadhi ya viongozi hapa nchini.
 Ipo haja kuwatafuta vigogo wanaohusika na biashara hiyo haramu kwa sababu wanaua taifa kwa kuwafanya vijana wanaotumia madawa hayo kuwa mazezeta.
Hakuna Mtanzania asiyejua kuwa biashara ya madawa ya kulevya imelaaniwa na kila taifa duniani kutokana na madhara yake katika jamii. Utajiri unaotokana na dawa za kulevya huangamiza nguvu kazi ya vijana na kupotosha maadili ya taifa.
Ni wajibu wetu sasa kuungana kama taifa kuhakikisha biashara hii haramu inakufa, tena haraka sana, tuweke sheria kali na wote kwa ujumla wetu tushirikiane kuwafichua vigogo hao wa unga kwa sababu hawaishi mbinguni.
Nasema hivyo kwa sababu biashara hii imeichafua nchi  na kuitia aibu kubwa kimataifa, hali hii ikiendelea tunaweza kutengwa na jamii ya kimataifa kutokana na tamaa ya watu wachache wanaowafanya vijana wetu mazezeta.
Jipu limepasuka ziwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

No comments: