Wednesday, August 20, 2014

Ajali mbaya sana: Mabasi ya Sabena na A.M. Dreamline yagongana uso kwa uso

Hali ni tete sana eneo la Mkolye, takribani km 4 toka Mjini Sikonge baada ya basi la Sabena toka Mbeya kwenda Mwanza na basi la A.M. toka Tabora kwenda Katavi kugongana uso kwa uso (head on collision).

Dreva wote wa mabasi hayo wamefariki hapo hapo, mmoja akiwa amekatika kichwa!

Nimeshuhudia abiria kadhaa wakiwa wamenasa ktk mabasi hayo, baadhi wakiwa wamekatika mikono na miguu!

Nitaweka picha muda si mrefu, lakini ni hatari saaaana ndugu zangu!

Abiria wapatao watano wamefariki hapo, na majeruhi zaidi ya 30 wamepelekwa ktk Hospitali ya Mission ya wilayani Sikonge.
Sorry, kazi ni kubwa kweli kweli! Robo tatu ya basi la Sabena imebonyea kwa kubamizwa na basi la A.M, nikimaanisha seat zote kuanzia kwa dreva hadi nyuma(3/4) kwishney!
Niko busy na ki-pick up changu tunasaidia kupeleka maiti na majeruhi hospital. Picha baadae wakuu. Ni hatari sana I see!

Wananchi wakiangalia mabasi mawili yaliyogongana uso kwa uso eneo la Mkolye, nje ya mji wa Sikonge, mkoani Tabora jana,
iliyohusisha basi la Sabena toka Mbeya kwenda Mwanza na basi la A.M. toka Tabora kwenda Katavi.
Na Mpiga picha Wetu na Robert Kakwesi, Mwananchi


Kwa ufupi
Inasemekana kuwa idadi ya waliofariki ni kubwa kutokana na mabasi hayo kung’ang’aniana na Sabena likiwa limeharibika zaidi kwa kupondeka karibu nusu yake.


Tabora.Zaidi ya watu 16 wamefariki dunia baada ya mabasi mawili kugongana uso kwa uso jana saa 9:30 alasiri umbali wa kilomita tatu kutoka Sikonge.

Basi la Sabena likitokea Mbeya kwenda Tabora liligongana uso kwa uso na jingine la AM Coach lililokuwa likitoka Tabora kwenda Mbeya.

Miongoni mwa waliofariki dunia, ni dereva wa Sabena aliyefahamika kwa jina moja la James ambaye kichwa chake kilitengana na kiwiliwili na hadi jana jioni kilikuwa kikitafutwa katika eneo la ajali.

Dereva wa AM Coach alikuwa amekwama kwa zaidi ya saa mbili ndani ya basi hilo na hadi tunakwenda mitamboni, jitihada za kumtoa kwa kukata basi zilikuwa zikiendelea.

Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Dk John Buswelu alisema hadi jana saa 12:30, walikuwa wamepokea maiti 16 kutokana na ajali hiyo na majeruhi 75 kati yao wanaume 45 na wanawake 30.

Inasemekana kuwa idadi ya waliofariki ni kubwa kutokana na mabasi hayo kung’ang’aniana na Sabena likiwa limeharibika zaidi kwa kupondeka karibu nusu yake.

Majeruhi wengi walikuwa wamevunjika viungo mbalimbali ambavyo baadhi vilionekana vikiwa vinatolewa kwenye mabasi hayo.

Mmoja wa abiria aliyenusurika kwenye ajali hiyo, Nuru Mtafya aliyekuwa amepanda Sabena kutoka Mbeya akielekea Shinyanga, alisema:

“Tulikuwa tumeongozana na basi la Sasebosa na kulikuwa na vumbi jingi, hivyo dereva wa AM alishindwa kuliona basi letu.”

Abiria mwingine Ally Hamis, alisema alikuwa ameanza kusinzia baada ya kutoka Sikonge na kuamshwa na kishindo kikubwa na vilio vya watu... “Ninachoweza kusema nimepona kutokana na kukaa nyuma kabisa ya basi, vinginevyo nisingetoka mzima.”

No comments: