ASHURA MOHAMED-ARUSHA
Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) itatoa hukumu ya kesi inayomkabili afisa wa zamani wa jeshi la Rwanda, Kapteni Idelphonse Nizeyimana Juni 19, 2012, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mahakama hiyo Ijumaa.
Nizeyimana anakabiliwa na mashitaka ya mauaji ya kimbari, kuteketeza kizazi, mauaji na ubakaji.
Mwendesha mashitaka pamoja na mambo mengine anadai kwamba mshitakiwa alikuwa mtu wa pili kimadaraka aliyekuwa anashughulikia Usalama na Operesheni za Kijeshi katika Chuo cha Maafisa wa Jeshi Wasiokuwa na Kamisheni (ESO), mkoani Butare, Kusini ya Rwanda.
Nizeyimana anadaiwa kuamuru, kusimamia na kupanga mauaji dhidi ya Watutsi katika maeneo mbalimbali mkoani humo ikiwa ni pamoja na mauaji dhidi ya Malkia wa Kitutsi, Rosalie Gicanda Aprili 21, 1994.
Katika kuwasilisha hoja za mwisho Desemba 7, 2011, mwendesha mashitaka aliiomba mahakama iliyokuwa inaongozwa na Jaji Lee Muthoga, kumpatia adhabu ya juu kabisa inayoweza kutolewa na mahakama hiyo ya kifungo cha maisha jela iwapo atatiwa hatiani.
‘’Adhabu pekee muafaka kwa mujibu wa mwendesha mashitaka ni kumpatia kifungo cha maisha jela ,’’ alipendekeza Mwendesha Mashitaka, Drew White.
White pia hakulifumbia macho suala la madai ya kuhusika kwa mshitakiwa katika mauaji dhidi Malkia wa Kitutsi, Rosalie Gicanda kwa kueleza kwamba, mashahidi wawili wa kuaminika wa upande wa mwendesha mashitaka walitoa ushahidi wao akiwemo mjukuu wake na mpishi.
Hata hivyo, John Philpot, Wakili Kiongozi wa Nizeyimana alipangua hoja za mwendesha mashitaka kwa kusema kuwa ameshindwa kuthibitisha mashitaka dhidi ya mteja wake pasipo mashaka. Alisema kwamba mteja wake alichukua hatua sahihi zilizopaswa kuchukuchukiwa na askari nyakati za vita.
‘’Mteja wangu hakuwa kiongozi wa ESO, hakuwa na mamlaka kamili na hakuwa na mamlaka ya kisheria juu ya askari waliodaiwa kuwa chini ya himaya yake,’’ alisema wakili huyo.
Pia wakili huyo aliwasilisha ushahidi wa kuwa mteja wake wakati fulani hakuwepo katika maeneo yalikofanyika uhalifu kwenye miezi ya Aprili na Mei, 1994 bali muda huo alikuwa katika kiwanda cha Chai cha Mata, mkoani Gikongoro akiendesha mafunzo ya kijeshi kwa askari wapya.
‘’Kesi hii sasa iko mikononi mwenu. Tunawaomba kusimama katika ukweli na haki kumwachia huru Nizeyimana,’’ Nizeyimana aliwaomba majaji alipokuwa anakamilisha kuwasilisha hoja zake za mwisho.
Nizeyimana alitiwa mbaroni nchini Uganda, Oktoba 5, 2009 na kuhamishiwa katika gereza la Mahakama ya Umoja wa Mataifa Arusha, Tanzania, siku iliyofuata. Alikana mashitaka dhidi yake alipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Oktoba 14, 2009.
Kesi yake ilianza kusikilizwa Januari 17, 2011 ambapo mwendesha mashitaka aliita mashahidi 38 na upande wa utetezi pia uliita idadi sawa na hiyo na kufunga kesi yake Februari 25, 2011.
No comments:
Post a Comment