Thursday, May 17, 2012

MANJI AWAPA MASHARTI YANGA KUREJESHA UDHAMINI

YUSSUF Mehboob Manji (pichani kushoto), ameibuka tena Yanga, baada ya kimya cha muda mrefu akijitokeza kwa nia ya kuokoa jahazi kutokana hali mbaya ya kiuchumi inayoikabili klabu kwa sasa.
Waajiriwa wa Yanga, wakiwemo makocha, wachezaji na watendaji hawajalipwa mishahara kwa takriban miezi minne, hali inayoashiria uongozi wa klabu hiyo, chini ya Mwenyekiti wake, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga umeelemewa.
Lakini mfanyabiashara kijana anayemiliki mamilioni ya fedha, Manji yu tayari kuokoa jahazi kwa kurejesha udhamini katika klabu.
Hata hivyo, ili kurejea kuidhamini Yanga, Manji ametoa masharti matano.
Masharti hayo ni; kufanyika uhakiki wa mahesabu ya akaunti za Yanga ndani ya siku 90 na wakaguzi wa hesabu wa kujitegemea kukagua hesabu za kipindi cha kuanzia mwaka 2006 hadi 2012 kwa ajili ya fedha zilizoingia klabuni.
Sharti la pili ni kuchapishwa magazetini kwa akaunti za Yanga siku 15 baada ya kumalizika kwa robo ya mwaka, tatu ni
kuendeshwa zoezi la kura ya maoni ndani ya siku  60 na kuamua kama wanachama wa Yanga wanataka klabu iwe Yanga au la na sharti la nne ni mabadiliko ya Katiba ndani ya siku 90.
Kwa mujibu wa barua ya Manji kwa Mwenyekiti wa Yanga, Nchunga ambayo BIN ZUBEIRYimeipata nakala yake, ameutaka pia uongozi kuidhinisha mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa klabu, nafasi ambayo iko wazi baada ya Davis Mosha kujiuzulu mwaka jana.
Sharti la mwisho la Manji ni kutaka kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa wanachama ndani ya siku 30, ili kujadili mustakabali wa klabu.

No comments: