Sunday, August 19, 2012

Taarifa Kwa Umma




JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII TAARIFA KWA UMMA

WATU WALIOVAMIA PORI TENGEFU LA KILOMBERO WAMETAKIWA KUONDOKA IFIKAPO TAREHE 31 AGOSTI 2012

Watu waliovamia na kuishi katika Pori Tengefu la Kilombero wametakiwa kutoka kwenye eneo hilo kwa hiari yao kabla ya tarehe 31 Agosti 2012. Watu hao ni wale ambao hawajaondoka baada ya kutakiwa kufanya hivyo mara kwa mara.

Azimio hilo lilifikiwa katika kikao cha pamoja kati ya uongozi wa Wilaya za Kilombero na Ulanga na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bibi Maimuna Tarishi kilichofanyika Kilombero tarehe 14 Agosti 2012. Nia ya kikao hicho ilikuwa ni kuweka mikakati ya kutekeleza azama ya Serikali ya kuwataka wavamizi katika Pori Tengefu la Kilombero kuondoka katika eneo hilo.

Wengine waliohudhuria kikao hicho ni Ni Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Francis Miti, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilombero Evarist Mmbaga, Mtendaji wa Wilaya ya Kilombero, Azimina Mbilinyi na watendaji wengine kutoka Wilaya za Kilombero na Ulanga.

Kikao hicho kiliamua kuwa ifikapo tarehe 8 Septemba, 2012 kazi ya kuwatoa wavamizi ambao bado watakuwepo katika pori hilo itaanza. Kazi hiyo ya kuwaondoa itatekelezwa kwa pamoja na Kamati za Usalama ngazi ya Mkoa na Wilaya za Ulanga na Kilombero, Kikosi Dhidi ya Ujangili, Askari Polisi na Askari kutoka Pori la Akiba Selous.

Hadi sasa wanachi wameelimishwa kuhusu umuhimu wa Pori Tengefu la Kilombero na manufaa yatakayopatikana kama litaachwa wazi. Wanavijiji wanaopakana na Pori hilo wameonyeshwa mipaka baina ya vijiji vyao na Pori.

Aidha mipango imekamilika ya kuiwekea mifugo alama (brandas) kwa lengo la kuweka mipango bora ya matumizi ya ardhi katika vijiji vilivyoko katika Bonde la Kilombero. Kazi hii inaratibiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Vilevile kazi ya kutambua mipaka, kufyeka, na kuweka alama (beacons) zinaendelea kwa pamoja katika vijiji 105 vya Wilaya za Ulanga na Kilombero na zinategemewa kukamilika tarehe 27 Agosti, 2012. Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na utalii aliahidi kuwa Wizara itachangia Shs. 106,500,000 ili kuharakisha utekelezaji wa kazi hiyo ya kuimarisha mipaka.Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii amevitaka Vijiji vinavyopakana na Pori hilo kuanzisha Jumuiya za Kuhifadhi Wanyamapori (WMA) ili kuimarisha ulinzi wa hifadhi hiyo dhidi ya wavamizi. Pia, kupitia WMA jamii husika zitapata manufaa kiuchumi kutokana na matumizi ya rasilimali za wanyamapori zilizopo.

Vilevile kila kijiji kimetakiwa kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi ambao, pamoja na mambo mengine, utaonyesha maeneo ya malisho ya mifugo.

                             George Matiko
    MSEMAJI WIZARA YA MALIASILI NA UTALII

No comments: