Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage akizungumza na baadhi ya wanachama wa klabu hiyo wa tawi la Wekundu wa Terminal Ubungo jijini Dar es Salaam leo. (Picha na habari Mseto Blog)
Baadhi ya wanachama wa tawi hilo wakimsikiliza Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage
Akuffo, Ochieng kwa heri Simba
>>Rage
amwaga cheche, amrejesha Hanspope
>>Amtangaza rasmi Julio, Prof Maji
Marefu naye aula
Na Clezencia Tryphone
WAKATI mzimu wa kufanya vibaya kwenye Ligi Kuu Bara mabingwa watetezi Simba, ukiwa unaiandama klabu hiyo, Mwenyekiti wake, Ismail Aden Rage ametangaza kuachwa kwa nyota wa kimataifa, Daniel Akuffo na Paschal Ochieng.
Rage aliyabainisha hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na wanachama wa Tawi la Simba la Wakali wa Terminal ‘Mwanzo Mwisho’ kuhusiana na mustakabali wa klabu hiyo ambayo hivi karibuni ilikumbwa na mtafaruku kutokana na kumaliza mzunguko wa kwanza wa ligi ikiwa nafasi ya tatu, baada ya kuongoza kwa muda mrefu.
Mwenyekiti huyo alisema, tayari wamemalizana Mghana Akuffo huku wakiwa katika mchakato wa mwisho kumuondoa Ochieng. Nyota hao ambao walisajiliwa msimu huu, wameshindwa kuonesha uwezo.
Pia Rage ambaye hivi karibuni alizifuta Kamati ndogondogo zote, alisema, amemteua Zakaria Hanspope kuwa Mwenyekiti Kamati ya Usajili akisaidiana na Mbunge wa Korogwe Vijijini, Steven Ngonyani maarifi kama, Profesa Majimarefu, huku wajumbe wakiwa ni wafanyabiashara maarufu, ili waweze kuiinua Simba. Alimsifu Hanspope, kwa kujitolea fedha zake mfukoni bila ya kuhitaji kutajwa.
Mwenyekiti huyo, pia alifafanua kuwa, alimuomba radhi Nahodha wa timu hiyo, Kipa Juma Kaseja kwa kitendo cha mashabiki kumtukana katika mechi na Mtibwa ambayo walilala 2-0 na kuwa, hawana mpango wa kumuondoa labda atake yeye kwanza, kwani licha ya kuwa mchezaji wao ni mwanachama halali wa Simba na ana kadi ya uanachama.
Aliwaeleza wanachama hao kuwa, pia wamefanya mabadiliko benchi la ufundi, ambako Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ atakuwa Meneja na Kocha Msaidizi pamoja na Mganda Amate, huku kuhusiana na Kocha Mkuu akidai atalizungumza siku nyingine, ambako wanachama wakadakia wakisema, tunamtaka Babu asiondoke, huku Rage akijibu Simba oyee na wanachama hao kuitikia tano bila.
Rage ambaye pia ni Mbunge wa Tabora Mjini, alitamba kuwa, mzunguko ujao watampiga mtani wao Yanga, ‘hamsa’ kama sio sita.
Kuhusiana na klabu kujiendesha, alisema inatumia sh mil 50 kwa mwezi kwa ajili ya mishahara na kuwa, mdhamini hatoi hata nusu yake na kuwa, Simba ina uwezo wa kujisimamia kwa asilimia 92, kwa kuwa toka wameingia madarakani Mei 31, 2010 walikuta haina umeme, madirisha na wao wamehakikisha wamelipa na kuweka vioo vya giza, ‘tinted’ na kwa sasa wameboresha maduka yao.
Akilizungumzia Tawi la Mpira Pesa, ambalo linataka mkutano wa dharura,
Alisema, kwa wameamua kumwaga ugali wao wamemwaga ugali, ambako limesimamishwa kwa miaka miwili ili waweze kuwa na nidhamu zaidi watakaporejea na kusisitiza hakuna tawi lolote ambalo liko juu ya klabu.
Alimaliza kwa kudai kuwa, leo wanatarajia Kamati ya Utendaji kukutana na Bodi ya Wadhamini kujadili mambo mbalimbali, huku akiruhusu maswali kwa wanachama hao huku akiwataka wanachama kuwa na utaratibu wa kumuita mara kwa mara na si kusubiri migogoro. Katika maswali hayo, wanachama wengi walitaka kujua hatma ya Kocha Mkuu, Milovan Cirkovick, ambako aligoma kabisa kulizungumzia kwa sasa .
No comments:
Post a Comment