MENGI yamesemwa na yanaendelea kusemwa kwamba, mpaka kifo chake, Marehemu Steven Charles Kanumba ‘The Great’ alikuwa mwanachama wa imani ya Freemason (wajenzi huru) ambayo inashika kasi katika nchi za Kiafrika, lakini mama wa marehemu, Flora Mtegoa ametoa tamko juu ya tuhuma hizo za mwanaye.
Akizungumza na waandishi wetu hivi karibuni nyumbani kwa marehemu Kanumba, maeneo ya Vatican City Hotel, Sinza jijini Dar, mama Kanumba alisema amesikia kuwa mwanaye alikuwa muumini wa imani hiyo yenye utata duniani.
Lakini akasema: “Namjua Kanumba, alikuwa mwanangu, mambo yake mengi nilikuwa nayajua maana tulikuwa tunaishi kama marafiki, habari hizo si za kweli.
“Watu wanasema sana, sijui wanatumia vigezo gani? Mwanangu alikuwa muumini mzuri sana wa Kanisa la African Inland Church (AIC), sasa huo u-Freemason aliuchukulia wapi?”
“Huo ni uzushi uliopitiliza,” alisema mama Kanumba.
VIGEZO VYA WATU MITAANI
Wengi mitaani wamekuwa wakisema baadhi ya picha za marehemu Kanumba zilionesha viashiria vya kuwa mfuasi wa imani hiyo ambayo mpaka sasa Watanzania wengi hawaijui vizuri.
KIGEZO CHA PICHA
Zipo baadhi ya picha ambazo marehemu Kanumba anaonekana akiashiria alama za Freemason. Mfano, kuna picha ambayo mkono wake wa kulia ameweka vidole mfano wa pembe za mbuzi.
SUTI YA MAZISHI
Miongoni mwa magumzo yaliyotikisa siku ya kuuaga mwili wake ni suti nyeusi aliyovalishwa ambapo upande wa kushoto wa koti kuna nembo inayotafsiriwa ni ya Freemason.
Waandishi wetu waliwasiliana na mama wa marehemu na kumuuliza nani aliyemvisha koti hilo, yeye alijibu kwa kifupi:
“Sijui ni nani?”
KASI YA MAFANIKIO
Kigezo kingine ambacho baadhi ya watu wamekuwa wakikiamini kwamba marehemu alikuwa muumini wa dini hiyo ni kasi ya mafanikio yake.
Kwa sababu hiyo, baadhi ya watu wakasema kuwa wamesikia mtu anapokuwa Freemason anawezeshwa kwenye shughuli zake kwa kuwa na bahati ya kutajirika.
MVUTO NAO WATAJWA
Baadhi ya watu wamekuwa wakitaja mvuto aliokuwa nao marehemu kwamba nao ni dalili tosha kuwa alikuwa kwenye imani hiyo.
Wengi waliodai wana elimu kuhusu Freemason walisema kuwa, mara nyingi mwanachama wao hupoteza maisha wakati nyota yake ikiwa inawaka sana.
Walitoa mfano wa marehemu Pepe Kalle, kwamba alipotoa albamu ya Cocktail aliwika sana na ndipo alipoaga dunia ghafla.KANUMBA NA MASTAA WENGINE
Bado wengi wanazidi kuamini kifo cha ghafla cha Kanumba kinafanana na cha maarufu wengine duniani, marehemu Michael Jackson ‘The Jacko’, Whitney Houston na Madilu System ambao pia walihusishwa na u-Freemason.
RAMSEY NOAH ANYOOSHEWA KIDOLE
Watu hao wanaopepeta huko mitaani kuwa marehemu Kanumba alikuwa muumini wa imani hiyo walizidi kuibua mapya ambapo wanaamini nyota wa filamu za Nollywood (Nigeria), Ramsey Noah naye ni mwanachama wa dini hiyo.
Wakadai mcheza filamu huyo alikuja Bongo na kucheza na Kanumba Filamu ya Devil’s Kingdom ambayo sehemu kubwa ya stori ni maisha ya imani ya Freemason.
“Mimi nina wasiwasi na Noah (Ramsey), yule jamaa nasikiasikia naye ni muumini, sasa alikuja hapa kwetu (Tanzania) akacheza na marehemu filamu ya Devil’s Kingdom, huenda alimuingiza mwenzake kwenye imani hii,” alisema Rukia, mkazi wa Ubungo Kibangu jijini Dar.
Ili kunogesha habari hizo, ilidaiwa kuwa baadhi ya waigizaji wa filamu hiyo akiwemo Ramsey mwenyewe walipatwa na masahibu ambapo ukiacha Kanumba aliyefariki, staa huyo wa Nigeria alipata ajali huku Kajala Masanja akisota Segerea hivyo inawezekana walibumburua siri za Freemason kupitia Devil’s Kingdom, jambo ambalo waumini wa imani hiyo hawakulipenda.Hakuna muda maalumu ambao mtu amepangiwa kupata utajiri, umaarufu au ushawishi hivyo sisi tumejaribu kuwasilisha kile kinachosemwa mitaani ambapo tunaamini mama mzazi wa marehemu Kanumba amemaliza utata hivyo mjadala huo umefungwa rasmi.
Chanzo na global publishers
No comments:
Post a Comment