Na. Zitto Kabwe.
UTANGULIZI
Julai 13, 2012 Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliwasilisha Maoni yake kuhusu Mpango na Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Pamoja na mambo mengine, Maoni ya Kambi yalihusu utaratibu wa uteuzi wa majaji wa Mahakama ya Tanzania.
Maoni ya Kambi yalizua mjadala mkubwa ndani na nje ya Bunge huku wachangiaji wengi wakimtuhumu Msemaji wa Kambi kwa “kuidhalilisha” Mahakama na/au “kuwadhalilisha majaji” (Gosbert Blandes-Karagwe CCM); “kuwavunjia heshima majaji” (Naibu Spika Job Ndugai); kuwatukana na kuwadhalilisha majaji (Murtaza Mangungu-Kilwa Kaskazini); “kuwa-offend, kuwadhalilisha na kuwanyanyasa majaji” (Assumpter Mshama-Nkenge CCM); “kufedhehesha Mahakama na majaji” (Mwanasheria Mkuu wa Serikali Frederick Werema).
Aidha, Msemaji wa Kambi alishambuliwa kwa kudaiwa kuwa mfitini na asiye na akili timamu (Muhammad Chomboh- Magomeni CCM)); na “kujiamini kwamba yeye anajua zaidi kuliko watu wengine wote” (Mangungu). Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe alilihakikishia Bunge kwamba “... haijatokea hata siku moja katika nchi hii Rais akamteua Jaji wa Mahakama Kuu bila kuzingatia mapendekezo yaliyopelekwa kwake na hii Tume ya Uajiri wa Mahakama.” Zaidi ya hayo, “... labda Mheshimiwa Lissu anamjua Jaji angalau mmoja na anaweza akamtaja aseme Jaji huyu ametolewa tu mitaani na Mheshimiwa Rais, yupi hakuna… hawa majaji wote walioteuliwa wamepitia mchakato huu wa kikao kizito sana cha watu ambao ndiyo wenye sheria ya nchi hii.”
Baadaye Msemaji wa Kambi alitakiwa kufuta kauli yake kuhusu uteuzi wa majaji usiofuata utaratibu uliowekwa na Katiba. Msemaji wa Kambi alikataa kufuta kauli hiyo ambako Mwenyekiti wa Kikao alielekeza Msemaji wa Kambi apelekwe kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa hatua zaidi. Alichukua uamuzi huo ili masuala hayo yapatiwe ufafanuzi ili wananchi wapate picha kamili na ya kweli kuhusu jambo hili muhimu. Maelezo haya yana lengo la kutoa ufafanuzi huo.
Katika maelezo yake kwa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya BUnge, Lissu alisema, “Nitajitahidi kwa kadri inavyowezekana kutoa ushahidi unaothibitisha kwamba siyo tu kwamba utaratibu wa kikatiba katika uteuzi wa majaji umekiukwa mara nyingi, bali pia majaji wengi walioteuliwa kwa utaratibu wa nje ya Katiba wamekuwa hawana ‘uwezo, ujuzi na kwa kila hali hawakufaa kukabidhiwa Madaraka ya Jaji wa Mahakama Kuu.”
TATIZO LA MUDA MREFU
Kuna ushahidi mkubwa kuthibitisha kwamba kuna watu wameteuliwa kuwa Majaji wa Mahakama Kuu “... wakiwa wamekaribia muda wao wa kustaafu kwingineko katika utumishi wa umma (na) wanapewa ‘zawadi’ ya ujaji ili kuwawezesha kupata mafao ya majaji wastaafu ambayo yameboreshwa sana katika miaka ya karibuni.” Ni muhimu kuweka wazi hapa kwamba utamaduni huu haukuanza baada ya Rais Jakaya Kikwete kuchaguliwa kuwa Rais, bali ni tatizo la muda mrefu. Kwa mfano, marehemu Jaji Kulwa Masaba na Jaji Madina Muro na majaji Stephen Ihema, Juxton Mlay, Augustine Shayo na Vincent Lyimo waliteuliwa majaji wa Mahakama Kuu baada ya utumishi wa muda mrefu kwingineko katika utumishi wa umma.
Majaji Masaba na Muro waliteuliwa huku wakiwa wagonjwa mahututi na – kwa kadri ninavyofahamu - hawakuwahi kuandika hukumu hata moja kabla ya mauti kuwafika! Jaji Lyimo aliteuliwa Machi 28, 2007 mwaka mmoja kabla ya muda wake wa kustaafu kwa mujibu wa sheria. Hata hivyo, ilipofika Oktoba 26, 2007 Katibu Mkuu Kiongozi wakati huo Phillemon Luhanjo alimtaarifu Jaji Mkuu kwamba Rais Kikwete “... ameamua kusogeza mbele muda wa kustaafu wa Mheshimiwa Jaji Vincent Kitubio Damian Lyimo kwa miaka mitatu kuanzia Machi 28, 2008 siku ambayo angestaafu kwa lazima”!
Kwa upande wao, Majaji Ihema, Mlay na Shayo walijizolea umaarufu kwa kuwa majaji wasioandika hukumu na hivyo kuwa wacheleweshaji wakubwa wa kesi katika Mahakama Kuu. Jaji Ihema alitia fora kwenye jambo hili kiasi kwamba Juni 16, 2003 Mwenyekiti wa sasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Mzee Joram Allute, alilazimika kumwandikia Rais Benjamin Mkapa maombi ya kumwondoa Jaji Ihema kama Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania “kwa uzembe na kukosa maadili.”
Mzee Allute alikuwa na kesi kwa Jaji Ihema ambapo Jaji huyo ‘alikalia’ uamuzi kwa zaidi ya miaka minne hadi aliponyang’anywa faili la kesi hiyo na kukabidhiwa Jaji mwingine aliyeandika uamuzi ndani ya wiki tatu! Mwezi mmoja kabla ya barua ya Mzee Allute kwa Rais Mkapa, mawakili wake walikuwa wamemwandikia Jaji Mkuu Barnabas Samatta kulalamikia ucheleweshaji wa uamuzi wa kesi hiyo. Mawakili hao walidai: “Hadhi na heshima ya Mahakama inaporomoka vibaya kama inachukua zaidi ya miaka mitatu kwa Jaji kutafakari na kutoa uamuzi kwa jambo jepesi kama maombi ya pingamizi.” Licha ya malalamiko haya dhidi yake, Jaji Ihema alipatiwa mkataba wa ajira wa miaka miwili mara baada ya kustaafu mwaka 2005.
MAJAJI WA MIKATABA
Agosti 2, 2005 Jaji Kiongozi Hamisi Msumi alitoa taarifa kwa majaji wote wa Mahakama Kuu kwamba Jaji Ihema alikuwa amepewa mkataba mpya baada ya kustaafu kama Jaji wa Mahakama Kuu. Taarifa hiyo ilimfanya Jaji Bernard Luanda, wakati huo Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, kuhoji ‘Uhalali Kikatiba kwa Majaji Kufanya Kazi kwa Mkataba Baada ya Kustaafu.’ Katika taarifa yake kwa Jaji Kiongozi Msumi, Jaji Luanda alisema kwamba “... suala la majaji kupewa mikataba ... linaenda kinyume na Katiba.” Jaji Luanda alifafanua: “Kwa kuwa Jaji amestaafu, basi kiapo chake nacho kimeondoka. Kwa bahati mbaya hawaapishwi ili washike kazi hizo za ujaji.... Ni hoja yangu kwamba Majaji waliostaafu na kupewa mikataba si Majaji kwa mujibu wa Katiba.”
Msimamo wa Jaji Luanda uliungwa mkono mwaka mmoja baadaye na Jaji wa Rufaa, Augustino Ramadhani wakati huo akiwa Kaimu Jaji Mkuu. Katika ‘Mawazo Kuhusu Vifungu Vinavyohusu Mahakama na Majaji’ aliyomwandikia Jaji Mkuu Samatta na kunakiliwa kwa Majaji wa Rufaa wote, Jaji Ramadhani alisema kwamba “... sio sahihi kwa Jaji Mkuu kustaafu na kupewa mkataba wa kuendelea na wadhifa huo kupindukia umri wa miaka 65 (ambao ndio umri wa kustaafu kwa lazima kwa Jaji wa Rufaa na Jaji Mkuu).” Baadaye Jaji Luanda aliteuliwa kuwa Jaji wa Rufaa wakati Jaji Ramadhani alikuja kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania.
Kauli ya Kambi kwamba kuna ukiukaji mkubwa wa Katiba kuhusiana na uteuzi wa majaji inaungwa mkono na nyaraka za ndani ya Serikali na hasa Ofisi ya Rais, Ikulu yenyewe. Desemba 6, 2007, mkutano kuhusu ajira ya majaji waliostaafu ulifanyika Ikulu, Dar es Salaam chini ya uenyekiti wa Katibu Mkuu Kiongozi Luhanjo. Wajumbe wengine walikuwa pamoja na Mwanasheria Mkuu Johnson Mwanyika na Naibu wake Sazi Salula, Katibu Mkuu Utumishi George Yambesi, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Sophia Wambura na Susan Mlawi wa Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri.
Kwa mujibu wa Kumbukumbu za Mkutano huo, “kwa utaratibu unaotumika sasa, baadhi ya Majaji wanaofikisha umri wa kustaafu kwa mujibu wa Ibara ya 110(1) kwa Majaji wa Mahakama Kuu na Ibara ya 120(1) ya Katiba wanaongezewa muda wa kuendelea na utumishi wao kwa mkataba baada ya wao kuwasilisha maombi rasmi.” Baada ya mjadala juu ya jambo hili, wajumbe wa mkutano walikubaliana kwamba “utaratibu wa kuongeza muda kwa njia ya mkataba unakiuka masharti ya Katiba na kuleta mkanganyiko kama Majaji hao wanastahili kulipwa mshahara au pensheni au vyote kwa pamoja.”
Matokeo ya mkutano wa Ikulu ilikuwa ni kuundwa kwa ‘Kikundi Kazi kwa Ajili ya Kuchambua na Kushauri Kuhusu Ajira ya Majaji Baada ya Kustaafu’ chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Kikundi Kazi kiliwasilisha Taarifa yake Machi 7, 2008. Katika Taarifa yake Kikundi Kazi kinakubaliana na msimamo wa kikatiba kwamba “kwa kuzingatia Ibara za 110 na 120 za Katiba inaonekana wazi kuwa suala la ajira za mikataba kwa Majaji ambao wamekuwa wakifanya kazi za Jaji baada ya kufikia umri wa kustaafu ni kinyume cha Katiba.” Kwa mujibu wa Taarifa hiyo, hadi mwezi Machi 2008, “... walikuwepo Majaji wawili ... wa Mahakama ya Rufani na Majaji tisa ... wa Mahakama Kuu, ambao wapo katika ajira za mkataba, na Jaji mmoja ... wa Mahakama Kuu aliyeongezewa muda wa ajira kwa mujibu wa masharti ya Katiba....”
Hii ina maana kwamba, kulikuwa na Majaji kumi na moja ambao walikuwa wanafanya kazi kinyume cha Katiba na – kwa maneno ya Jaji wa Rufaa Luanda – hawakuwa Majaji kwa mujibu wa Katiba! Aidha, kwa mujibu wa ushahidi wa nyaraka hizi, kulikuwa na Jaji mmoja tu ambaye alikuwa ameongezewa muda wa ajira ya ujaji kwa mujibu wa Katiba. Katika mapendekezo yake, Kikundi Kazi hakikumung’unya maneno:
“Mikataba iliyopo hivi sasa iko kinyume cha Katiba.... Hii ina maana kwamba Majaji hao wanafanya kazi ya Jaji kinyume cha Katiba, hivyo kazi zote ambazo wamezifanya na wanaendelea kuzifanya wakiwa chini ya ajira mpya za mikataba hazina uhalali wowote kisheria. Kazi hizo ni sawa kama vile zimefanywa na mtumishi mwingine yeyote asiye na madaraka ya Jaji. Hivyo basi, Rais ashauriwe kuifuta mikataba hiyo mara moja kwa vile ina madhara makubwa kwa jamii na katika uteuzi wa Majaji wapya kuchukua nafasi zao. Majaji waliofutiwa mikataba waendelee na pensheni zao kama kawaida.”
Miaka minne imepita tangu Kikundi Kazi kiwasilishe mapendekezo yake Ikulu lakini hakuna hatua zilizochukuliwa kutekeleza mapendekezo hayo. Aidha, licha ya msimamo wa majaji Luanda na Ramadhani kuwa na umri wa takriban miaka saba, utaratibu wa uteuzi wa majaji wastaafu haujaachwa na mamlaka husika ya uteuzi. Ajira ya sasa ya Jaji Kiongozi Fakih Jundu iko katika kundi hili la watu wasiokuwa Majaji kwa mujibu wa Katiba.
JAJI KIONGOZI FAKIH JUNDU
Jaji Kiongozi Fakih Jundu aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu na Rais Mkapa mwaka 2003. Julai 29, 2009, Jaji Jundu wakati huo akiwa Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Iringa, alitoa taarifa ya kustaafu kwa mujibu wa sheria. Hata hivyo, mara baada ya kutoa taarifa hiyo, Jaji Jundu siyo tu alipewa mkataba wa ujaji kwa miaka mitatu, bali pia alipandishwa cheo na kufanywa Jaji Kiongozi.
Kama hiyo haitoshi, inasemekana sasa kwamba Jaji Kiongozi Jundu ameongezewa mkataba mwingine tena wa miaka miwili kuendelea kuwa Jaji Kiongozi kuanzia Julai 29, 2012! Huu ni ukiukaji wa Katiba. Kwanza, kwa mujibu wa Taarifa ya Kikundi Kazi, “... umri wa kustaafu wa Jaji Kiongozi ni miaka sitini.... Hivyo, iwapo Rais atamuongezea Jaji Kiongozi muda wa kufanya kazi, hatamuongezea kama Jaji Kiongozi.”
Kwa maana nyingine, kama ilikuwa makosa kikatiba kumpa Jaji Jundu mkataba wa ajira kama Jaji wa kawaida, ilikuwa makosa makubwa zaidi kikatiba kumpandisha cheo na kumfanya Jaji Kiongozi wakati alikwishafikisha umri wa kustaafu wa Jaji Kiongozi! Pili, kwa utamaduni uliozoeleka Tanzania, majaji wamekuwa wanaongezewa kipindi kimoja cha miaka miwili ili wamalizie kesi walizokuwa nazo hadi muda wao wa kustaafu unawadia. Kwa msimamo wa kikatiba ulioelezwa na Jaji wa Rufaa Luanda, Jaji Mkuu Ramadhani na Kikundi Kazi, siyo sahihi kwa Jaji Kiongozi Jundu kustaafu na kupewa mkataba wa kuendelea na wadhifa huo kupindukia muda wake wa kustaafu kwa mujibu wa Katiba!
Nyongeza hii ya pili ya mkataba wa Jaji Kiongozi Jundu imewafanya watu wanaojiita ‘Watumishi wa Mhimili wa Mahakama’ kumwandikia Msajili wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania kulalamikia jambo hilo. Kwa mujibu wa barua yao, ambayo pia ilinakiliwa kwa Mwanasheria Mkuu na Jaji Mkuu, watu hao wamesema yafuatayo kuhusu Jaji Kiongozi Jundu: “Sisi watumishi wa Mahakama tunafahamu udhaifu mkubwa kiutendaji alionao Jaji Kiongozi wetu wa sasa. Kimsingi hamudu madaraka haya. Ipo mifano mingi ya udhaifu wa Jaji Jundu. Mfano alimhamisha hakimu kutoka kituo chake cha kazi kama adhabu kwa vile hakimu huyo alitoa maamuzi ambayo yeye hakuyafurahiya kwenye ile kesi maarufu ya kibaragashia. Ni busara za Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman, ndizo zilizomsaidia hakimu huyo.”
JAJI THOMAS MIHAYO
Thomas Bashite Mihayo aliteuliwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Oktoba 8, 2003. Januari 16, 2006 Jaji Mihayo alitoa notisi ya kustaafu kwa mujibu wa Katiba kuanzia Juni 8, 2006 atakapokuwa ametimiza umri wa miaka sitini. Hata hivyo, Machi 8 ya mwaka huo, Jaji Mihayo alitaarifiwa na Jaji Mkuu kwamba Rais Kikwete alikuwa amempa “... mkataba wa miaka miwili kuanzia Juni 9, 2006.” Mkataba huo ulifikia mwisho wake Juni 8, 2008. Hata hivyo, Jaji Mihayo alipatiwa mkataba mwingine tena wa mwaka mmoja ulioanzia Juni 9, 2008 hadi Juni 8, 2009 na baada ya hapo hakupatiwa mkataba mwingine.
Inaelekea Jaji Mkuu Ramadhani alisahau msimamo wake wa awali kuhusu ajira za mikataba kwani ndiye aliyependekeza Jaji Mihayo “... apewe mkataba mwingine wa mwaka mmoja...” Na wala si Jaji Mihayo pekee aliyepatiwa au kuongozewa mkataba katika mazingira tatanishi kama haya. Kwa mujibu wa nyaraka za Idara Kuu ya Utumishi, Jaji Donasian Mwita alipatiwa mkataba wa ujaji Juni 28, 2004. Mkataba huo wa miaka miwili ulianza kutumika Julai 1, 2004. Vile vile, Jaji Joseph Masanche alisaini mkataba wa aina hiyo hiyo na Idara Kuu ya Utumishi ulioanza kutumika kuanzia Machi 7, 2006.
MAADILI YENYE SHAKA
Msemaji wa Kambi hakuzungumzia masuala yanayohusu maadili ya majaji. Hata hivyo, kutokana na mjadala uliojitokeza ndani na nje ya Bunge kutokana na hotuba yake, ushahidi umepatikana unaoonyesha kwamba baadhi ya majaji wameteuliwa bila ya kwanza kuwafanyia uchunguzi juu ya maadili yao.
MAJAJI KASSIM NYANGARIKA NA ZAINAB G. MURUKE
Kassim Nyangarika alikuwa wakili wa kujitegemea na wakili mwenza wa Jaji Kiongozi Jundu kabla ya uteuzi wake kuwa Jaji wa Mahakama Kuu mwaka 2003. Kama wakili, Bwana Nyangarika aliwahi kumwakilisha mlalamikaji katika kesi ya Peter Muti dhidi ya CIELMAC Ltd., Kesi ya Madai Na. 314 ya 2003 iliyofunguliwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni. Katika kesi hiyo mteja wa wakili Nyangarika alishinda.
Hata hivyo, kufuatia rufaa dhidi ya uamuzi huo, Mahakama Kuu ilifutilia mbali mwenendo wa kesi hiyo baada ya kugundua kwamba Wakili Nyangarika alikuwa amefanya vitendo vyenye kuashiria uvunjifu mkubwa wa maadili. Kwa mfano, Mahakama Kuu iligundua kuwa Wakili Nyangarika alimwelekeza hakimu – kwa kutumia ‘kipande cha karatasi cha rafu na kilichoandikwa kirafiki’ - namna ya kuendesha kesi hiyo. Mahakama Kuu iligundua makosa makubwa zaidi ya hilo. Kwa mujibu wa Jaji Kalegeya, “... kulikuwa na mawasiliano yasiyokuwa rasmi kati ya Mahakama na Wakili.” Jaji Kalegeya alikuta ushahidi wa uwezekano mkubwa kwamba Wakili Nyangarika ndiye aliyeandaa uamuzi wa Mahakama katika kesi hiyo. Aidha, Mahakama Kuu iligundua kwamba Wakili Nyangarika “... aliielekeza Mahakama kutokutoa uamuzi kwa tarehe iliyopangwa badala yake aliielekeza itoe uamuzi huo tarehe nyingine.”
Kwa mujibu wa Jaji Kalegeya, kama kilichoonyeshwa katika mawasiliano ya Wakili Nyangarika na Mahakama ya Wilaya kilikuwa cha kweli basi “... utoaji haki katika Mahakama hiyo uko katika hatari kubwa kama sio jina la Mahakama yote, kitu kinachohitaji marekebisho ya haraka.” Kwa sababu hiyo, Jaji Kalegeya alielekeza kwamba “mamlaka husika zichukue hatua za kufichua ukweli kuhusu barua ya Wakili Nyangarika ya tarehe 18/03/2004.” Hukumu na maelekezo ya Jaji Kalegeya yalitolewa tarehe 22 Julai, 2005. Miezi saba baadaye, Wakili Nyangarika aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania!
Wakili mwingine mwenye maadili ya mashaka yanayofanana na ya Jaji Nyangarika ambaye pia ameteuliwa Jaji Mahakama Kuu ni Zainab Muruke. Kama wakili, Zainab Muruke alimwakilisha Stephen Hill Forwood ambaye alikuwa amepatikana na hatia na kuhukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka miwili bila faini katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu. Baadaye kampuni ya mawakili ya Z.G. Muruke & Co. Advocates iliwasilisha Hati ya Mapitio (Memorandum of Review) katika Mahakama hiyo hiyo ikiomba Bwana Forwood abadilishiwe hukumu.
Ombi hilo lilikubaliwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi Kabuta na tarehe 26 Julai, 2004, Bwana Forwood akabadilishiwa adhabu kuwa faini ya shilingi 20,000 au kifungo cha miaka miwili. Jambo hili liliripotiwa kwa Jaji Kiongozi ambaye aliamuru uchunguzi ufanywe uliopelekea kushushwa cheo cha Hakimu Mkazi Kabuta. Jaji Kiongozi pia aliamuru Wakili Muruke atoe maelekezo ya ushiriki wake katika sakata hilo. Hiyo ilikuwa tarehe 14 Desemba, 2004. Mwaka mmoja na miezi miwili baadaye, Zainab Muruke aliteuliwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
MAJAJI PELAGIA B. KHADAY NA PATRICIA FIKIRINI
Bi. Pelagia B. Khaday ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania aliyeteuliwa mwaka 2009. Kabla ya uteuzi huo Bi. Khaday alikuwa Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kabla ya hapo alikuwa Hakimu Mkazi Mkuu na Msajili wa Wilaya, Mahakama Kuu Kanda ya Arusha. Agosti 12, 2004, alipewa taarifa ya kusimamishwa kazi kama Msajili wa Wilaya na kuhamishiwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutokana na ‘uzito wa shutuma’ zilizotolewa dhidi yake kwa Jaji Mkuu.
Taarifa hiyo iliandikwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Edward Rutakangwa, kwa maelekezo ya Jaji Mkuu na ilieleza kwamba Bi. Khaday alikuwa anatuhumiwa kwa “kuwashinikiza au kuwashawishi baadhi ya mahakimu mkoani Arusha kushughulikia au kuamua kwa upendeleo mashauri yaliyowahusu ... jamaa au rafiki zake”; na “kuwaandalia sababu za rufaa baadhi ya washitakiwa waliotiwa hatiani na mahakama za mahakimu hapa mkoani.”
Kabla ya kumsimamisha Bi. Khaday kazi, Jaji Mfawidhi Rutakangwa alikuwa amemteua Mheshimiwa Jacob Somi, wakati huo akiwa Msajili wa Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi, kuwa Afisa Uchunguzi (Enquiry Officer) ili kuchunguza tuhuma dhidi ya Bi. Khaday. Taarifa ya Uchunguzi wa Awali ya Afisa Uchunguzi Somi inasema kwamba Bi. Khaday alikuwa amelalamikiwa na mahakimu kwa kuwashinikiza ili watoe maamuzi ya kesi zilizokuwa zinawakabili jamaa au marafiki zake.
Kwa mujibu wa Taarifa hiyo, Hakimu Mkazi Elvin Mugeta “alikiri kuwa-approached na Bi. Khaday ili atoe hukumu ya upendeleo kwa mshtakiwa Richard Bareto ambaye inasadikiwa kuwa ni jamaa wa rafiki yake wa karibu.” Ijapokuwa Bi. Khaday alikanusha kufanya hivyo, Afisa wa Uchunguzi Somi aliridhika kwamba “Bi. Khaday alikuwa amejiwekea utaratibu, kama alivyodai mwenyewe, wa kuwasiliana na Mahakimu kwa lengo la kuwafahamisha pamoja na mambo mengine malalamiko yaliyokuwa yakimfikia dhidi yao ili kuwanusuru wasiharibikiwe.”
Hata hivyo, Afisa Uchunguzi Somi aliridhika kwamba “utaratibu huu ulikuwa kero kwa mahakimu pale alipoutumia kwa kushinikizwa na jamaa zake na/au rafiki zake kwa lengo la kupata maamuzi ya upendeleo. Kitendo cha kumtoa mahakamani Hakimu kwa lengo la kutaka kujua hatima ya mshtakiwa Bareto aliyekuwa asomewe hukumu siku hiyo, ni mfano wa matumizi mabaya ya utaratibu huo.”
Afisa Uchunguzi Somi hakupata uthibitisho wa madai ya Bi. Khaday kuwaandalia sababu za rufaa washtakiwa waliotiwa hatiani. Hata hivyo, kwa mujibu wa Taarifa yake, “... sikuridhishwa na utaratibu wake wa kupeleka nakala ya hukumu kwa Bi. Mushi na kumtaka aisome ili kuona kama kuna uwezekano wa mshtakiwa Hussein Ramadhani Kitema kukata rufaa Mahakama Kuu baada ya kufungwa jela na Bw. Mugeta.” Afisa Uchunguzi Somi alipendekeza kwamba Bi. Khaday – “ambaye ni mtumishi wa Mahakama kwa kipindi kisichopungua miaka 20...” - apewe nafasi ya kujirekebisha.
Baada ya kuwasilishwa kwa Taarifa ya Afisa Uchunguzi Somi, Jaji Mfawidhi Rutakangwa alimteua Mh. Samuel Karua, Msajili wa Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi, kuwa Investigation Officer. Tarehe 23 Februari 2007, Investigation Officer Karua aliwasilisha Taarifa ya Uchunguzi wake kwa Jaji Mkuu. Taarifa ya Investigation Officer Karua ilimkosha Bi. Khaday kwa tuhuma zote dhidi yake.
Hata hivyo, Taarifa ya Investigation Officer Karua ina maeneo mengi yanayoleta mashaka. Kwanza, kama Investigation Officer Karua mwenyewe alivyosema, shahidi muhimu katika uchunguzi wake alikuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi Mushi. Vile vile, shahidi huyu alikuwa ‘star witness’ katika uchunguzi wa awali mbele ya Afisa Uchunguzi Somi na ndiye aliyetoa ushahidi wa yeye na mahakimu wengine kuingiliwa katika kazi zao na Bi. Khaday.
Hata hivyo, mbele ya Investigation Officer Karua, shahidi huyu muhimu alikana kila kitu alichokisema mbele ya Afisa Uchunguzi Somi. Kwa kiasi kikubwa, Investigation Officer Karua aliitumia about turn hii kumkosha Bi. Khaday dhidi ya tuhuma zote zilizokuwa zinamkabili. Cha kushangaza ni kwamba Investigation Officer Karua hakujiuliza na hakumuuliza shahidi huyu sababu za kukana ushahidi wote alioutoa mbele ya Afisa Uchunguzi Somi.
Je, alirubuniwa au kutishwa ili amsaidie Hakimu na mtumishi mwenzake katika Mahakama ya Tanzania asifukuzwe kazi? Kama sio hivyo, je, ni sababu zipi zilizomfanya shahidi huyu muhimu kubadili ushahidi wake kwa kiasi hicho? Je, ushahidi alioutoa shahidi huyu mbele ya Afisa Uchunguzi Somi ulikuwa wa uongo? Na kama ulikuwa wa uongo, ushahidi wake wa pili kwa Investigation Officer Karua ni wa kweli kiasi gani mpaka kumfanya Investigation Officer Karua kutamka kuwa shahidi huyu ‘anaweza ... kuwa anasema ukweli.’
Inaelekea Investigation Officer Karua, Hakimu Mkuu Mkazi mwenye uzoefu wa miaka mingi katika Mahakama, alifanya kazi yake kwa mtazamo wa kimahakama zaidi badala ya kutumia mtazamo wa kiupelelezi na/au kiuchunguzi ambayo hasa ndiyo ilikuwa kazi yake katika uchunguzi wa tuhuma dhidi ya Bi. Khaday. Kwa mtazamo wa kimahakama, ukweli kwamba shahidi muhimu kama Hakimu Mkazi Mfawidhi Mushi alikana ushahidi wake wa awali mbele ya Afisa Uchunguzi Somi ilikuwa inatosha kumfutia Bi. Khaday hatia yote. Kwa mtazamo wa kiupelelezi/kiuchunguzi, about turn ya shahidi huyu ingemfanya Investigation Officer Karua kuchunguza zaidi sababu za kigeugeu hicho.
Pili, Investigation Officer Karua hakuipa uzito wa kutosha Taarifa ya Afisa Uchunguzi Somi. Kwa mfano, Taarifa ya Afisa Uchunguzi Somi – yenye kurasa 14 zilizochapwa - imeelezewa katika Taarifa ya Investigation Officer Karua kwa aya moja tu! Kwa sababu hiyo, ni vigumu kukubaliana na Investigation Officer Karua kwamba Taarifa ya Afisa Uchunguzi Somi ‘ilikuwa muhimu sana’ wakati umuhimu huo haujafafanuliwa wala kuelezewa hata kidogo katika Taarifa yake.
Aidha, Investigation Officer Karua alitakiwa kueleza sababu za kutofautiana na Afisa Uchunguzi Somi kwamba Bi. Khaday alikuwa anakera mahakimu kwa kuwasiliana nao baada ya kushinikizwa na ndugu au rafiki zake ili wapatiwe upendeleo katika kesi zilizokuwa zinawakabili. Investigation Officer Karua hakufanya hivyo. Vile vile, Investigation Officer Karua hakuona ajabu wala kujiuliza kama ilikuwa ni kitu cha kawaida kwa Bi. Khaday kumleta Richard Bareto – mshtakiwa aliyehusishwa na shinikizo la Bi. Khaday kwa Hakimu Mkazi Mugeta – kama shahidi wake wa utetezi.
Tatu, Investigation Officer Karua hakutoa sababu za maana za kutochukua ushahidi wa mahakimu wengine waliodaiwa kushinikizwa na Bi. Khaday. Katika aya moja tu iliyowahusu mahakimu hao, Investigation Officer Karua alisema kwamba siku ya kutoa ushahidi wao kwake, watu hao “... walishikilia msimamo wa kauli walizotoa mbele ya Bwana Somi ... na baada ya tafakuri ya muda ... mashahidi hawa waliachiwa.”
Mbele ya Afisa Uchunguzi Somi, mashahidi hawa wawili, Hakimu Mkazi Msumi na Hakimu Mkuu wa Wilaya Mlay, walikuwa wamesema kwamba “... huko nyuma (Bwana Msumi) aliwahi kuitwa na mlalamikiwa baada ya wadhamini walioshindwa kukidhi masharti ya dhamana ... kumpelekea malalamiko ya kukataliwa dhamana, maelezo ambayo hayakuwa na ukweli wowote.” Aidha, kwa mujibu wa Afisa Uchunguzi Somi, “... katika hali isiyokuwa ya kawaida Bw. Mlay, PDM hakuwa tayari kueleza kilichomsibu hadi kujiengua katika usikilizaji wa kesi ambayo Bi. Mushi alidai ilikuwa inamkabili rafiki yake wa karibu na Bi. Khaday.” Investigation Officer Karua hakuona sababu yoyote ya kufuatilia ushahidi wa mahakimu hawa wawili!
Nne, Investigation Officer Karua anakubali kwamba hali ilikuwa tete katika Kituo cha Arusha: “Inaelekea mtuhumiwa alikuwa na mahusiano mabaya na baadhi ya mahakimu.” Kama hivyo ndivyo ilivyokuwa, Investigation Officer Karua alikuwa na wajibu wa kuchunguza chanzo cha mahusiano hayo mabaya, hasa kwa vile kulikuwa sio tu na tuhuma bali pia ushahidi wa mahakimu husika kwamba Bi. Khaday alikuwa anawaingilia mahakimu katika kazi zao. Hakufanya hivyo. Badala yake Taarifa ya Investigation Officer Karua inaonekana kama jitihada za kumkosha Bi. Khaday dhidi ya tuhuma nzito za ukosefu wa maadili ya kimahakama. Jitihada hizi zilifanikiwa kwani miaka miwili baada ya Taarifa ya Investigation Officer Karua, Bi. Khaday aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Na wala siyo Bi. Khaday pekee aliyeneemeka na taarifa hiyo. Bi. Patricia Fikirini, ambaye Taarifa ya Afisa Uchunguzi Somi inamwelezea kama mmoja wa mahakimu waliosikiliza kesi ya mfanyabiashara maarufu wa Arusha, Justin Nyari iliyokuwa chanzo cha tuhuma dhidi ya Bi. Khaday – alihusishwa na tuhuma dhidi ya Bi. Khaday kwa maneno yafuatayo: “... Kama mtawala ... (Bi. Khaday) ... alisema aliwahi, tena kwa nia njema, kumweleza Bi. Fikirini ... kuhusu uvumi kwamba mume wake alikwenda gerezani na kuchukua mamilioni ya fedha kwa Bw. Nyari na hivyo kumshauri awe mwangalifu zaidi”! Katika uteuzi wa majaji uliofanywa na Rais Kikwete mwezi Juni mwaka huu, Bi. Patricia Fikirini naye ameteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Wapo wanaoweza kusema kwamba Bi. Khaday hakupatikana na hatia yoyote na kwa hiyo haikuwa makosa kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu. Aidha, inaweza kudaiwa kwamba Bi. Fikirini hajawahi kutuhumiwa kwa kosa lolote la maadili na kwamba ‘uvumi’ pekee hautoshi kumnyima mtu mwenye sifa haki ya kuteuliwa Jaji wa Mahakama Kuu. Kwa wenye hoja za aina hii jibu langu ni kwamba kiwango cha ‘sifa maalum’ kinachotakiwa na Katiba kwa mtu kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ni mtu ambaye “... kwa kila hali anafaa kukabidhiwa madaraka ya Jaji wa Mahakama Kuu....” Kiwango hiki ni cha juu kiasi kwamba kutokuwa na hatia pekee haitoshi kumfanya mhusika kuwa ‘kwa kila hali anafaa kukabidhiwa madaraka ya Jaji wa Mahakama Kuu.’ Kwa maoni yangu, mtu aliyeundiwa uchunguzi wa kimaadili au ambaye kuna uvumi unaomhusisha na rushwa ‘hafai kwa kila hali’ kukabidhiwa madaraka ya Jaji wa Mahakama Kuu. Majaji Khaday na Fikirini wapo kwenye kundi hili.
JAJI ALOYSIUS MUJULIZI
Jaji Aloysius Mujulizi alikuwa miongoni mwa watu ishirini walioteuliwa Majaji wa Mahakama Kuu mwezi Februari, 2006. Kabla ya uteuzi wake, Jaji Mujulizi alikuwa wakili wa kujitegemea katika kampuni ya mawakili ya Ishengoma, Masha, Magai & Mujulizi Advocates (IMMMA) ya Dar es Salaam. Kampuni hii ya mawakili ndiyo iliyoshiriki katika kuanzishwa kwa kampuni iitwayo Deep Green Finance Co. Ltd. mnamo tarehe 18 Machi 2004. IMMMA Advocates vile vile walikuwa mawakili wa Tangold Ltd.
Makampuni haya mawili yanatuhumiwa kutumika kupitishia mabilioni ya fedha zilizoibiwa Benki Kuu ya Tanzania kati ya mwaka 2005 na 2006. Kwa mfano, katika kipindi kifupi cha miezi minne kati ya Agosti 1 na Desemba 10, 2005 kampuni ya Deep Green Finance ilipokea jumla ya shilingi 10,484,005,815.39 kutoka akaunti ya kulipia madeni ya nje (EPA) iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania. Katika kipindi hicho hicho, kampuni ya Tangold Ltd. ililipwa dola za Marekani 13,736,628.73 kutoka kwenye akaunti hiyo ya EPA. Nyaraka zilizowasilishwa BRELA na mawakili wa IMMMA Advocates na kusainiwa na Gavana wa Benki Kuu wa wakati huo Daudi Ballali tarehe 20 Mei 2005 zinaonyesha kwamba Tangold Limited ilikuwa kampuni ya kigeni kutoka Jamhuri ya Mauritius. Haya yote yalitokea wakati Jaji Mujulizi akiwa wakili mwenza wa IMMMA Advocates.
‘SIFA MAALUM’ ZENYE SHAKA
JAJI WA RUFAA MBAROUK SALIM MBAROUK
Mbarouk Salim Mbarouk aliteuliwa kuwa Jaji wa Rufaa wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania mwaka 2008. Kabla ya uteuzi huo Jaji Mbarouk alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar. Sifa za mtu kuteuliwa kuwa Jaji wa Rufaa zimeainishwa katika ibara ya 118(3) ya Katiba: “Majaji ... wa Rufani watateuliwa na Rais, kwa kushauriana na Jaji Mkuu, kutoka miongoni mwa watu wenye sifa za kuteuliwa kuwa Majaji wa Mahakama Kuu ... zilizoainishwa katika Ibara ya 109 ya Katiba au kutoka miongoni mwa watu wanaoweza kuteuliwa kuwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar kwa mujibu wa sheria zinazotumika Zanzibar na wamekuwa na sifa hizo kwa muda usiopungua miaka kumi na tano.”
Kwa mujibu wa Ibara ya 94(3) ya Katiba ya Zanzibar, 1984, “mtu hatoweza kuteuliwa kuwa Jaji au Kaimu Jaji wa Mahkama Kuu mpaka awe na shahada ya Sheria ya Chuo Kikuu kinachotambuliwa au Chuo cha aina hiyo; au awe au amewahi kuwa Jaji wa Mahkama zilizofanana na hii kwa kesi zote za jinai na madai katika Tanzania au sehemu yoyote ya Jumuiya ya Madola au Mahkama ya Rufaa kutoka Mahkama hizo; au awe Mwanasheria wa Zanzibar au Tanzania kwa kipindi kisichopungua miaka saba; au awe na uzoefu wa Jaji au mwanasheria kwa pamoja usiopungua miaka saba.” Jaji Mbarouk hajatimiza hata moja ya masharti hayo ya Katiba ya Zanzibar. Jaji huyu hana shahada yoyote ya sheria inayotambuliwa na mamlaka ya ithibati ya Tanzania kama inavyotakiwa na Ibara ya 109(7) ya Katiba. Jaji huyu ana stashahada ya juu ya sheria (Post Graduate Diploma in Law) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Shahada ya Uzamili ya Sanaa ya Chuo Kikuu cha nchini Uingereza.
Uteuzi wa Jaji Mbarouk kuwa Jaji wa Rufaa ulileta minong’ono mingi katika taaluma ya sheria kiasi kwamba marehemu Wakili Leopold Kalunga anasemekana kufungua shauri katika Mahakama Kuu ya Tanzania kutaka uteuzi huo utenguliwe. Hata hivyo, Wakili Kalunga alifariki kabla ya shauri lake kusikilizwa na kwa hiyo liliondolewa mahakamani. Aidha, monong’ono hiyo ilimfanya Jaji wa Rufaa Mbarouk kujiunga na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ambako bado ni mwanafunzi hadi ninapoandika Addendum hii.
MAJAJI ‘WALIOTOLEWA MITAANI’
Katika Maoni ya Kambi tulidai kwamba “... sasa watu wanateuliwa kuwa Majaji wa Mahakama Kuu ambao hawajawahi kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama na - kwa sababu hiyo - hawajafanyiwa vetting yoyote na mamlaka hiyo ya kikatiba....” Ukiacha uteuzi wa Jaji wa Rufaa Mbarouk ambao haubanwi na masharti ya Ibara ya 109(1) na 113(1)(a) ya Katiba, majaji wengine waliotajwa kwenye Addendum hii hawakupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama. Majaji wengine ambao pia hawajawahi kupendekezwa na Tume hiyo ni pamoja Fatuma Massengi, Mary Sumari, Imani Mkwawa-Aboud na Sekela Mushi.

No comments:
Post a Comment