KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbroad Slaa amesema Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, ni msaliti wa demokrasia nchini kwa kuwa hana dhamira ya kutetea mageuzi ya kisiasa kwa maslahi binafsi.
Akihutubia katika mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Luatala, Kata ya Sindano, Jimbo la Lulindi mkoani Mtwara jana, Dk. Slaa alisema kuwa Maalim Seif ni kiongozi asiyeeleweka, na ameshindwa kutumia chama chake cha CUF na nafasi aliyonayo kutatua matatizo ya wananchi wanyonge, badala yake amekifanya kipoteze heshima na mvuto ikiwa ni pamoja na kupoteza dhamira ya kushika dola.
“Tulimuamini Maalim na timu yake kuwa wangeweza kupambana kuisaidia mikoa ya kusini, kwa maana wao washambulie huku na sisi maeneo mengine na kisha tumuondoe adui. Lakini cha kusikitisha wenzetu wameungana na hao tunaotaka kuwaondoa, na tunachoshuhudia huku sasa ni wananchi kuaminishwa kuwa kuna vyama vya kidini vinafaya siasa,” alisema Dk. Slaa.
Alisema kutokana na usaliti wa kiongozi huyo, hatakuwa tayari kukaa nae meza moja kwa ajili ya kuzungumzia siasa, hata kama ataombwa na wananchi, kwa vile haaminiki na anaweza kumsaliti.
Alidai kuwa, muungano baina ya Maalim Seif na chama chake na watawala, umewafanya washindwe kupigia kelele uonevu unaofanywa na Serikali ya CCM dhidi ya wakulima wa korosho katika mikoa ya Mtwara na Lindi, na badala yake wabunge wa vyama hivyo (CUF na CCM) wakiungana kutetea vitu visivyo vya msingi ikiwamo kudai posho katika vikao vya Bunge.
Dk. Slaa alisema hakuwahi kuwa na tuhuma zozote za ufisadi, ndiyo maana Serikali ya CCM inashindwa kumdhibiti kila mara anapoamua kuweka uozo wao hadharani, badala yake imekuwa ikifanya kila mbinu kumsingizia mambo yasiyo ya msingi, ambayo mwishowe wananchi hubaini hayana ukweli wowote.
Mnyika ataka kauli ya JK kuhusu ushoga
Katika hatua nyingine, CHADEMA kimemtaka Rais Jakaya Kikwete atoe tamko na msimamo wa Tanzania kuhusu hatua ya Rais Barack Obama wa Marekani kuidhinisha sheria ya ushoga nchini mwake.
Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika juzi kwenye Kata za Mnavira na Mchauru, Jimbo la Lulindi, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika alisema ukimya wa Rais Kikwete hauleti picha nzuri katika suala hilo linalopingwa na dini zote.
Kauli hiyo ya Mnyika ilifuatia swali aliloulizwa na Katibu wa Chama cha Wananchi (CUF), Kijiji cha Rivango, Keneth Khamis aliyetaka kujua ukweli kuhusu taarifa zilizowasilishwa kwao, zikieleza kuwa CHADEMA inaunga mkono ushoga na usagaji, kutokana na kuwa na uhusiano na ushirikiano na chama cha Conservatives cha Uingereza.
Alisema hizo ni propaganda zilizopangwa na CCM ili CHADEMA kisikubalike katika jamii, na kusema kauli iliyowahi kutolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye ikiihusisha CHADEMA na kuunga mkono ushoga ni ya unafiki.
Alisema baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron kuukubali ushoga na usagaji na kutaka iwe sehemu ya masharti kwa misaada inayotolewa na nchi za Magharibi, CHADEMA ilipinga na kuweka wazi kwamba haiungi mkono ‘uchafu’ huo.
Mnyika alisema kutokana na Rais Kikwete kwenda Marekani kwa lengo la kutafuta misaada, kuna dalili ya kuwepo uwezekano wa taifa hilo kupenyeza ajenda ya ushoga na ikakubaliwa na serikali kama ilivyotokea kwa Malawi.
Chanzo:Tanzania daima
No comments:
Post a Comment