Wamefanya kitendo hiki kwa lengo la kumuogopesha (intimidate) Wakili Abdulla Juma na labda kuwahadharisha mawakili wengine waache au waogope kuwatetea watuhumiwa wa kesi hizi zinazoendelea na nyenginezo. Mabomu hayo yameathiri sana ofisi na kuifanya kutokalika kwa siku tatu na hadi wakati huu hatujuwi athari za kiafya zilizowakuta mawakili waliokuwemo ndani ya ofisi hiyo. Vitisho na hujma dhidi ya mawakili vina lengo la kudhoofisha ustawi wa utawala wa sheria, haki za binaadamu na utawala bora. Endelea kusoma taarifa hii
P.O.BOX 3319, Zanzibar, Tanzania. Bwawani Hotel – Ground Floor, Suite # 107 Tel/Fax +255 24 2234890 Mobile: +255 773 092511 Email: zls@zanlink.com
Our Ref: ZLS/Council/09/2012 30 Mei, 2012Kamishna wa Polisi
Makao Makuu ya Polisi
Ziwani, Zanzibar
Kamishna Mussa Ali Mussa,
KUH: MALALAMIKO YA CHAMA CHA WANASHERIA ZANZIBAR KWA KITENDO CHA POLISI KUPIGA MABOMU OFISI YA WAKILI
Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS), kwa masikitiko makubwa, kinaomba kuwasilisha kwako malalamiko yetu kufuatia kitendo cha Polisi kupiga mabomu ofisi ya wakili ya AJM Solicitors iliopo Amani, Zanzibar. Jumatatu tarehe 28 Mei 2012 majira ya asubuhi katika Mahkama ya Mwanakwerekwe iliopo nje kidogo ya Manispaa ya Zanzibar, walifikishwa katika mahkama hizo watuhumiwa kadhaa kwa mashtaka mbalimbali yahusuyo uvunjifu wa amani. Hii ilikuja baada ya Jeshi la Polisi kuamua kumchukuwa kutoka msikitini Sheikh Mussa Juma Issa, Imam wa msikiti wa Kwa Biziredi majira ya saa 1.30 usiku wa Jumamosi 26 Mei 2012. Wafuasi wake walimfuata hadi polisi Madema alipowekwa ndani. Baada ya muda kupita na taarifa kuenea ndipo waumini wa dini ya Kiislam walipoanza kumiminika kituo cha Polisi, Madema wakisubiri kujua khatma ya kiongozi wao.
Watuhumiwa waliokamatwa Jumamosi tarehe 26 Mei na Jumapili tarehe 27 Mei 2012 walifikishwa mahkamani asubuhi ya tarehe 28 Mei 2012. Kama sote tunavyoelewa, ni msingi mkuu wa sheria zetu kwamba mtuhumiwa huwa hana hatia yoyote mpaka pale Mahkama itakapotamka hivyo baada ya kesi kuendeshwa kisheria. Na ni haki ya kikatiba kwa mshtakiwa kupata utetezi wa kisheria kutoka kwa watu wanaotambuliwa na sheria kuwa mawakili. Wakili Abdulla Juma Mohamed wa AJM Solicitors & Advocates Chambers ni wakili wa utetezi katika kesi ya Jinai inayotokana na MAD/PCR/45/2012 ya Mahkama ya Wilaya Mwanakwerekwe (Mhe. Janet Sekihola) na pia kwa kesi nyengine ya Mahkama ya Wilaya Mwanakwerekwe (Mhe. Mohamed Ali) inayotokana na MKD/PCR/05/2012 inayomkabili Mbarouk Said Khalfan na Mussa Juma Issa. Wakati watuhumiwa katika kesi ya kwanza wanashtakiwa kwa uzembe na ukorofi (kif. 181(d) Sheria ya Jinai 6/2004), kesi ya pili ni ya shtaka la mkusanyiko usio halali (kif. 55 na 56 Sheria Nam 6/2004).
Baada ya kesi tajwa hapo juu kuakhirishwa, Wakili Abdulla Juma aliondoka na kuelekea katika Mahkama ya Ardhi, Vuga Zanzibar. Majira ya saa 6.30 mchana ofisi yake ya uwakili iliopo karibu na Amani Roundabout, ilishambuliwa na Polisi ambao waliingiza mtutu/mitutu ya bunduki ndani ya madirisha na kupiga mabomu ya machozi. Sisi tunaamini kabisa kwamba askari waliofanya hivi wamefanya wakijuwa kabisa kwamba kitendo chao kinakiuka maadili yote ya kazi yao ya kulinda usalama wa raia na mali zao. Wamefanya kitendo hiki kwa lengo la kumuogopesha (intimidate) Wakili Abdulla Juma na labda kuwahadharisha mawakili wengine waache au waogope kuwatetea watuhumiwa wa kesi hizi zinazoendelea na nyenginezo. Mabomu hayo yameathiri sana ofisi na kuifanya kutokalika kwa siku tatu na hadi wakati huu hatujuwi athari za kiafya zilizowakuta mawakili waliokuwemo ndani ya ofisi hiyo. Vitisho na hujma dhidi ya mawakili vina lengo la kudhoofisha ustawi wa utawala wa sheria, haki za binaadamu na utawala bora.
ZLS inalaani kwa nguvu zote kitendo cha Polisi cha kupiga mabomu ofisi ya wakili. Tunasema kitendo hiki kinalitoa thamani Jeshi la Polisi na kinaondosha imani ya wananchi kwao na pia kuharibu uhusiano wa karibu unaopaswa kujengwa baina ya raia na jeshi la polisi kupitia dhana ya “Polisi Shirikishi”. Sisi kama maofisa wa mahkama tunasikitishwa sana na hali hii na tunakutaka ufanye uchunguzi na watakaobanika kufanya kitendo hiki wachukuliwe hatua zifaazo. Tunaamini kwamba utendaji kazi wa Polisi hauendi kiholela – kila kikundi kinakuwa chini ya udhibiti na uangalizi wa Jeshi la Polisi kama taasisi. Hivyo hakutakuwa na ugumu wowote kumtambua askari aliefanya uhalifu huo. Vyenginevyo utatujengea imani kwamba kitendo hiki kina baraka zote za Jeshi la Polisi.
Wako katika kuheshimu Sheria za Nchi,
………………………….
Awadh Ali Said
Rais, ZLS
Nakala kwa:
1. Mhe. Jaji Mkuu, Zanzibar
2. Mhe. Mwanasheria Mkuu, Zanzibar
3. Mhe. Waziri wa Katiba na Sheria, Zanzibar
4. Mhe. Waziri wa Nchi, Afisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Zanzibar
5. Mhe. Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Zanzibar
6. Mkurugenzi wa Mashtaka, Zanzibar
7. Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Tanzania
8. Rais, Chama cha Wanasheria wa Afrika Mashariki (EALS) – Arusha, Tanzania
9. Rais, Chama cha Wanasheria wa Uganda
10. Rais, Chama cha Wanasheria wa Tanganyika
11. Mwenyekiti, Chama cha Wanasheria wa Kenya
12. Mwenyekiti, Chama cha Wanasheria wa Burundi
13. Mwenyekiti, Chama cha Wanasheria wa Rwanda
No comments:
Post a Comment