Monday, June 4, 2012

Watakiwa Kutumia Vizuri Fedha Za Sensa

WARATIBU WA SENSA YA WATU NA MAKAZI 2012  WATAKIWA KUSIMAMIA FEDHA NA RASILIMALI ZINAZOTOLEWA.
 
Na. Aron Msigwa - MAELEZO
4/6/2012, Morogoro.
 
Ikiwa imebaki miezi michache kabla ya kuanza kwa zoezi la Sensa ya watu na makazi nchini  serikali imewataka waratibu wa zoezi hilo  kuhakikisha kuwa wanasimamia kikamilifu fedha na rasilimali zinazopelekwa kwenye mikoa na wilaya zote nchini ili kufanikisha zoezi hilo.
 
Akizungumza na waratibu wa Sensa  ya watu na makazi 2012 kutoka  katika  mikoa na wilaya zote nchini  leo mjini Morogoro naibu katibu mkuu Ofisi ya Waziri mkuu ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw.Alphayo Kidata amesema kuwa zoezi hilo litafanikiwa kwa  kiwango kikubwa kama waratibu  hao watasimamia ipasavyo matumizi  ya fedha na rasilimali zinazopelekwa  katika meneo yao. 
 
Amesema  jukumu la usimamizi wa Sensa kwenye ngazi ya mikoa na wilaya ni la viongozi wa maeneo hayo na kufafanua kuwa kushindwa kwa zozei hilo katika wilaya au mikoa husika ni kiashirio cha viongozi hao kushindwa kusimamia majukumu yao kwani takwimu zitakazopatikana zitatumiwa pia na mamlaka za mikoa na wilaya katika shughuli za maendeleo.
 
"Napenda kusisitiza kuwa mafanikio ya Sensa ya watu na makazi 2012 yanawahusisha pia viongozi wa mikoa na wilaya zote nchini hivyo usimamizi usioridhisha kwenye mikoa na wilaya zetu utasababisha upatikanaji wa takwimu zisizosahihi na hivyo kuathiri maendeleo ya maeneo hayo hivyo tunawajibu wa kuhakikisha kuwa zoezi hilo linafanikiwa" amesisitiza. 
 
Amesema kuwa kwa kutambua umuhimu wa zoezi hilo serikali imeiweka Sensa ya watu na makazi kuwa moja ya vipaumbele vyake kwa mwaka huu na kuongeza kuwa zoezi hilo ambalo ni la kitaifa licha ya kuwa jukumula kila mtanzania  waratibu hao wana wajibu wa kusimamia ufanikishaji wa zoezi hilo.
 
" Zoezi la ukusanyaji wa takwimu katika zoezi la Sensa haliwezi kutimizwa iwapo kazi ya ukusanyaji wa takwimu katika maeneo yote ya wilaya na mikoa hamtaifanya kwa umakini na jukumu lenu kuhakikisha kuwa mnatekeleza maagizo yote kutoka ngazi za juu ili kufanikisha zoezi hilo" amesema Bw. Kidata.
 
Amewataka waratibu hao kuwa wasimamizi wazuri na kuhakikisha kuwa uteuzi wa makarani na wasimamizi wa zoezi la sensa unafanywa kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa ili kuondoa manung'uniko na kuleta ufanisi wa kazi wa kazi wakati wa zoezi hilo.
 
Amefafanua kuwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzbar ndio waratibu wa Zoezi hilo na Kufafanuz kuwa sensa ya watu na makazi kwa mwaka huu inalenga kupata takwimu sahihi ambazo zitasaidia kutunga  Sera  na kupanga programu za maendeleo za kuiwezesha serikali kupanga na kutathmini mipango ya maendeleo nchini.
 
Awali akizungumza kabla ya ufunguzi wa mkutano huo Mkurugenzi wa Sensa ya watu na Takwimu za jamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu  Bw. Ephraim Kwesigabo  amesema kuwa hivi sasa maandalizi yamekamilika na kuongeza kuwa mafunzo hayo ya awali kwa waratibu wa Sensa kutoka mikoa na wilaya zote nchini yanalenga kuwajengea uwezo waratibu hao ili waweze kusimamia vyema maeneo yao wakati wa zoezi la Sensa.
 
Amesema mafunzo hayo yanajadiliwa na kutoa ufafanuzi  wa masuala mbalimbali ya ufanikishaji wa zoezi hilo yakiwemo namna ya kuwapata makarani na wasimamizi wa Sensa, maandalizi ya mafunzo katika wilaya  na mikoa yao, usimamizi wa zoezi la kuhesabu watu na ubora.
 
Naye Mratibu wa taifa wa Sensa ya watu na makazi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Irenius Ruyobya amefafanua kuwa tayari maandalizi ya ufanikishaji wa zoezi la sensa ikiwemo upatikanaji wa vifaa vya kisasa kwa ajili ya zoezi hilo yamekwishafanyika.
 
Pia amefafanua kwa zoezi la  uchapaji wa karatasi za maswali ya sensa (madodoso) linaendelea kufanyika kwa ufanisi mkubwa  huku akifafanua kuwa zoezi hilo litafanyika mwezi Agositi tarehe 26 kama ilivyopangwa na kutoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa makarani wa sensa watakaopita katika maeneo yao kwa lengo la kukusanya takwimu.

No comments: