SIR ALEX ANAAMINI KWENYE MPIRA CHOCHOTE CHAWEZA KUTOKEA NA KWA HARAKA SANA NA KUBADILISHA MATOKEO.
Wakati Sir Alex Ferguson ameshaeleza hii ndio Dabi kubwa kupita zote katika himaya yake ya Miaka 26 akiwa Meneja wa Manchester United, mwenzake wa Man City, Roberto Mancini, amepooza kwa kudai wako nyuma ya Man United hivyo pambano hili halitaamua nani Bingwa.
Carlos Tevez na James Milner wakifanya mazoezi hivi karibuni
Ni mtazamo tofauti lakini ukweli ni kuwa yeyote atakaeshinda Mechi itakayochezwa Uwanja wa Etihad Jumatatu Usiku ndie ana nafasi kubwa ya kutwaa Ubingwa hasa kwa vile zimebaki Mechi 3 tu Ligi kumalizika.
Mbali ya Ubingwa, pia ile vita ya kuwania nafasi mbili zilizobaki za 4 bora, ambayo inapiganwa na
Arsenal, Newcastle United, Tottenham Hotspur na Chelsea, itazidi kupamba moto hasa kwa vile Chelsea wametinga Fainali ya UEFA CHAMPIONZ LIGI.
Endapo Chelsea atatwaa Ubingwa wa UEFA CHAMPIONZ LIGI, basi wao watacheza michuano hiyo Msimu ujao na ile Timu itakayomaliza nafasi ya 4 haitaingizwa na badala yake itacheza EUROPA LIGI.
Mabingwa watetezi Man United wapo kileleni wakiwa Pointi 3 mbele ya Man City lakini ikiwa Man City watashinda Mechi hiyo basi watatwaa uongozi kwa vile wana ubora wa tofauti ya magoli na endapo Man United watashinda watapaa juu zaidi wakiwa Pointi 6 mbele huku Mechi zikiwa zimebaki mbili.
Ferguson ametamka: ‘Nadhani ndio Dabi kubwa katika muda wangu wote hapa. Lazima twende huko, kucheza vizuri na sio kutoa magoli ya kijinga. Hamna sabau kwanini tusipate matokeo mazuri. City walitegemea hili ndilo litakaloamua Ubingwa lakini kwetu pia ni hivyo hivyo. Vyovyote vile hili ndio litaamua Ubingwa!’
Hata hivyo, Roberto Mancini yeye anaamini Man United ndio wana nafasi kubwa kutwaa Ubingwa na amesema: ‘Wako juu. Pointi 3 mbele. Baada ya Dabi wana mechi laini. Tunaweza kuzungumzia Ubingwa baada ya Jumatatu lakini haiwezekani!’
Mechi ya Jumatatu itakuwa ni Dabi ya 4 kwa Msimu huu na walikutana mara ya kwanza kwenye Ngao ya Hisani na Man United walishinda 3-2 baada ya kutanguliwa 2-0, Oktoba 23 Man City walishinda 6-1 Old Trafford kwenye Mechi ya Ligi huku Man United wakicheza Mtu 10 na Mwezi Januari Man United iliwachapa City bao 3-2 Uwanjani Etihad na kuwatoa nje ya FA Cup, Kombe ambalo walikuwa wakilishikilia.
POLISI WAONYA!
Polisi wa Jijini Manchester wamewaonya Washabiki ambao wataleta vurugu kwenye Dabi ya Jumatatu Aprili 30 kati ya Manchester City na Manchester United itakayochezwa Etihad ambayo ni Mechi ya Ligi Kuu England yenye umuhimu mkubwa katika kuamua nani Bingwa Msimu huu.
Ingawa Wakuu wa Polisi wamewasifia Mashabiki wa Timu hizi hasa walipokutana kwenye Raundi ya 3 ya FA Cup Uwanjani Etihad na Man United kushinda bao 3-2, Watu 29 walikamatwa na Polisi kwenye Mechi ya Carling Cup Miaka miwili iliyopita.
Mashabiki wa Man United wamepewa mgao wa Tiketi 2,620 tu ili kuona Mechi hiyo ambayo itakuwa na ulinzi mkali.
Polisi wameonya kuwa haitaruhusiwa kwa Mtu yeyote kuwa na pombe kwenye eneo lililokatazwa linaloanzia katikati ya Mji hadi Uwanjani Etihad na yeyote atakaekutwa nayo atanyang’anywa.
Mbali ya hilo, Polisi pia imeonya Mtu ambaye ataefika Uwanjani akiwa amelewa hataruhusiwa kuingia ndani.
MSIMAMO Timu za juu:
1 Man United Mechi 35 Pointi 83 [Tofauti ya Magoli 54]==Wamebakisha Mechi 3
2 Man City Mechi 35 Pointi 80 [Tofauti ya Magoli 60]==Bado 3
3 Arsenal Mechi 35 Pointi 65 [Tofauti ya Magoli 24]==Bado 3
4 Newcastle Mechi 34 Pointi 62 [Tofauti ya Magoli 11]==Bado 4
[MECHI ZILIZOBAKI kwa Man United & Man City]
Man City | Man Utd |
Jumatatu Aprili 30 Man City v Man Utd Jumamosi Mei 5 Newcastle v Man City Jumapili Mei 13 Man City v QPR | Jumatatu Aprili 30 Man City v Man United Jumamosi Mei 5 Man United v Swansea Jumapili Mei 13 Sunderland v Man United |
No comments:
Post a Comment