Rais amteua wakili wa Lulu kuwa Jaji
RAIS Jakaya Kikwete amemwapisha kuwa Jaji wakili wa kujitegemea, Joaquine De-Mello ambaye alikuwa akimtetea msanii wa filamu Elizabeth Michael (Lulu) anayetuhumiwa kwa mauaji ya msanii mwenzake, Steven Kanumba.
Wakili huyo, ambaye ni mshindi wa tuzo ya Mwanamke Jasiri Tanzania ya Martin Luther King ya mwaka 2012 na ambaye alikuwa pia alikuwa mmoja wa makamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG) ni miongoni mwa majaji 10 walioapishwa jana na Rais Kikwete, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
De-Mello ni miongoni mwa mawakili wanne waliojitokeza Aprili mwaka huu kumtetea Lulu katika kesi hiyo ya mauaji inayomtuhumu kumuua usiku wa kuamkia Aprili 7, mwaka huu.
Mawakili wengine wanaomtetea Lulu ambaye umri wake umekuwa na utata ni Kennedy Fungamtama, Peter Kibatala na Fulgence Massawe.
Akizungumza kwenye viwanja vya Ikulu, De-Mello alisema baada ya kuteuliwa kuwa Jaji, sasa atafanya kazi hiyo na moja ya mikakati yake ni kukabiliana na changamoto za wingi wa kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania.
No comments:
Post a Comment