WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda , amesema tukio la kupigwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Dk Stephen Ulimboka, lina utata na kuongeza kuwa uchunguzi utakaofanywa na vyombo vya usalama ndio utakao maliza utata huo.
Pinda aliyasema hayo jana bungeni alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni Freeman Mbowe, katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo.
“Mazingira ya tukio hili bado yana utata mwingi, yanahitaji uchunguzi wa kina, kila mtu anasema lake, mwingine hili na wengine wanasema Serikali ndiyo imehusika,” alisema na kuongeza:
“Mimi nasema kama ni Serikali basi tutakuwa ni watu wa ajabu sana, Serikali tufanye ili iweje.”
Pia Pinda alisema kuwa, Serikali imefanya juhudi mbalimbali ili kuhakikisha kuwa wanaweza kuokoa maisha ya Watanzania ikiwa ni pamoja na kutumia hospitali za Lugalo pamoja na matawi yake, kutumia madaktari waliostaafu na wengine walio wizarani.
“Tumezungumza na wenzetu wa Lugalo ili wananchi waweze kutibiwa katika hospitali hiyo na matawi mengine,” alisema Pinda.
Baada ya maelezo hayo, Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Tundu Lisu, alimuuliza Pinda kwa nini asiwajibike katika suala la mgomo wa madaktari kwani ni yeye amekuwa akilishughulikia kwa muda na halionekani kupata ufumbuzi.
Baada ya swali hilo, Pinda alisema kuwa, yapo mazingira yanayoweza kumlazimu kuwajibika lakini siyo, haya ya mgomo wa madaktari kwani amejaribu kwa kiasi kikubwa kutafuta ufumbuzi wa suala hilo.
“Yapo mazingira yanayoweza kunifanya nijiuzulu, lakini hili la madaktari nimejaribu kwa uwezo wangu, lakini be what it is (kwa jinsi lilivyo), kuna changamoto nyingi katika suala hili,” alisema Pinda.
Baada ya majibu hayo, Lisu alipewa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza na kusema “If you have tried your very best and you failed, why don't you resign?” (kama umejaribu kufanya kila linalowezekana ukashindwa, kwa nini usijiuzulu??)
Baada ya swali hilo, Spika Anne Makinda alimtaka Waziri Mkuu kutojibu swali hilo la nyongeza kwa maelezo kuwa, linafanana na swali la msingi.
Hata baada ya maelezo ya Spika, Waziri Mkuu alijibu kwa kumueleza Lisu kuwa, anamuheshimu sana lakini lugha aliyotumia katika kuuliza swali lake siyo nzuri.
Mbunge Mwingine aliyezungumzia suala hilo ni Martha Mlata, aliyesema kuna uvumi kuwa, kuna watu wanawapa baadhi ya madaktari fedha ili wahamasishe wenzao kugoma.
Alisema kuwa, lengo la kikundi hicho ambacho hakukitaja, ni nchi isitawalike.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema na wao (Serikali) wamesikia uvumi huo na wameviagiza vyombo vya usalama vilifanyie uchunguzi.
CHANZO :http://www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment