Sunday, July 15, 2012

Baraza la madiwani Meru latoa mwezi mmoja gari la kubebea wagonjwa kuanza kazi


BARAZA la madiwani la halmashauri ya wilaya ya Meru wilayani Arumeru mkoani Arusha limetoa mwezi mmoja kwa  idara ya Afya katika halmashauri hiyo kuhakikisha kuwa gari la kubebea wagonjwa (Ambulance) liwe limeshatoka kwenye matengenezo na kuanza kutoa huduma kwa wananchi wake.

Hayo yameelezwa hivi karibuni  katika baraza la madiwani hao lililofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo, kutokana na kuwa Ambulance hiyo imekuwa ikifanyiwa matengenezo kwa muda mrefu sana na wagonjwa kuendelea kuteseka sana hususani wanawake .

Akizungumza katika baraza hilo,Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Godson Majola alisema kuwa , lazima idara hiyo ihakikishe kuwa inafanya liwezekanalo ndani ya mwezi mmoja gari la kubebea wagonjwa liwe limeshatengemaa na kuhudumia wagonjwa kama kawaida kwani wengi wao wanapata shida kubwa sana.

Alisema kuwa,kutokana na kuwepo kwa adha ya gari la kubebea wagonjwa katika wilaya hiyo , wagonjwa wamekuwa wakitumia bajaji kupelekwa hospitali hali ambayo  amesema kuwa haisaidii kabisa kwani bajaji hazina uwezo wa kumwahisha mgonjwa aliyezidiwa hospitali.

Aliongeza kuwa, hali hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa sana kuzorota kwa huduma za afya katika  hospitali mbalimbali kutokana na kutokuwepo kwa usafiri huo na hivyo kuwapelekea wananchi kupata hadha kubwa , kwani bajaji zinazotumika hazifai na wala hazirahisishi huduma kwa wagonjwa hao.

Akichangia mada katika baraza hilo,Diwani wa kata ya Makiba wilayani Arumeru , Mwanaidi Hamis Kimu alisema kuwa, kukosekana kwa gari hiyo ya kubebea wagonjwa imepelekea wanawake kuendelea kuteseka zaidi hususan kipindi cha kutaka kujifungua huku ikilinganishwa kuwa wengi wao wanaishi maeneo yaliyo mbali.

Alisema kuwa, ni vizuri gari hilo likafanyiwa marekebisho haraka iwezekanavyo ili kuokoa maisha ya watu walio wengi ambao ndio wanateseka , wakati gari hilo likiendelea kufanyiwa  marekebisho kwa muda mrefu sasa likifanyiwa matengenezo bila kuwepo kwa taarifa za uhakika.

'Ninaombeni jamani tuwe makini na maisha ya wananchi wetu kwani wanaoteseka zaidi ni wanawake wanapoenda kupata huduma za matibabu hususani wanawake wajawazito, kwani wengi wao wamekuwa wakijifungulia hata njiani jamani kutokana na kuwepo kwa changamoto hiyo,naomba idara husika ihakikishe ndani ya huo mwezi gari ifanze kazi ya  kuhudumia wananchi 'alisema Mwanaidi.

Katika hatua nyingine , baraza hilo limeagiza kamati ya fedha katika halmashauri hiyo kushughulikia kwa haraka utata unaojitokeza kwenye masoko mbalimbali ya wilaya hiyo ,kutokana na kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara wadogo wadogo kutozwa ushuru mara mbili.

Aidha kufuatia utata huo, baraza hilo limeitaka kamati kuweka mipango madhubuti ambayo itaondoa utata huo na kuweka utaratibu utakowezesha wafanyabiashara kulipa ushuru mara moja tu .

Kwa upande wake, Mkugenzi wa halmashauri hiyo,Trisias Kagenzi amelieleza baraza hilo kuwepo kwa utaratibu wa kupandisha mishahara na vyeo kwa watumishi wote wa serikali katika halmashauri hiyo kutokana na serikali kuu kurudisha mamlaka hiyo kwenye halmashauri.

Alisema kuwa, hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa sana kurahisisha usumbufu uliokuwepo kwa wafanyakazi hao kufuata fedha zao hazina na wakati mwingine kukuta fedha zao hazijaiingia benki, hivyo kupitia mfumo huo utarahisisha kwa kiasi kikubwa sana wafanyakazi kuweza kupata haki zao kwa wakati na kuondoa malalamiko.

No comments: