WAKAZI wa Temboni Mtaa wa Kimara ‘B’ na Upendo jijini Dar es Salaam, wameliomba jeshi la polisi, kutoa ushirikiano wa dhati katika kupambana na wimbi la majambazi lililoshamiri maeneo hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Diwani wa Kata ya Saranga Efraimu Kinyafu (Chadema),alieleza kuwa awali maeneo hayo yalikuwa na matukio ya ujambazi wa kutisha ambao ulisababisha baadhi ya watu kupoteza maisha yao huku wengine wakipata ulemavu.
Alichanganua kuwa kutokana na wimbi hilo la majambazi mwaka 2010 hadi 2011 jeshi la polisi kwa ushirikiano wa wananchi liliweka askari wa doria kwa masaa 24 ambao kwa pamoja walifanikiwa kutokomeza majambazi hao ila kwa sasa wimbi hilo limejitokeza kwa mara nyingine tena.
“Majambazi hao wameanza kujitokeza tena katika maeneo ya upendo, kimara, temboni maduka saba, na wanatumia silaha vikiwemo vitu vyenye ncha kali kwa kuvamia maduka na kupora fedha pamoja na kuacha madhara mbalimbali kwa wananchi.
Hata hivyo, diwani huyo alitumia fursa hiyo kuwataka askari polisi wa kituo cha Mbezi Luis kuwa makini katika kutekeleza kazi zake badala ya kuwa chachu ya kusababisha vifo kwa wananchi wasiokuwa na hatia.
Mbali na hilo diwani huyo alidai kuwa askari polisi waliopo kwa sasa katika kituo hicho hawana ushirikiano kama walivyokuwa awali,kwani wamekuwa wakiwashinikiza wananchi kutumika kama askari wa ulinzi shirikishi.
“Katika hili kuna baadhi ya uzembe unafanywa na kituo hicho, mfano hivi karibuni kuna kijana mmoja mwendesha bodaboda alipoteza maisha yake baada ya kujigonga katika nguzo ya umeme wakati akiwakimbia polisi waliokuwa wakimfukuza wakimshuku kuwa ni mhalifu alifafanua Kinyafu.
Naye Kamanda wa polisi Mkoa wa Kinondoni Charlrs Kenyela alishangazwa na tukio la kijana huyo ambalo hadi sasa halijafikishwa ofisini kwake, ila akahaidi kutoa ushirikiano pindi taarifa hizo zikiwasili kwake.
No comments:
Post a Comment