Friday, September 7, 2012

TANESCO YATWISHWA MZIGO WA DENI

Mahakama Kuu Yaamuru Tanesco Iilipe Dowans

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia mbali maombi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kutaka isitishe utekelezaji wa malipo ya Sh96 bilioni kwa Kampuni ya Kufua Umeme ya Dowans kutokana na kuvunja mkataba wa kibiashara kinyume na sheria.

Kufuatia uamuzi huo, Tanesco sasa inatakiwa kuilipa Dowans kiasi hicho cha fedha ambacho kwa ujumla kinaliongezea shirika hilo mzigo wa madeni.

Tanesco kupitia mawakili wake Rex Attorneys iliwasilisha mahakamani hapo maombi mawili; kibali cha kukata rufaa kupinga hukumu ya Mahakama hiyo iliyotolewa Septemba 28, 2011 na kuomba kusimamishwa kwa utekelezwaji wa hukumu hiyo.

Katika hukumu ya awali iliyotolewa na Jaji Emilian Mushi, mahakama hiyo ilikubali maombi ya Tuzo kwa Dowans iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC), Novemba 15, 2010.
ICC iliamuru Tanesco kuilipa Dowans fidia ya Dola za Marekani billion 65,812,630.03, kutokana na kuvunja mkataba wa kibiashara kinyume cha sheria. Mahakama Kuu Tanzania ilikubaliana na tuzo hiyo na kuipa kampuni hiyo nguvu ya kisheria.

Hata hivyo, Tanesco haikuridhika na hukumu hiyo, badala yake ikawasilisha mahakamani hapo taarifa ya kusudio la kukata rufaa kuipinga.

Jana, kwa mara nyingine mahakama hiyo iliendelea kubariki Dowans kupewa tuzo hiyo na kutupilia mbali maombi ya Tanesco, ikiwamo pingamizi la utekelezaji wake.
Katika uamuzi wake aliousoma jana asubuhi, Jaji Dk Fauz Twaib alikubaliana na hoja za Wakili wa Dowans, Kennedy Fungamtama kwamba mahakama hiyo haina mamlaka kisheria kusimamisha utekelezaji wa malipo hayo baada ya hukumu ya ICC.

Awali, wakili Fungamtama katika hoja zake, alidai kuwa maombi hayo yamefunguliwa chini ya Kanuni ya 11 (2) na ya 47 ya Mahakama ya Rufani ya Tanzania ya mwaka 2009.
Alidai kuwa kanuni hiyo ya 47 inatumika kwa maombi ambayo Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu nchini zina mamlaka ya kisheria lakini, katika maombi hayo ya Tanesco kusimamisha utekelezaji wa malipo hayo, mahakama kuu haina mamlaka hayo.

Kwa mujibu wa Fungamtama, kanuni ya 11(2) (b) ya kanuni za Mahakama ya Rufani za 2009, zinaihusu Mahakama ya Rufani tu na kwa maana hiyo, ni Mahakama ya Rufaa pekee ndiyo inaweza kusimamisha utekelezwaji wa malipo.
Hata hivyo, wakili wa Tanesco aliyejitambulisha kwa jina la Mwandambo akijibu hoja za Wakili Fungamtama alidai kuwa, kanuni hizo zinaipa nguvu mahakama hiyo kusimamisha utekelezaji wa malipo iliyotolewa katika mahakama hiyo ambazo zinakatikwa rufaa katika Mahakama ya Rufaa.

Lakini, Jaji Dk Twaib alikubaliana na hoja za wakili Fungamtama kwamba kifungu cha kanuni ambacho Tanesco ilikitumia katika maombi hayo, hakiipi mamlaka Mahakama Kuu kusimamisha utekelezaji wa hukumu zake.
Jaji Dk Twaib alisema kuwa, namna na masharti ya kusimamisha utekelezaji wa hukumu yalivyoainishwa katika kifungu (d) cha kanuni hizo za Mahakama ya Rufani.

Alisema kama Wakili Fungamtama alivyoeleza kwa usahihi, kanuni hizo zinaihusu Mahakama ya Rufaa tu kama ilivyoainishwa vizuri katika Kanuni ya 3 ya Kanuni za Mahakama ya Rufaa za mwaka 2009.

“Mheshimiwa Jaji Mkuu anatambua msimamo wa kisheria uliowekwa katika maamuzi mbalimbali kwa misingi kwamba, mchakato wa rufaa unapokuwa umeanza kwa kuwasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa, mahakama hii inakoma kuwa na mamlaka ya kusimamisha utekelezaji wa hukumu,”, alisema Jaji.
Jaji Dk Twaib alisema mahakama hiyo inaweza kuwa na mamlaka hayo kabla kuwasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa.

“Mara tu taarifa ya kusudio la kukata rufaa inapokuwa imewasilishwa (kama ilivyo katika kesi hii), Mahakama Kuu inakoma kuwa mamlaka,” alisisitiza Jaji Dk Twaib na kuongeza:

“Kwa misingi iliyoelezwa mahakama hii haina mamlaka ya kisheria kushughulikia maombi ya kusimamisha utekelezaji yaliyowasilishwa na muombaji (Tanesco)”, alihitimisha uamuzi wake Jaji Dk. Twaib.

Sakata lenyewe Mwaka juzi jopo la majaji watatu wa ICC lilitoa uamuzi wa kuitaka Tanesco kuilipa Dowans Tuzo ya Sh96 bilioni, kutokana na madai ya kuvunja mkataba wa kibiashara kinyume cha sharia. Hata hivyo, uamuzi huo umekuwa ukipingwa na baadhi ya watu wakisema Dowans ilirithi mkataba haramu wa Richmond hivyo, mkataba huo haukuwa halali.

Tanesco nayo kwa upande wake, katika maombi yake ilidai kuwa kama mchakato wa utekelezaji wa hukumu hiyo utaendelea, itaathiri uwezo wake wa kuzalisha na kusambaza umeme nchini na hivyo kusababisha tatizo kubwa la ukosefu wa umeme nchini na hivyo kuathiri uchumi wa nchi kwa jumla.

Pia lilidai kuwa iwapo maombi yao hayatakubaliwa itapata hasara kubwa na hivyo kuathiri kwa kiwango kikubwa utendaji wake na hata kuleta wasiwasi wa kusimama kwa shughuli zake za kila siku. Mawakili hao walisihi mahakama hiyo kuzingatia maombi hayo kwa madai kuwa hasara itakayotokana na tatizo la ukosefu wa umeme itakuwa ni kubwa na isiyoweza kufidiwa kwa namna yoyote ile.

Walidai kuwa ingawa taarifa ya kusudio la kukata rufaa siyo kigezo cha kuzuia utekelezaji huo, lakini kwa hoja za kesi yake ni nzito kiasi cha kutosha kuifanya mahakama kutumia uwezo wake wa kisheria kuzingatia maombi yao. “Mahakama ina uwezo wa kuamuru kusimama kwa utekelezaji huo kwa namna itakavyoona inafaa.”, walisisitiza mawakili hao wa Tanesco katika maombi hayo.

Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz/habari

No comments: