MADARAKA NYERERE ABISHANA NA RAIS MSITAAFU MKAPA
MADARAKA
Nyerere ambaye ni mtoto wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere,
ameibuka na kuthibitisha kuwa Mbunge wa sasa wa Musoma mjini (Chadema),
Vincent Nyerere ni mdogo wao na mwanafamilia hiyo, kwani ni mtoto wa
baba yao mdogo, Josephat Kiboko Nyerere.
Kauli
ya Madaraka imekuja siku chache baada ya Rais mstaafu wa awamu ya tatu
Benjamin Mkapa, kudai kwamba hamtambui mbunge huyo kuwa ni miongoni mwa
familia ya Mwalimu Nyerere kwani katika kipindi chote alichofanya kazi
na Mwalimu, hakusikia jina hilo.
Jumatatu ya
wiki, akizindua kampeni za CCM katika uchaguzi mdogo wa Arumeru
Mashariki, mkoani Arusha, Mkapa aliuambia umati uliohudhuria kwamba
hakuwahi kusikia kama kulikuwa na mtoto wa familia hiyo aliyekuwa
akiitwa Vincent Nyerere.
Kauli hiyo ilipingwa vikali juzi na Vincent akisema si jambo la
ajabu Mkapa kutomfahamu yeye kwasababu Mkapa si sehemu ya ukoo wao huku
akimrushia kombora kwamba akiwa madarakani alishinikiza Mwalimu Nyerere
kupelekwa Hospitali ya St Thomas, Uingereza, kinyume na matakwa ya
familia yao na wakati huo huo, daktari wake Profesa David Mwakyusa
alijua maradhi ya mwasisi huyo wa taifa.
Vincent
alikwenda mbali zaidi na kumshambulia Mkapa kwa kuongoza ubinafsishaji
holela enzi za utawala wake huku akimtuhumu kuuza viwanda na rasilimali
za nchi kwa kisingizio cha ubinafasishaji.
Jana
gazeti hili liliwasiliana na Madaraka kutaka kupata ukweli wa kauli
hiyo ya Mkapa. Katika jibu lake fupi, Madaraka alithibitisha kuwa
Vincent ambaye sasa ni Meneja Mwenza wa Chadema katika kampeni za
Arumeru Mashariki, ni mmoja wanafamilia ya Mwalimu Nyerere ambayo
chimbuko lao ni Kijiji cha Butiama mkoani Mara.
Katika
jibu lake alilolituma kwa barua pepe Madaraka alisema; “Naomba kutoa
maelezo yafuatayo kuhusu yanayozungumzwa kwenye kampeni za uchaguzi wa
Arumeru; Ili kuepuka kujiingiza kwenye masuala ya kampeni, nitajibu
sehemu ndogo sana ya maswali yako”.
Aliongeza
“Nataka kuthibitisha tu kuwa Mhe. Vincent Nyerere ni ndugu yetu, mtoto
wa marehemu baba yetu mdogo, Mzee Josephat Kiboko Nyerere. Hayo maswali
mengine naomba yaelekezwe kwa Mhe. Benjamin Mkapa au Mhe.Vincent
Nyerere”.
Maswali mengine ambayo Madaraka
aliulizwa na Mwananchi ni pamoja na kwamba; Nani alishinikiza Mwalimu
Nyerere kupelekwa St Thomas, Uingereza na kama familia hiyo iliridhia
apelekwe Uingereza au nchi nyingine za Kijamaa.
Madaraka pia aliulizwa anamtambuaje Vincent Nyerere, Ni mmoja wa familia hiyo ama la?
Akizindua kampeni za CCM kwenye uwanja wa michezo wa Ngaresero, Usa River Jumatatu wiki hii, Mkapa alisema:
“Nimefanya
kazi na Mwalimu kwa miaka 25, nikiwa mwandishi wake, Waziri na katika
muda huo, nimemzika yeye, kaka yake na mama yake mzazi, sijawahi kusikia
jina la mtu kama huyo katika familia ya hiyo”.
Vicent
alimtaka pia Mkapa kuacha kujiingiza katika masuala ya familia
yasiyomuhusu na kwamba akiwa Rais mstaafu, ana kashfa nyingi zinazougusa
utawala wake wa awamu ya tatu.
Chadema wazidi kumlipua
Katika
hatua nyingine, Mkapa amezidi kulipuliwa katika kampeni za uchaguzi huo
mdogo baada ya mbunge mwingine wa Chadema, Israel Natse wa jimbo la
Karatu na Peter Msigwa wa Jimbo la Iringa, kumtaka Rais huyo mstaafu na
Serikali ya CCM kumuogopa Mungu kutokana na kuwadanganya wananchi wa
Meru kuwa wakimchagua mgombea wa CCM watarudishiwa ardhi yao ambayo
inamilikiwa na walowezi.
Wakizungumza katika
mikutano tofauti ya kampeni jana, katika Kijiji cha Njeku na Sura,
wachungaji hao, walisema kama Mkapa alikaa madarakani miaka 10
akashindwa kurejesha ardhi inayomilikiwa na walowezi itakuwaje, leo yupo
nje amshauri Rais Kikwete kurejesha ardhi hiyo?"
Natse
alisema, “Ndugu zangu msidanyanyike na kuendelea kuwasikiliza CCM miaka
yote wameshindwa kurejesha ardhi ya Meru sasa wanaibuka…..huyo Mkapa
alishindwa akiwa rais sasa amekaa nyumbani akisubiri posho ataweza
kumshauri rais awarudishie ardhi yetu?”
Wakati
akizindua kampeni za CCM Machi 12 mwaka huu, Mkapa alisema CCM
inatambua tatizo kubwa la ardhi katika jimbo hilo kwani kuna ardhi kubwa
ambayo inamilikiwa walowezi na kuna maeneo ambayo hayatumiki ipasavyo
kwa mujibu wa hati
miliki na tayari utambuzi umefanyika.
Mkapa
alisema atamshauri Rais Kikwete kuchukuwa hatua kuhusiana na tatizo
hilo, na kama kuna watendaji ambao watakwamisha watachukuliwa hatua.
Naye
Mchungaji Msigwa, alisema moja ya sifa ya kuwa mwana CCM ni
kutomuogopa Mungu kwa kuwa mwongo, mtu wa kujipendekeza na mpenda rushwa
mambo ambayo
Chadema hayapo.”
Alisema tatizo la Ardhi Meru litamalizwa na Wameru wenyewe na sio CCM kwani ndio waliosaidia kutoa ardhi kwa walowezi.
CCM wajibu mapigo
Katika
kampeni zilizoanza rasmi jana baada ya uzinduzi uliofanyika Jumatatu
wiki hii, CCM kimebeba ajenda ya kufuta kile kinachodaiwa kuwa ni
uongozi wa kifalme unaotaka kujengwa ndani ya chama hicho.
Ajenda
hiyo inatokana na madai ambayo yamekuwa yakitolewa kwenye mikutano ya
Chadema kwamba wasimchague mgombea wa CCM, Siyoi Sumari kwani kwa
kufanya hivyo watauegeuza ubunge wa Arumeru Mashariki kuwa Ufalme kwani
watakuwa wanamrithisha mgombea huyo nafasi iliyoachwa wazi na baba yake
mzazi.
Meneja wa kampeni wa CCM, Mwigulu Nchemba
akimnadi Sioi jana alisema: “Chadema ndio vinara wa sera ya utawala wa
kifalme na kwamba kudhihirisha hilo, baadhi ya wabunge wa chama hicho
wameamua kusaidia watoto wao, wake pamoja mashemeji zao kupata nafasi
ndani ya Bunge”.
Akihutubia mikutano ya kampeni
katika sehemu za Shambarai, Msitu wa Mbogo na Mbuguni madukani, Nchemba
aliwashutumu Chadema kwamba ndani ya chama hicho wamekuwa wakipeana
nafasi kindugu.
Mwigulu alidai kuwa
Katibu Mkuu wa chama hicho,Dk Willibrod Slaa baada ya kuacha ubunge
aliyekuwa mke wake, Rose Kamili amechaguliwa kuwa mbunge wa Viti maalumu
kutoka mkoa wa Manyara.
Kwa upande wake mbunge wa
Mtera (CCM), mkoani Dodoma, Livingstone Lusinde amekipiga vijembe
Chadema kwa madai kwamba kinatumia alama ya vidole viwili kama manati
huku akiwaambia wakazi wa Shambarai manati kamwe haiwezi kuua tembo.
Lusinde
alisema kwakuwa Chadema wamekuwa wakiendeleza sera za matusi katika
mikutano yao ya kampeni, nao (CCM) watamwomba mwenyekiti wao, Rais
Jakaya Kikwete kuwapa ruksa ya kujibu mapigo.
Naye
mbunge wa Simanjiro (CCM) mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka
akimpigia debe Sumari alisema atahakikisha anashirikiana naye pindi
atakapopatiwa ridhaa kuwa mbunge kutatua tatizo la ajira wilayani humo
kwa kuwatafutia ajira katika mgodi wa madini wa Tanzanite One uliopo
wilayani Simanjiro mkoani Manyara.
Wagombea wa
pande hizo mbili Sioi wa CCM na yule wa Chadema, Joshua Nassari
waliendelea kunadi sera za vyama vyao pamoja na kutoa ahadi kadhaa kwa
wapigakura, huku suala la ardhi likionekana kupewa nafasi kubwa katika
kampeni hizo.
Sioi kwa upande wake alisema ikiwa
atachaguliwa atashughulikia kero za maji, barabara, uhaba wa masoko,
ajira na migogoro ya ardhi.
Alisema migogoro ya
ardhi wilayani humo ni tatizo la muda mrefu na kwamba suala hilo ni moja
ya mambo ambayo atalitafutia suluhu ikiwa atachaguliwa kuwa mbunge.
Alitaja
tatizo jingine kuwa ni uhaba wa ajira kwa vijana na kwamba tatizo hilo
atalishughulikia kwa kufungua vituo vya elimu ya ujasiriamali wilayani
humo ili waweze kutambua njia za kujiajiri badala ya kusubiri ajira za
Serikali.
Naye mjane wa mpigania ardhi ya Wameru,
Nderetwa Kirilo (85), amembariki Mgombea Ubunge wa Jimbo hilo kwa
tiketi ya Chadema, Joshua Nassari kwa kumshika kichwa Kaman ishara ya
kumkubali na kumtaka kulinda haki za Wameru kama alivyokuwa mume wake
Japhet Kirilo aliyefariki dunia Mei 30 mwaka 1997.
Akizungumza
jana nyumbani kwake katika kata ya Poli, mara baada ya kumbariki
mgombea ubunge huyo wa Chadema, alisema yeye anambariki hata kama ni
mgombea wa upinzani, ili mradi anaamini kuwa ataleta maendeleo kwa watu
wa Meru.
Kwa upande wake Nassari
alimshukuru bibi huyo na kumwaahidi kuendeleza aliyoasisi Mzee Kirilo
kwa kutete haki za wameru hasa kaika suala la ardhi.
Naye
Nyerere alisema chama hicho, kina ushahidi wa kutosha juu ya utata wa
Uraia wa Sumari na kuna taarifa kuwa sio mtoto wa kuzaa wa mke wa Sumari
ambaye alikuwa Mtanzania.
“Sisi tunataka sheria ifuate mkondo
sio kutaka kusafishana na tunaomba ieleweke kuwa hatumuogopi Siyoi
kwani tunajua tutashinda mapema asubuhi”alisema Nyerere.
Hata
hivyo, akizungumza na waandishi wa habari juzi,Msimamizi wa Uchaguzi wa
jimbo la Arumeru Mashariki, Trasias Kagenzi, alisema majibu ya rufani
ya Tume ya Taifa ya uchaguzi yatatolewa ndani ya siku saba .
Imeandikwa na Ramadhan Semtawa Dar, Musa Juma, Arumeru
Send to a friend |
MICHEZO NA BURUDANI NDANI YA NCHI | ||||||||||
Sweetbert Lukonge
MABINGWA
watetezi, Yanga leo watarudi kwenye nafasi yao ya pili kama
watafanikiwa kuichapa Villa Squad katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania
Bara utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Yanga
ina pointi 40 baada ya kucheza michezo 19, ikiwa nyuma ya Azam kwa
pointi moja na nne kwa vinara wa ligi Simba wenye pomti 44, ambapo Azam
watashuka dimbani kesho kuikabili Ruvu JKT huku Simba ikicheza na
Mtibwa Sugar.
Pamoja na Yanga kuwapoteza nyota wake kadhaa, katikati ya wiki hii ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya African Lyon na kurudisha matumaini yao kwamba wanaweza kutetea taji lao. Mabingwa hao watetezi wataingia uwanjani wakiwa na tumaini la kuendeleza kasi ya ushindi dhidi ya vibonde wa ligi Villa Squad yenye pointi 16 ambayo inaonekana kama imekubali kushuka daraja msimu huu. Kocha wa Villa, Habibu Kondo alisema wao wana nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi kwenye mechi ya leo kutokana na maandalizi mazuri waliyofanya. "Hatuwaogopi Yanga na tumejipanga kuhakikisha tunaibuka na ushindi kwenye mchezo wa leo kama ilivyokuwa kwa Simba," alisema Kondo. Villa Squad iliwashangaza watu mwaka huu pale ilipowafunga Simba bao 1-0 ukiwa ni moja ya ushindi wake wa nne katika mechi 19 ilizocheza msimu huu. Nahodha wa Villa, Nsa Job atakuwa na kazi moja ya kuhakikisha anawaongoza wenzake kuifunga timu yake ya zamani ya Yanga ili kufufua matumaini yao ya kubaki Ligi Kuu. Pamoja na kushikilia mkia, Villa imefanikiwa kufunga mabao 20 wastani wa bao moja kwa mechi huku nahodha wao Job akiwa amezifumania nyavu mara nane. Ubora huo wa safu ya ushambuliaji wa Villa ni kitu ambacho kocha Kostadin Papic wa Yanga anapaswa kuutafakari na kuangalia upya ukuta wake ulioruhusu mabao 16 wavuni msimu huu. Kurejea kwa kiungo Haruna Niyonzima katika mechi hii kumetoa faraja mpya kwa kocha Papic. Niyonzima atakuwa na jukumu moja la kuwatengenezea nafasi washambuliaji wake Kenneth Asamoah na Davies Mwape na kuna shaka kwamba wataendelea kusababisha maafa kwa ngome ya Villa iliyoruhusu mabao 40. Kwa mara nyingine Shirikisho la Soka Tanzania TFF, limemteua mwamuzi Oden Mbaga mwenye beji ya Fifa kuchezesha mechi ya Yanga katika kipindi cha siku nne. Mwamuzi Mbaga ndiye aliyechezesha mechi ya Jumatano iliyopita wakati Yanga iliposhinda 1-0 dhidi ya Lyon. Mechi nyingine ya leo itachezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, ambapo Coastal Union watakuwa wenyeji wa Oljoro JKT ya mkoani Arusha. Ligi itaendelea tena kesho kwa mechi mbili wakati vinara wa ligi Simba watakapokuwa wageni wa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro wakati Azam watakuwa wenyeji wa Ruvu Shooting Stars kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam. Simba na Azam zitaingia uwanjani kwa lengo moja la kupata ushindi na kuendelea kubaki katika nafasi mbili za juu. Simba pia watautumia mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar kama sehemu ya maandalizi yao ya mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya ES Setif ya Algeria utaofanyika wiki ijayo.
|
No comments:
Post a Comment