SAKATA LA MADAWA YA KULEVYA LIYUMBA KITANZINI ATAKIWA KUTUPWA RUMANDE HARAKA KUTOKANA NA SHINIKIZO LA VIGOGO.
APONZWA NA MWANAYE SAKATA HILO LINASEMEKANA KUMHUSISHA ASKOFU.
Morine Amatus.
Madawa ya kulevya waliyokutwa nayo akina Morine na wenzake.
Na Eliud RussetaLILE sakata la msichana Morine Amatus (22), anayetajwa kuwa ni mtoto wa Amatus Liyumba, aliyekamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Lindi, akiwa na wenzake watatu, wakidaiwa kukutwa na madawa ya kulevya ya kilo 210 , yenye thamani ya shilingi Bilioni 9.4 limeingia katika sura mpya baada ya baba yake (Morine) kutakiwa kukamatwa, hivyo kuingia kitanzini.
Habari za uchunguzi kutoka ndani ya jeshi la polisi zinadai kuwa Liyumba anaingia kitanzini kwa kuwa anatakiwa akamatwe na ahojiwe kuhusiana na madawa hayo kwa kuwa mtoto wake amedaiwa kuhusika na tayari katupwa gerezani akisubiri kesi yake kusikilizwa.
Chanzo chetu ndani ya jeshi la polisi kimesema kumekuwa na shinikizo kutoka serikalini kwa waziri mmoja (jina limehifadhiwa) kutaka Liyumba akamatwe na kutupwa rumande kwa kile kilichodaiwa kuwa, ili upelelezi uweze kufanyika kwa kina.
Alipoulizwa kwa njia ya simu na mimi Jumapili iliyopita, Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya Tanzania, Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Polisi, Godfrey Nzowa hakukiri wala kukataa kuhusu kukamatwa Liyumba ili uchunguzi ufanyike.
“Ninachoweza kusema ni kwamba uchunguzi juu ya tukio lile unaendelea. Kuhusu Liyumba ni kwamba mtoto wake ana miaka 22, hivyo ni mtu mzima kuna mambo anaweza kuyafanya bila baba yake kujua, lakini kama uchunguzi utatutaka baba yake akamatwe kuhojiwa, hatuwezi kushindwa kufanya hivyo,” alisema Kamanda Nzowa.
Alipododoswa zaidi, kamanda huyo alisema kwa kawaida polisi wanapofanya uchunguzi wao hawawezi kusema ni nani akamatwe na kuhojiwa na wala huwa hawasemi nani amewapa taarifa za mtu anayechunguzwa.
“Hizo ni kanuni zetu, hatuwezi kusema nani atakamatwa kwa jambo fulani au kumtaja mtu ambaye ametuletea taarifa za watu wanaojihusisha na madawa ya kulevya na ndiyo maana tunafanya kazi vizuri sana, nawaomba wananchi wema wazidi kutupa ushirikiano,” alisema Nzowa.
Hata hivyo, Nzowa alifafanua kuwa kutokana na wingi wa madawa waliyokamatwa nayo, mtoto huyo wa Liyumba na wenzake, kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa itapelekwa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Watuhumiwa wengine waliokamatwa pamoja na Morine katika Kijiji cha Mchinga Mbili, Lindi kwa mujibu wa Nzowa na kufikishwa mahakamani ni Pendo Mohamed Cheusi (67), mkazi na mkulima wa kijiji hicho na Hemedi Said (27), dereva na mkazi wa Mtoni, jijini Dar es Salaam ambaye pia ni mtoto wa mwenye nyumba hiyo.
Aliwataja watuhumiwa wengine kuwa ni Ismail Adamu, kwa jina lingine Athuman Mohamed Nyaubi (28), mfanyabiashara wa magari nchini Afrika Kusini na mkazi wa Morocco jijini Dar es Salaam.
Morine Amatus ni mkazi wa Mikocheni ‘B’ jijini Dar es Salaam na baba yake (Liyumba) alikuwa Mkurugenzi wa Utumishi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na aliwahi kufungwa miaka miwili, Mei 24, 2010 kwa makosa ya kutumia vibaya ofisi ya umma.
NZOWA ATAHADHARISHA
“Niwatahadharishe wale wote wanaofanya au kufikiria kufanya biashara hii haramu ya dawa za kulevya, waache kwa sababu polisi kwa kushirikiana na raia wema tumejipanga. Maeneo yote siku hizi tunayalinda, watakaojiingiza ni lazima watakamatwa tu,” alionya.
Kamanda Nzowa amewashukuru wote waliofanikisha kutoa taarifa ya kuwepo kwa madawa nchini na amewataka kuendelea kushirikiana na jeshi lake kwani alidai wote wanaokoa taifa na kuwa na watu mazezeta.
UCHUNGUZI WETU
Uchunguzi uliofanywa na FOUR WAYS BUKOBA umegundua kuwa watuhumiwa hao wanahusishwa na askofu mmoja, Moris Charles ambaye inadaiwa amekimbilia nje ya nchi.
Tayari magari yake matatu yamedakwa na polisi wakati upelelezi ukiendelea huku kukiwa na taarifa kuwa familia yake ameitoroshea nje ya nchi.
Na Eliud
Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harisson Mwakyembe.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harisson Mwakyembe.
Na Eliud ADUI namba moja wa Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harisson Mwakyembe ametajwa kuwa ni yule aliyevumisha na kusambaza ujumbe kwa watu mbalimbali kuwa kiongozi huyo amefariki dunia.
Chanzo chetu cha habari ambacho ni mmoja wa wanafamilia wa Dk. Mwakyembe kimeliambia gazeti hili kuwa adui huyo wa ndugu yao, familia inamjua lakini hivi sasa ni mapema mno kumtaja.
“Tunamjua tena ni mbunge kupitia Chama Cha Mapinduzi. Hatuwezi kumtaja kwa sasa lakini nakuhakikishia tunamjua,” kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, msemaji wa Dk. Mwakyembe ambaye pia ni Mbunge wa Kyela, Victor Mwambalaswa alimwambia mwandishi wetu kuwa ni kweli kuna mtu alizusha na kusambaza habari za kifo cha mpendwa wao.
“Hawa wanaoeneza uvumi huo wanasikitisha, kuishi au kufa ni mipango ya Mungu. Sijui anayeeneza hayo ana makusudi gani?” alihoji Mwambalaswa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Lupa.
Alisema Dk. Mwakyembe ni mzima wa afya na angezungumza na waandishi wa habari jana (Jumatatu) baada ya kurejea kutoka India mwishoni mwa wiki iliyopita.
Dk. Mwakyembe amekuwa akisumbuliwa na maradhi ya ngozi ambayo Oktoba 9, mwaka jana yalimlazimu kupelekwa katika Hospitali ya Apollo, India kwa matibabu zaidi.
Maradhi hayo yamezua utata mkubwa baada ya kudaiwa kuwa yametokana na kulishwa sumu huku kukiwa na kauli zinazotofautiana kutoka kwake na baadhi ya watendaji wengine wa serikali.
Kauli tete ziliibuka baada ya baadhi ya viongozi akiwamo Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta kudai kuwa maradhi yanayomsumbua Dk. Mwakyembe yametokana na kulishwa sumu.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Manumba alijibu madai hayo aliposema kuwa uchunguzi wa polisi umebaini kuwa Dk. Mwakyembe hajaugua kwa sababu ya kulishwa sumu bali ana maradhi ya ngozi na kutishia kuwachukulia hatua waliotoa kauli hizo.
Ripoti ya uchunguzi aliyoisoma Manumba katika mkutano wake na waandishi wa habari Februari 16, mwaka huu Dar es Salaam, inaonyesha kuwa Dk.Mwakyembe hakulishwa sumu huku akisema kwamba pia ulijumuisha taarifa kutoka hospitalini India ambako alikuwa anatibiwa.
Alisema uchunguzi huo unalipa jeshi la polisi picha kuwa waliotoa taarifa hizo hadharani wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria.
Baada ya kauli hiyo, Dk. Mwakyembe aliibuka na kutoa kauli nzito iliyoonekana kumjibu Kamishna Manumba akielezea kushangazwa kwake na majibu hayo na kudai kuwa hayakuwa sahihi.
Mbali ya Dk. Mwakyembe, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha, kwa nyakati tofauti walikana kuijua ripoti hiyo ya Kamishna Manumba na kila wanapobanwa anamtupia ‘mzigo’ kachero huyo mkuu wa upelelezi nchini.
Hata hivyo, katika kile kilichoonekana kudhamiria kuchukua hatua, inadaiwa kuwa Kamishna Manumba aliwasilisha jalada la mashtaka kwa watu anaodai wanaeneza habari ya kulishwa sumu Mwakyembe kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Eliezer Feleshi ambaye alithibitisha kulipokea lakini akasema ni vigumu kufahamu ni lini atalipeleka mahakamani jalada la kesi hiyo.
No comments:
Post a Comment