Friday, April 6, 2012

BI. HARUSI HAINGIA MITI SIKU YA NDOA

Ndugu, wageni waalikwa wakiwa na simanzi.
Ukumbi ukiwa mtupu baada ya tukio hilo.
..Hali ilikuwa hivi ukumbini hapo.
Na Mwandishi Wetu
NDOA iliyokuwa ifungwe kwenye Kanisa la E.A.G.T Manga jijini Mbeya kati ya Bwanaharusi Gervas Shihamba na Bibiharusi Ikupa Ackimu Mwalukosya iligeuka simanzi kufuatia bibiharusi huyo kuingia mitini nusu saa kabla, Amani linashuka na data.
Kwa mujibu wa chanzo chetu ambacho ni rafiki wa karibu wa familia ya bwanaharusi, ndoa hiyo ilikuwa ifungwe Machi 31, 2012 saa 7:00 mchana, lakini mpaka mtumishi wa Mungu anaingia madhabahuni tayari kwa ibada, maharusi hawakuwepo.
Ndoa ilikuwa ifungwe saa saba mchana, lakini mchungaji alisubiri mwisho akachoka, alipoulizia akaambiwa bibiharusi hajafika,” kilisema chanzo hicho.
Kiliongeza kuwa, mpaka hapo, bwanaharusi na ndugu zake walikuwa wamechanganyikiwa kwani sababu za bibiharusi kutotokea zilikuwa zimejaa utata.
SABABU TATA
Awali ilidaiwa kuwa, bibiharusi aligoma kutoka saluni kwenda kanisani kwa madai kwamba gari alilopelekewa kupanda hakulipenda.
“Awali ilisemekana kuwa bibiharusi alitaka kupelekewa gari ndogo aina ya Toyota Cresta, lakini akapelekewa Hiace, kitendo kilichomfanya agome kupanda.
“Lakini baadaye kukazuka minong’ono kuwa, familia ilimkatalia bibiharusi kwenda kufunga ndoa kwa sababu bwanaharusi alikuwa hajamaliza kulipa mahari. Sasa mpaka muda huu hakijulikani kipi ni kipi,” kilisema chanzo hicho.
Chanzi kikaendelea kudai kuwa, bwanaharusi na nduguze wakiwa nje ya kanisa zilitolewa shilingi laki mbili (200,000) kupelekwa ukweni, lakini haikujulikana mara moja zilikuwa kwa lengo gani.

WAALIKWA UKUMBINI WALA, WANYWA
Habari zaidi zikadai kuwa licha ya kutokufungwa kwa ndoa hiyo, waalikwa walitingia kwenye Ukumbi wa Kiwira Motel, Soweto, jijini humo kuanzia saa 1:00 usiku wakiamini sherehe za ndoa zinaendelea.
“Waalikwa na baadhi ya ndugu walifika ukumbini saa moja, hata kamati ya harusi ilifika, maana maandalizi yalikuwa yamekamilika, lakini maharusi hawakuwepo.

“Hata hivyo, kutokuwepo kwa maharusi hao  hakukuwafanya waalikwa washindwe kula na kunywa, kasoro kucheza hakukuwepo kwani watu walijawa na simanzi,” kiliongeza chanzo.

MAOMBI UKUMBINI
Habari zaidi zinasema kuwa baadhi ya walokole waliokuwemo ukumbini waliangusha sala ya nguvu wakiikemea roho chafu ya matengano iliyosababisha kutokea kwa hali hiyo.

MWENYETIKI WA KAMATI KIGUGUMIZI
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya harusi hiyo aliposhika maiki kuzungumza hakuweza kuweka wazi kisa cha ndoa hiyo kutokufungwa zaidi ya kuwakaribisha  waalikwa.

USIRI WATANDA WALIPO MAHARUSI
Paparazi wetu alianza jitihada za kuwasaka maharusi hao ili kusikia kutoka kwenye vinywa vyao, lakini hakuna ndugu hata mmoja aliyekuwa tayari kusema neno kuhusu utata huo wala kutoa maelekezo ya sehemu walipo ingawa habari zinasema kila mmoja yupo kivyake.

No comments: