Sunday, May 13, 2012

KIPAJI CHA DOGO.Uchambuzi Wa Olle: Blue Nyepesi Kutawala England; Ni Man City!

Bluu Nyepesi Kutawala England; Ni Man City!
Na Olle Bergdahl Mjengwa,

Wiki ya jana tuliwaona Manchester United na Manchester City wakiumana vikali. Ni katika  pambano kali la ‘ watani wa jadi’ katika historia ya mpira wa Uingereza.
Yawezekana mechi ile imeamua bingwa wa Ligi ya Uingereza, lakini, kubwa zaidi, ilikuwa na maana ya kipekee kwa wapenzi wa Manchester City.
  
Ni kwa sababu, Manchester City siku zote imekuwa ikiishi chini ya kivuli cha ’ kaka zao’ Manchester United.  Lakini, ushindi ule wa Manchester City  umeonyesha kuwa klabu hiyo hatimaye imefika juu kimpira. Manchester City imekuwa bora kuliko Manchster United. Na sasa inaonekana ubingwa kwa Man City  uko jirani sana.

Ikifanikiwa kutwaa ubingwa,  itakuwa ni mara ya kwanza kwa Man City, tangu mwaka 1968, kutwaa tena tena ubingwa wa England.  Na  inawezekana, Man City wataendelea kufanya hivyo kwa miaka mingine kadhaa.

Kwa wakati huu, Manchester City ndio timu bora kuliko zote kwenye Ligi ya Uingereza. Vyovyote vile, ligi hiyo itakavyomalizika, kwangu mimi, Manchester City ndio timu iliyokuwa bora zaidi msimu huu. Wamefunga magoli mengi  kuliko timu nyingine yeyote huku tofauti ya magoli  ikiwa ni magoli 61 ukilinganisha na 53 ya Manchester United na 21 ya Arsenal. Tofauti ya magoli hupatikana baada ya kutoa jumla ya magoli  ya kufunga na yale ya kufungwa.

Msimu huu Manchester City imecheza kandanda ya mashambulizi zaidi  ikiwa na wachezaji ambao mara zote  wamekuwa na hamu ya kuusukuma mpira mbele uwafikie akina David Silva na  Yaya Toure.

Inavyoonekana, hata mwakani, timu hizi mbili; Man City na Man United ndizo zitakazochuana vikali katika kuwania taji la ubingwa  Uingereza.  Hata hivyo, naamini Man City ndio watakaokuja kutwaa tena ubingwa.
Man United  na Man City zote zina vikosi vya kwanza vilivyo imara pale ambapo wanakuwa hawana majeruhi. Tofauti ni hii;  Man City ina kikosi chenye nguvu na kilichokamilika zaidi kuliko Man United. Man City ina zaidi ya mchezaji mmoja aliye bora katika kila nafasi ya uwanjani.

Ina maana, mchezaji mmoja akiumia, haileti tofauti kubwa kwa uchezaji wa timu uwanjani.  Kwa mfano, kama Aguero  ameumia, kuna wachezaji wa kiwango cha dunia wanaoweza kuingia badala yake.  Ni kama vile  Balotelli, Dzeko na  Tevez.  Hawa wote ni wenye uzoefu mkubwa. Man United hawana anasa hii. Kwa mfano, ikitokea Rooney ameumia,  Man United hawana wachezaji wa uhakika wa kucheza badala yake.

Ingewezekana kuwachezesha Chicharito au  Welbeck ambao ni wenye vipaji, lakini, si wa kiwango cha dunia, na si mahiri uwanjani kama ilivyo kwa Rooney, wakati huo huo,  Balotelli na Tevez uwezo wao kwa pamoja ni sawa na Aguero wa Man City.

Na  Man City wana uwezo mkubwa kifedha kuweza kuwanunua machezaji wapya mahiri katika kila msimu. Hivyo, kuwawezesha kutwaa mataji mengi zaidi katika  Ligi ya Uingereza katika miaka ijayo.
Kwa sasa Man United ni timu yenye wakongwe wengi kama tulivyowaona walipocheza na Man City kwenye mechi iliyopita. Wachezaji wao kadhaa ni wazee kimpira. Wachezaji kama Scholes, Giggs, Carrick, Evra na Ferdinand.

Hali hii itawafanya Man United wapate tabu sana msimu ujao . Kocha Alex Ferguson sasa anafanya  kazi ya kubadilisha kizazi katika kikosi chake. Ni   kwa kuwachanganya wachezaji wachanga na wakongwe.
Wachezaji kama  Smalling, Jones, Cleverly, na Welbeck watakuja kukua zaidi kimchezo na kufikia kiwango cha dunia. Lakini, ili wakue kimchezo, watahitaji kupangwa kwenye mechi nyingi zaidi. Hivyo basi, msimu ujao tutakuja kuiona Man United yenye wachezaji wengi vijana.

Hata hivyo, siamini kama Man United yenye wachezaji vijana na wasio na uzoefu wa muda mrefu  wanaweza kuja kuwanyang’anya  ubingwa  Man City iliyosheheni wachezaji nyota.

Isipokuwa, katika miaka michache ijayo, inawezekana, wachezaji kama Smalling and Cleverly watakuwa wamekua kimchezo na kufikia kiwango cha juu na kuifanya Man United kurudi tena katika kiti chake cha ufalme wa soka ya England.

Naamini , ushindi wa hivi karibuni wa Man City dhidi ya Man United  ni mwanzo wa Man City kuelekea kwenye kurithi Ufalme wa soka wa Uingereza utakaokuwa umeachwa wazi na Man United. Na kama Man City itaendelea kuwekeza kwenye wachezaji wapya mahiri,  inawezekana, katika miaka ijayo,  Man City ikatoka kwenye ’ Ubwana mdogo’ na ikawa ndio ’ Kaka mkubwa’ wa Man United.

Olle Bergdahl Mjengwa ni kijana wa miaka 16 aliyedhamiria kujikita katika uchambuzi wa kandanda ya Kimataifa.  Ni mwanafunzi na anaishi Iringa.

No comments: