Sunday, April 8, 2012

Chadema kukata rufaa ya Lema Jumanne


Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema chama chake kimeamua kukata rufaa Jumanne ijayo, ili haki itendeke na kuepushia hasara Taifa ya kurudia uchaguzi bila sababu za msingi.
Akizungumza jana katika mkutano mkubwa uliokusanya umati jijini Arusha, wakiwa na mabango yenye jumbe mbalimbali, kwenye viwanja vya NMC, alisema wameshauriana kwa kina pamoja na baadhi ya majaji wengine walio na hekima, wakaamua kusikiliza ushauri huo na kukata rufaa.
Mbowe ambaye alipanda gari aina ya Benz akiwa na Mbunge Godbless Lema, alionekana kushangiliwa na umati wa watu, huku wakipepea bendera na matawi ya miti, kuashiria kufurahia ujio wao.
“Mahakama Kuu siyo mwisho, hukumu hii imetolewa na jaji siyo mahakama, sababu za shinikizo la watawala, ila lengo lao kuondoa silaha hii ya Lema, ambayo wanajisumbua, kwa sababu silaha hii itatumika kufanya kazi ya kujenga chama nchi nzima,” alisema.
Alisema Mbowe kuwa rufaa inapaswa kusikilizwa ndani ya miezi 12 ila wao kama Chama wataomba ikiwezekana isikilizwe ndani ya kipindi kifupi, ili Arusha amani na utulivu irejee na kuwaomba wakazi wa Arusha kusubiri hatma ya rufaa hiyo ambayo wanatumaini itatenda haki
ya kurudisha ubunge wa Lema au kuamua kurudi katika uchaguzi.
Alisema kuwa ni vema wakazi wa Arusha na nchi nzima wasigeuze kosa la mtu mmoja, kuwa kosa la mahakama nzima, kuna Majaji wengine wenye busara zao, watatenda haki.
Alisema iwapo watawala wamefikiri kumwangusha Lema katika Ubunge ni kukomoa chama, wanajidanganya kwa sababu chama kina watu makini wengi zaidi ya Lema.
Mbowe alisema kukubali kwenda katika uchaguzi ni kukubali kuwa Lema alipata ubunge kwa kutoa kauli za kudhalilisha, kama walivyotunga huo uwongo wa mchana kweupe, ambao wameshindwa kuthibitisha wahusika wakuu Edward Lowassa na Dk.Batilda Buriani, wanaodaiwa kutajwa.
Alisema pia wana imani rufaa ina nafasi kubwa ya kutenda haki kwa sababu inasikilizwa na Majaji watatu, ila kwa sababu ya upinzani wana nafasi ya kusikiliza Majaji hata watano, hivyo haki itatendeka.
Aidha aliilaumu serikali kuingilia mihilimi mingine kwa kutumia fedha zao na madaraka waliyonayo, hivyo wao kama Chama ndio sababu wanapigania kuandika katiba mpya yenye kuleta usawa na kuacha huru mihilimi mitatu ya Bunge, Serikali na Mahakama kufanya kazi zao bila kushurutishwa na mhimili mwingine.
Mbowe alisema uchaguzi Arumeru umeingiza gharama kubwa Taifa zaidi ya shilingi bilioni tatu zimetumika kwa sababu ya mapenzi ya Mungu, ila siyo kwa makusudi ya Arusha mjini yanayofanywa na watu wachache kwa matakwa yao binafsi.
“Hawa watu wa CCM wanataka uchaguzi ili waendelee kulipana posho, hii ni dhambi kubwa, sababu tuna mahitaji mengi, japo hatuogopi uchaguzi, maana tuna hakika tutashinda asilimia mia moja, ila sisi chama makini tunapinga matumizi mabaya ya rasilimali za umma ndio sababu tunakata rufaa,” alisema.
Alisema hukumu ya Lema imetolewa kwa uhuni kwa kukaa wahuni wachache kwa maslahi yao binafsi na kukiuka taratibu na maadili ya sheria.
Mbowe alisema chama kimeamua kumpa Lema kazi ya kujenga chama katika mikoa ambayo haina uwakilishi, kama Mtwara, Lindi, Songea na Monduli, ili wapate ukombozi wa kweli.
Alisema Arusha kwa sasa imeiva na haihitaji tena kupikwa, bali kuna viraka vichache vimebaki vinahitajika kukombolewa, ambavyo Lema atafanya kazi hiyo wakati anasubiri hatma yake ya rufaa.
Pia alisema iwapo Chadema kitashika dola mwaka 2015 watawala wote wanaotumia fedha za umma kwa maslahi binafsi watashitakiwa mahakamani na kupewa adhabu stahiki kama ilivyo kwa nchi zingine.
Kwa upande wake Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, alipozungumza na wananchi wake waliokuwa wakishangilia kila wakati, alianza kwa kuweka CD iliyorekodiwa wimbo wa Ehe…Mungu kwanini umeniruhusu haya yatokee na kusema maneno yake machache ya kuwatia ujasiri wananchi wasikate tamaa.
Alisema kuwa wananchi wasiogope wakati huo mgumu wa mpito, ila wanapaswa kufunga pamoja naye kwa muda wa siku saba na baada ya mfungo huo wakatoe sadaka kwa yatima na wajane, ili Mungu akasimame kwa wote waliohusika kupanga hukumu hiyo hata ikiwezekana kuchukua maisha yao.
Lema alisema kuwa wakati huo wa mpito atakuwa Mbunge asiyekwenda ofisi za serikali, ila anakaribisha maoni ya wananchi nyumbani kwake na atayafanyia kazi.
Alisema amevuliwa ubunge kihuni na alifahamu hilo kabla ya siku tatu, sababu wahuni wachache walikaa na kujadili jinsi ya kumvua ubunge, ila analia na Mungu ashughulike nao.
Aidha alisema alipoingia chumba cha mahakama, alimwangalia Jaji usoni, kabla ya kutoa hukumu, aliona kabisa anakwenda kutenda dhambi, kwani uso wake ulionyesha na aliendesha kesi hiyo kwa miezi mitatu kwa Kiswahili, lakini siku ya hukumu alisoma Kiingereza na Kiswahili alitumia dakika moja tu.
“Mimi Lema nitaendelea na harakati zangu miguu kwa miguu nchi nzima hata ikibidi kupanda toyo, bito ambayo nimezoea, ili mradi kukomboa taifa hili kwa ajili ya mwaka 2015,” alisema.
Alisema ubunge kwake siyo dili, bali ni utumishi na siyo kujisikia kama mfalme na hivyo ataendelea kushirikiana na wananchi kama kawaida.
Lema alisema makosa aliyohukumiwa nayo yanamruhusu kugombea Ubunge wake, ila kwa sababu ubunge kwake siyo dili, anaweza kumwachia hata Dk. Slaa agombanie Arusha Mjini kuwa mbunge na yeye akaendelea kujenga chama nchi nzima.
Alisema wana kila namna ya kuamua kukata rufaa kwa sababu kuna wabunge wa chama hicho wamefunguliwa kesi kama yake, hivyo wanaweza kufanyiwa kama uhuni huo, hivyo lazima wakatae.
SOURCE: NIPASHE JUMAPILI

No comments: