Tuesday, April 3, 2012

Kagenzi: Sitasahau uchaguzi Arumeru

                                       
  Tuesday, 03 April 2012 21:29
MSIMAMIZI wa uchaguzi wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Trasias Kagenzi,  amesema kamwe hawezi kusahau uchaguzi mdogo kutokana mvutano mkubwa uliokuwapo baina ya wafuasi wa CCM na Chadema.

Pia, Kagenzi ndiye alikuwa msimamizi wa uchaguzi mdogo wa Jimbo la Tarime, ambako Chadema iliibuka na ushinda, lakini alisema uchaguzi wa Arumeru ulikuwa mgumu zaidi ya Tarime.

“Niliyoyaona uchaguzi huu, kamwe sitayasahau maana ninaweza kupata PhD (Shahada ya Uzamivu) kupitia uzoefu niliopata kwenye uchaguzi huu,” alisema Kagenzi.

Alisema kabla ya jana alfajiri kutangaza matokeo, alikuwa akiomba Mungu, uchaguzi huo umalizike kwa amani na utulivu na aweze kutenda haki kwa yoyote ambaye atashinda.

“Nilimuomba Mungu aniwezeshe kutenda haki na nilichokifanya ni kutenda haki, kwani mimi siwezi kumpendelea mtu au chama chochote au kuhujumu mtu au chama chochote cha siasa,” alisema Kagenzi.

Msimamizi huyo ambaye mara kadhaa kabla ya kutangaza matokeo alikuwa akitoka nje na kufanya shughuli nyingine, huku akiwaacha maofisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) wakijumlisha matokeo kwa kompyuta.
Alisema anaamini haki imetendeka kwa upande wake na hategemei kuwapo malalamiko.

CCM waipongeza Chadema
Viongozi mbalimbali wa CCM wamekipongeza  Chadema kwa ushindi walioupata katika uchaguzi wa Arumeru na madiwani katika kata za Kiwira, Kirumba Lizaboni.


Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM, Hussein Bashe, ameeleza  katika taarifa yake mtandaoni kuwa anawapongeza Chadema kwa ushindi wa Arumeru Mashariki, Kiwira, Kirumba, Lizaboni na pia Cuf.

"Nimeamua kufanya hivi kwa misingi ya demokrasia ni wapongeze mmepewa heshima hiyo watumikieni,” alisema Bashe.
Alisema kwa uchaguzi huo litakuwa funzo kwa viongozi wa CCM watatumia busara, kwani matokeo hayo yanaoinyesha ishara kuwa Kaskazini inaanza kupotea mikononi mwao, Nyanda za Juu Kusini  nayo inaanza kupotea na Kanda ya Ziwa inaanza kupotea hiyo ni filimbi kwa CCM.

“Hii ni alarm (ishara) kwa chama changu, umewadia wakati kwa ujumbe huu viongozi wakuu warudi katika Round Table (meza ya mazungumzo) kujadili upya na kutazama kama makundi yetu yatakisaidia chama,” alisema Bashe.

Alisema matokeo hayo Kirumba alikuwapo Samwel Sitta, ,Mbeya alikuwapo Anne Kilango, Arumeru Benjamen Mkapa, Willson Mkama, Edward Lowassa, Nape Nnauye, Lizaboni Dk Emmanuel Nchimbi na maeneo hayo yote CCM imeshindwa.

"Umewadia wakati wa kujitafakari na kujiangalia kwa kina na si kuja na majibu kama yale tuliokuja nayo baada ya uchaguzi mkuu 2010, tunatakiwa kuja na majawabu,”alisema.

Nape
Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alipongeza Chadema na kuwataka wafanye kazi kutimiza waliyowaahidi wapigakura.

"Hongereni watani (Chadema) kwa ushindi Arumeru Mashariki. Ninawapongeza mmeshinda! Ndio kauli ya wana Arumeru Mashariki nasi tunaiheshimu,” alisema.

Chiligati
Naibu Katibu Mkuu CCM Bara, John Chiligati, naye kupitia mtandao alikipongeza Chadema akieleza demokrasia imechukua mkondo wake.

Pia, amekipongeza chama chake kwa kuonyesha ukomavu wa kisiasa kwa kukubali matokeo na kulinda amani chini ya demokrasia changa."Tujipange tuna nafasi ya kurudisha imani ya chama chetu kwa Watanzania,” alisema Chiligati.

No comments: