Na Elisante John
Singida
MAHAKAMA kuu kanda ya Dodoma imetupilia mbali kesi iliyofunguliwa na wanachama wawili wa CCM, kupinga ushindi uliompa ubunge wa Jimbo la Singida,Tundu Lissu (CHADEMA).
Akisoma hukumu hiyo, iliyochukua saa nne, Jaji Moses Mzuna wa Moshi, mkoani Kilimanjaro, alisema wadai wameshindwa kuthibitisha hoja 11 walizomtuhumu Lissu, msimamizi wa uchaguzi na mwanasheria wa Serikali.
Alisema, baada ya mashahidi 24 wa upande wa wadai kutoa ushahidi wao na wanne wa wadaiwa, ameona uchaguzi huo ulikuwa huru, haki na ulifuata taratibu zote, hivyo hauhitaji kutenguliwa.
Baada ya hukumu na Jaji kutoka mahakamani ,Lissu alishindwa kujizuia na alianza kulia huku akitoa machozi ya furah na kuwapa wakati mgumu,jamaa na wafuasi wa CHADEMA, kumbembeleza.
Baadhi ya wabunge wa CHADEMA waliokuwepo mahakamani kusikiliza hukumu hiyo ni Israel Natse-Karatu, Paulina Gekul na Rose Kamili wa viti maalumu, mkoa wa Manyara.
Wengine ni Christina Mughwai na Christowaja Mtinda, wote viti maalumu, mkoa Singida.
Kesi hiyo ilisikilizwa mfululizo kuanzia Machi 12, 2012, walalamikaji ni Shabani Selema Itambu na Pascal Masele Hallu, wakazi wa kijiji cha Mkiungu, Singida vijijini.
Wadai walitetewa na wakili Godfrey Wasonga, wa kampuni ya Wasonga $ Associates Advocates ya Dodoma, wakati Lissu alisimamia mwenyewe, akishirikiana na wanasheria watatu wa serikali, Vicent Tangoh, Juma Ramadhani na Abdallah Chavula.
“Matakwa ya wananchi yaweza kuheshimiwa….kupepeta tu mdomo, bila ya kuwa na ushahidi wa kuthibitisha, ukitengua matokeo hivi hivi tu, wengi utawaharibia, siyo tu uchaguzi, bali hata maisha yao ya baadaye,’alisema Jaji Mzuna.
Baada ya kutoka nje ya mahakama, Lissu aliishukuru mahakama na kwa maamuzi sahihi hadi kushinda kesi hiyo,huku akisema haki ya mtu haipotei.
Aliondoka viwanja vya mahakama akisindikizwa na magari ya polisi, wakiongozwa na OCD wilaya, msululu wa magari ya wafuasi wa CHADEMA, waliojawa na furaha kuu tele, waki wilaya mpya ya Ikungi, kwa mkutano hadhara.
Naye mmoja wa wadai wa kesi hiyo, Shabani Itambu, alisema kwa kuwa kesi hiyo ni ya chama chake (CCM), atakutana na viongozi wake na wakili, wajue cha kufanya.
No comments:
Post a Comment