Thursday, April 12, 2012

Msama Promotions kutathminimaeneo ya kutoa msaada Mtwara

Alex Msama kulia, Mkuu wa wilaya ya Dodoma Betty Mkwasa, Naibu Spika wa bunge Job Ndugai na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk Rehema Nchimbi wakiwa kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma katika tamasha la pasaka lililofanyika jumatatu iliyopita.
 
 
 
Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya Msama Promotions, waandaaji wa tamasha la Pasaka, inatarajia kuanza kutekeleza ahadi yake ya kuwasaidia wanawake wajane na watu wasiojiweza fedha za mitaji ya biashara.

Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama, alisema kwa njia ya simu jana kutoka Dodoma kuwa Kamati ya Maandalizi ya Pasaka inatarajia kwenda Mtwara Jumatatu kufanya tathmini ya maeneo ya kutoa msaada.

"Kamati inatarajia kwenda Mtwara Jumatatu kufanya tathmini ya maeneo gani ya kusaidia wasiojiweza... safari hii walengwa hasa ni watu wa vijijini.

"Kama ilivyo ada, kamati yetu haitoa msaada kwa kubagua itikadi za kidini, awe Mkirsto au Muislamu, wote tunawapa msaada na ndiyo maana hata Serikali imekuwa mstari wa mbele kutuunga mkono.

"Tunasaidia wasiojiweza wote wakiwamo wanawake wajane, watoto yatima na walemavu bila kujali udini... watu wa imani zote za dini tunawatendea haki kwa vile hata kwenye matamasha ya Pasaka, wanaohudhuria ni watu wa imani zote za dini," alisema Msama.

Alisema wamekusudia kutimiza ahadi waliyoitoa wakati wa maandalizi ya tamasha la Pasaka lililofanyika Aprili 8 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na lile la Jumatatu ya Pasaka, Aprili 9 mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Msama juzi alitoa taarifa ya kuwashukuru wadau mbalimbali waliofanikisha tamasha hilo kwa hali na mali.

Katika tamasha la Uwanja wa Taifa, mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ambaye pamoja na marafiki zake alioongozana nao jukwaani walichangia sh. milioni 10, Rais Kikwete aliahidi kuchangia sh. milioni 10 na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda sh. milioni 5, hivyo kufanya jumla kuwa sh. milioni 25, zitakakazotumika kusaidia wasiojiweza.

Pia katika tamasha la Dodoma, Naibu Spika, Job Ndugai alichangia sh. milioni 2 kwenye mfuko huo.

Mwaka jana, wanawake wajane waliokabidhiwa fedha za mitaji walitoka mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro ambapo sh. milioni 4 zilitumika. Fedha nyingine zilitumika kusaidia kusomesha watoto yatima.

No comments: