Thursday, June 28, 2012

Jumuiya Ya Ulaya (EU) Yaimwagia Mabilioni Taasisi Ya TRIT

Balozi wa Jumuiya ya Ulaya Nchini (EU), Filiberto Ceriani Sebregondia akiizindua rasmi tovuti ya Taasisi ya Utafiti wa Chai Tanzania (TRIT)


Hapa akimshuhudia Naibu Afisa Muidhinishaji Mkuu wa Fedha zinazotolewa na Jumuiya ya Ulaya, Samwel Marwa akisaini hati hiyo ya makubaliano ya msaada huo kwa niaba ya serikali ya Tanzania


Balozi wa EU, Filiberto Ceriani akianguka saini yake kukamilisha mkataba wa makubaliano ya msaada huo.


Balozi wa EU akiangali moja ya mashamba ya chai ya mfano ya taasisi hiyo. Chanzo: www.frankleonard.blogspot.com



JUMUIYA ya Ulaya (EU) imeahidi kuendelea kusaidia uboreshaji wa miundombinu na matumizi ya teknolojia zitakazowawezesha wakulima wadogo wa chai kuongeza uzalishaji na kumudu ushindani katika masoko.

EU kwa kupitia awamu ya pili ya pragramu yake ya Kusaidia Biashara na Kilimo (TASP II), juzi ilitoa msaada wa zaidi ya Sh Bilioni tatu kwa Taasisi ya Utafiti wa Chai Tanzania (TRIT).

Fedha hizo zitakazotumika kwa miaka minne (2012-2015) zitaiwezesha TRIT kusaidia maendeleo ya wazalishaji wadogo na wakubwa wa zao hilo kwa kufanya tafiti zitakazoongeza ubora na uhamishaji na matumizi ya teknolojia.

Hati ya makubaliano ya msaada huo ilisainiwa katika ofisi Kuu za TRIT wilayani hapa na Balozi wa EU nchini, Filiberto Cerian Sebregondi kwa upande wa jumuiya hiyo na Naibu Afisa Muidhinishaji Mkuu wa fedha zinazotolewa na jumuiya hiyo, Samwel Marwa kwa upande wa serikali ya Tanzania.

Katika hafla hiyo Balozi huyo alisema EU inafahamu umuhimu na mahitaji ya chai kama zao la biashara lenye soko kubwa nje ya Tanzania.

“Likiwa linalimwa na wakulima wadogo zaidi ya 30,000, ni zao la tano linalouzwa nje ya nchi huku likiingizia nchi ya Tanzania na watu wake zaidi ya dola za kimarekeni bilioni 30 kila mwaka,” alisema balozi huyo.

Alisema pamoja na umuhimu wake huo, EU inafahamu changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo hususani faida ndogo wanayopata wakulima wadogo kwa kuzingatia mchakato wa shughuli za kilimo nchini na kushuka kwa uzalishaji wa zao hilo kunakotokana na urasimu wa kuyafikia masoko.

“Hii ndio sababu Jumuiya ya Ulaya katika kuitekeleza ahadi yake ya kuisaidia Tanzania kuhamasisha kilimo endelevu, imekuwa ikielekeza nguvu zake katika kusaidia kuboresha hali za wakulima wadogo,” alisema.

Akishukuru kwa msaada huo wa fedha, Mkurugenzi Mtendaji wa TRIT anayemaliza muda wake, Profesa Bruno Ndunguru alisema unatarajiwa kutoa matokeo yatakayopimika kwa kuwajengea uwezo wakulima wadogo ili wazalishe kwa ubora wa viwango vya juu, kuiboresha sekta na kuiongezea TRIT uwezo wa kuzishughulikia changamoto zinazowakabili wakulima kwa haraka.

Naye Naibu Afisa Muidhinishaji Mkuu wa Fedha zinazotolewa na EU alisema matarajio ya serikali ni kuona tija inaongezeka katika kilimo cha chai na hivyo kukuza uchumi wa nchi.

Marwa alisema fedha hizo zitasaidia kuboresha biashara na kilimo katika sekta hiyo inayoendelea kutoa ajira kubwa kwa watanzania wengi. Chanzo: www.frankleonard.blogspot.com

No comments: