Thursday, June 28, 2012

Madaktari 72 Watimuliwa Kazi -MBEYA

 Mwenyekiti wa Bodi Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Norman Sigara Aikzungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu kufukuzwa kazi kwa madaktari hao.

Mkurugenzi wa wa hospitali ya rufaa Mbeya Dr  E. Sankey akimsikiliza kwa makini kaimu mkuu wa mkoa Mbeya.



                                     Waandishi wa habari

BODI ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya, imewasimamisha kazi madaktari 72 kwa kosa la kutoingia kazini kwa siku tano jambo ambalo ni kinyume cha makubaliano ya mkataba.

Imeelezwa kuwa madaktari hao ambao 54 ni wale wa mafunzo ambao waliingia mkataba wa miaka miwili na hospitali ya Rufaa na madaktari 18 ni wale walioajiriwa na Wizara ya afya.Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Bodi Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Norman Sigara, alisema kitendo cha madaktari kutoripoti kazini kwa siku tano ni ukiukwaji wa kanuni za utumisha wa umma toleo
la 2009 kifungu namba F.16-F17 na F. 27.

"Hivyo kupitia kanuni hiyo madaktari hao wamesimamishwa kazi na kurudishwa kwa mwajiri wao ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa hatua zaidi za kinidhamu,"alisema Sigara.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo wa Bodi, imeelezwa kuwa siku ya tarehe 23/6/2012 wafanyakazi 15 waliokuwa zamu(Intern Doctors 12 na Registrars3) hawakufika kazini na tarehe 24/6/2012 wafanyakazi
19(Intern doctors 15 na Registrars 4) hawakufika kazini.

Alisema, kuanzia tarehe 25/6/2012 hadi leo imethibitika kuwa Interns
doctor 54 na Registrars 18 hawakufika kazini hadi leo tarehe 28/6/2012
ambapo tarehe 25/6/2012 bodi ya hospitali ilifanya kikao cha dharura
kujadili hali ya utendaji kazi na utoaji huduma hospitalini na kutoa
uamuzi.
Sigara, aliyataja maamuzi hayo kuwa ni Mwenyekiti wa Bodi akutane na madaktari ambao hawakufika kazini ili awasikilize sababu za kutofika na kujadili namna ya kumaliza matatizo hayo jambo ambalo madaktari hao waligoma. 
Alisema, baada ya madaktari hao kukaidi ombi hilo, Bodi ya hospitali ili waandikia barua za kujieleza kwanini wasichukuliwe hatua za kinidhamu kwa kuvunja mkataba walioingia na hospitali na pia kukiuka kanuni za kudumu za utumishi wa umma nalo walilikaidi

"Iwapo madaktari ambao hawakuripoti au kueleza sababu za kuridhisha ifikapo tarehe 28/6/2012. Kwa kuzingatia kanuni za utumishi wa Umma, madaktari hao watasimamishwa kazi na kurudishwa kwa mwajiri wao ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,"alisema.

Aidha, alisema kuwa kwa ujumala madaktari hao waligomea barua zote mbili yaani ya kuitwa kwenye kikao pamoja na ile ya kuwataka kujieleza hivyo Bodi imechukua hatua za kisheria za kuwafukuza kazi.
Hata hivyo Mwenyekiti huyo wa bodi, alisema kuwa tayari hospitali ya Rufaa kwa ushirikiano wa Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, madaktari watano wamepatikana ili kusaidia huduma kwa hospitali hiyo.

Tamko FupIi La Jumuiya Ya Madaktari Tanzania

    KAMATI YA JUMUIYA YA MADAKTARI TANZANIA

YAH: TAMKO FUPI LA JUMUIYA YA MADAKTARI KWA WAANDISHI WA HABARI LEO TAREHE 28.06.2012

Madaktari wote hatuna imani na tume iliyoundwa na Jeshi la polisi nchini yenye lengo la kuendesha uchunguzi juu ya kutekwa, kunyanyaswa na kupigwa vibaya kwa Dr. Ulimboka Stephen na tunataka chombo huru kiundwe ili kupata ukweli wa tukio hilo.

Pia tunakemea na kuonya juu ya vitisho vyote vinavyotolewa na baadhi ya watawala katika taasisi mbalimbali dhidi ya madaktari mfano Hospitali ya Rufaa ya Dodoma, Bugando, Mbeya na kwingineko ambapo wametishwa na kufukuzwa kwa kutumia mabavu.

Madaktari tunazidi kusisitiza kuwa hakuna njia nyingine yeyote ya kusuluhisha mgogoro huu isipokuwa ni kwa kutekeleza madai na hoja za msingi za madaktari kwa njia ya mazungumzo ya dhati.

Madaktari tumechoka kuona huduma za afya nchini zikizidi kudorora mwaka hadi mwaka, Tumechoka kuona wagonjwa wakilala chini na watoto wakilala wanne katika kitanda kimoja Tumechoka kuona msongamano mkubwa kwa wagonjwa katika hospitali zetu huku kukiwa hakuna mpango wowote wa uboreshaji.

Tumechoka kuona wagonjwa wakikosa dawa, vipimo sahihi na watumishi wa afya wakifanya kazi katika mazingira magumu yanayoviza ubora wa huduma na misingi ya taaluma.

Kwa hiyo, kwa moyo wetu leo tumejitolea kutetea uboreshaji wa sekta ya afya licha ya vitisho tunavyoendelea kuvipata.

Rai kwa Madaktari; Madaktari wote kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu, tunashukuru madaktari wote kwa ushirikiano na kuendelea na mshikamano.

              Imetolewa na Kamati ya Jumuiya ya Madaktari.

No comments: