Serikali imewataka wananchi kujitokeza kwa wito katika zoezi la sensa ya watu na makazi itakayoanza tarehe 26 Agosti mwaka huu nchini kote na kuendelea katika kipindi cha siku saba(7) tangu siku ya zoezi hilo litakapoanza.
Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati anafungua mafunzo ya siku 10 ya wakufunzi wa sensa ya watu na makazi mjini Dodoma.
Alisema kuwa ili kufanikisha zoezi la sensa kwa mwaka huu ni vema wananchi wakatunza kumbukumbu za taarifa za maswali yatakayoulizwa kwa watu wote watakaolala katika kaya zao usiku wa kuamkia tarehe 26 Agosti 2012.
Waziri Mkuu alisema kuwa kumbukumbu hizo ndio zitakazowasidia kujibu maswali watakayoulizwa na makarani wa sensa katika siku watakapofika katika kaya zao kwenye kipindi cha siku saba za kuhesabu watu.
Alisema kuwa ili kufanikisha zoezi hilo ni vema viongozi wa vyama vyote vya siasa , wabunge , wawakilishi , viongozi wa madhehebu ya dini , watendaji wa kata, masheha, wenyeviti wa vijiji na watendaji wengine wakashirikiana katika kuelimisha na kuhamasisha umma kuhusu umuhimu wa kushirikiana na makarani , wasimamizi na watumishi wengine watakaofanya zoezi la sensa ili kufanikisha kazi hiyo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
Aidha Waziri Mkuu alisema kuwa pamoja na kufanyika zoezi la sensa hakusudii kusimamisha shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii kwani makarani wa sensa watapita kwenye kaya za wananchi katika muda wowote kuanzia usiku wa kuamkia tarehe 26 Agosti 2012 na kuendelea kwa siku saba.
Mheshimiwa Pinda alisema kuwa jambo la msingi ni kuhakikisha kuwa kila mtu atakayekuwa nchini usiku wa kuamkia tarehe 26 Agosti mwaka huu anahesabiwa mara moja tu.
"Naomba wa wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa makarani wa sense kwa kutoa taarifa sahihi za kaya zao ili kupata takwimu sahihi kwa mipango ya maendeleo” alisisitiza Waziri Mkuu.
Aliwahakikisha kuwa wananchi wasiogepe kutoa taarifa zote watakazoulizwa kwani kwa mujibu wa sheria ya sensa sura 351 taarifa zitakazokusanywa zitatumiwa kwa siri na zitatumika kwa shughuli za kitakwimu tu.
Aidha aliwataka wakufunzi wa sense ngazi ya kitaifa kujifunza kwa bidii kuwa mafanikio ya zoezi hilo yanategemea kwa kiwango kikubwa uelewa mpana na ushirikiano mkubwa wa viongozi na wakufunzi na makarani wa sense katika ngazi zote .
Sensa ya watu makazi hapa nchini ilifanyika mwaka 1910 na iliyofuata ilifanyika mwaka 1948 na 1957 kwa upande wa Tanzania bara na 1958 kwa Tanzania Visiwani.
Tangu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964 sensa ya mwaka huu itakuwa ya tano ambapo zilifanyika mwaka 1967,1978,1988 na mwaka 2002.
No comments:
Post a Comment