Sunday, June 24, 2012

UFAHAMU WA KAZI ZA BODI YA KANDARASI ZANZIBAR WAZIDI KUFAHAMIKA

Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar

Imeelezwa kuwa ufahamu wa kazi za Bodi ya Usajili wa Wakandarasi Zanzibar umeongezeka kwa kiasi kikubwa na kwamba mwitikio wa usajili umekuwa ukiongezeka siku hadi siku.

Hayo yameelezwa leo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Mwinyihaji wakati alipokuwa akimuwakilisha Waziri wa Ardhi, Makazi Maji na Nishati Ramadhan Shaaban katika tafrija ya kuhitimisha Bodi ya usajili wa Wakandarasi iliyofanyika ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar  Beach Resort Mazizini.

Dk. Mwinyihaji amesema matokeo ya ufahamu huo yanatokana na kazi kubwa iliyofanywa na bodi hiyo ambayo imemalizika muda wake na kwamba wajumbe wake bado wanahitajika kutoa ushauri kwa Bodi mpya ambayo itaundwa tena upya.

“Tunaomba muwe tayari kuwapatia uzoefu wenu vijana na wajumbe wote ambao watateuliwa katika bodi mpya, bado nyinyi ni watu muhimu katika nchi hii” Alisema Dk. Mwinyihaji.

Akielezea malengo makuu ya Bodi hiyo Dk. Mwinyihaji alisema ni pamoja na kusimamia Sekta ya ujenzi hasa katika ujenzi wenyewe,majirani na hata wapita njia.

Malengo mengine ni pamoja na kuhakikisha Wakandarasi ambao wanasajiliwa wanapangwa kwenye madaraja kwa mujibu wa uwezo wao samba na kutoa elimu kwa wakandarasi ili kukuza uwezo wao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi hiyo Ramadhani Kesi aliipongeza Serikali kwa kuwaamini kusimamia majukumu ya Bodi hiyo ambayo ilikuwa inakabiliwa na changamoto nyingi.

Miongoni mwa changamoto ni pamoja na Bodi kuanzishwa kwa muda wote wa miaka mitatu bila kuwekewa fungu la ruzuku na kuifanya Bodi hiyo kujiendesha yenyewe kwa kusua sua.

Changamoto nyingine ni pamoja na kukosa Ofisi na watendaji wa kudumu jambo ambalo limekuwa likiwakosesha kufanya kazi kwa ufanisi.

Bodi hiyo iliyohitimisha kazi zake imeshasajili Wakandarasi katika fani za majengo,majenzi, umeme na fani maalumu ambapo Wakandarasi 19 kutoka Zanzíbar,10 kutoka Tanzania Bara na Saba kutoka nchi za kigeni wamesajiliwa.

Bodi hiyo ambayo iliundwa June,2009 inahitimisha kazi zake June 2012 ambapo Waziri wa Ardhi, Makazi Maji na Nishati Ramadhan Shaaban anajukumu la kuunda Bodi mpya ili kuendeleza majukumu yaliyoachwa na Bodi hiyo.

No comments: