Thursday, July 12, 2012

AFARIKI DUNIA MARA BAADA YA KUPIGWA NA FIMBO

MKAZI  mmoja wa kijiji cha Piyaya kilichopo wilayani Ngorongoro aliyefahamika kwa jina la Alaisieleke Korio (48) amefariki dunia baada ya kupigwa fimbo kichwani na mwenzake  .

Kamanda wa polisi mkoani hapa, ACP Liberatus Sabas alisema kuwa marehemu huyo alipigwa fimbo kichwani na mtu aliyefahamika kwa jina la Zablon Shilalo(32) mkazi wa Ingarasero wilayani Ngorongoro.


Alisema kuwa, tukio hilo limetokea july 8 mwaka huu majira ya saa 7;00 usiku katika kijiji cha Piyaya kilichopo wilayani Ngorongoro mkaoani Arusha.


Sabas alisema kuwa ,chanzo cha mauaji hayo ni ugomvi uliotokana na madai ya fedha kati ya marehemu mtuhumiwa ambapo marehemu alikuwa anakumbusha deni lake kwa mtuhumiwa huyo , hali iliyozusha mabishano kati yao wawili.


Alisema kuwa,kutokana na mabishano hayo ndipo mtuhumiwa alichukua fimbo na kumpiga marehemu aliyepata jeraha kichwani ambalo lilimsababishia kifo chake.


 Aidha Kamanda Sabas aliongeza kuwa, kufuatia tukio hilo jeshi la polisi mkoani hapa linaendelea na uchunguzi zaidi wa kumhoji mtuhumiwa huyo kutokana na tukio hilo.

Alisema kuwa,mara baada ya uchunguzi huo ,mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani kujibu shitaka hilo la mauaji hayo na mwili wa marehemu umeshazikwa baada ya kufanyiwa uchunguzi na daktari wa hospitali ya Wasso.

Wakati huo  huo, mtoto wa siku moja wa jinsi ya kiume amekutwa akiwa ametupwa katika eneo la Mianzini mjini hapa .

Aidha mtoto huo alikutwa akiwa amefunikwa kwenye mfuko wa rambo ambapo kugundulika kwa mtoto huyo ni baada ya mbwa aliyekuwa akila jalalani kuona mfuko huo na kuanza kuufungua akidhani ni chakula.


Hata hivyo kitendo cha mbwa huyo kufungua mfuko huo ndipo mtoto huyo alipoonekana akiwa tayari ameshakufa ,na wasamaria wema walipiga simu polisi na kuja kuuchumua mwili wa mtoto huyo ambao umehifdhiwa katika hospitali ya mkoa ya Mount Meru.


Kamanda wa polisi mkoani hapa, ACP Liberatus Sabas amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na uchunguzi zaidi unaendelea wa kumsaka aliyehusika na unyama huo.

No comments: