Saturday, August 11, 2012

Hotuba Ya Waziri Wa Maliasili Na Utalii Balozi Khamis Kagasheki Bungeni Ya Makadirio, Mapato Na Matumizi Ya Mwaka 2012/2013

HOTUBA YA WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII MHESHIMIWA BALOZI KHAMIS S. KAGASHEKI (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2012/2013

I. UTANGULIZI

1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba kutokana na Taarifa iliyowasilishwa leo ndani ya Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliyochambua Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Bunge lako sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Utekelezaji ya Mwaka 2011/12 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Taasisi zake kwa mwaka 2012/13. Napenda nianze kwa kuishukuru kwa dhati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira chini ya Mwenyekiti wake Mhe. James Daudi Lembeli (Mb.) kwa kuchambua Taarifa ya Utekelezaji kwa mwaka 2011/12 na Mpango wa Bajeti wa Wizara yangu kwa mwaka 2012/13. Ushauri wao umezingatiwa katika Bajeti hii.

2. Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniteua na kunipa fursa ya kuiongoza Wizara hii yenye dhamana ya kusimamia Rasilimali za Maliasili na Malikale na kuendeleza Utalii. Namhakikishia kuwa nitajitahidi kwa kadri ya uwezo wangu kwa kushirikiana na wadau wote kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi hii zinalindwa na kuwanufaisha watanzania wote.

3. Mheshimiwa Spika, kwa majonzi makubwa, naungana na Wabunge wenzangu kutoa pole kwa Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wananchi wote kwa msiba uliotupata kutokana na kuzama kwa meli ya MV Skagit tarehe 18 Julai,
2012. Nawatakia ahueni wale wote walionusurika katika ajali hiyo na kwa wale waliofariki namuomba Mwenyezi Mungu aziweke roho zao mahali pema peponi, Amin.

4. Mheshimiwa Spika, hotuba yangu inajikita katika maeneo makuu manne kama ifuatavyo:- Kwanza nitaelezea kuhusu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2010-2015; Pili ni utekelezaji wa ahadi nilizozitoa katika Bunge la Bajeti la mwaka 2011/12 pamoja na maagizo mbalimbali yaliyotolewa na Bunge na Viongozi Wakuu wa Serikali; Eneo la tatu ni changamoto zinazoikabili Wizara yangu katika kutekeleza majukumu yake pamoja na Mikakati iliyopo; na Sehemu ya nne ni Mpango wa Utekelezaji na Malengo ya Wizara kwa mwaka 2012/13.
II. UTEKELEZAJI WA ILANI YA UCHAGUZI YA CCM YA MWAKA 2010-2015

5. Mheshimiwa Spika, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2010-2015 imeelekeza Wizara ya Maliasili na Utalii kutekeleza yafuatayo:- kuziwezesha jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi kunufaika na rasilimali za wanyamapori na misitu; kuboresha mazingira ya makazi ya watumishi wanaoishi kwenye mazingira magumu; kuweka utaratibu shirikishi wa upandaji na uvunaji miti na udhibiti wa moto; kuboresha miundombinu ndani ya Mapori ya Akiba, Hifadhi za Wanyamapori na Misitu; na kuendeleza jitihada za kuhifadhi mazingira katika mbuga za wanyama, misitu, fukwe za bahari na maziwa.
Aidha, Wizara imetakiwa kuongeza msukumo katika maeneo yafuatayo:- kuendeleza ufugaji wa nyuki kwa ajili ya kuzalisha asali na nta kibiashara; kukuza mwamko na kuendesha kampeni za kuwashawishi watanzania kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vya utalii; na kupanua wigo wa aina za utalii kwa kuendeleza utalii wenye kuhusisha utamaduni, mazingira na makumbusho.

6. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza Ilani, Wizara imeendelea kuhamasisha wananchi kushiriki katika uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za wanyamapori. Aidha, imewezesha kuanzishwa na kuendelezwa kwa maeneo 38 ya Jumuiya ya Hifadhi za Jamii (WMAs) na kufanya matengenezo ya viwanja 12 vya ndege vilivyoko katika Hifadhi. Vilevile, nyumba sita za watumishi kwenye Mapori ya Akiba Ibanda na Rumanyika zimewekewa mfumo wa umeme.

7. Mheshimiwa Spika, kampeni kwa njia ya sinema kuhusu upandaji miti zimefanyika katika vijiji 22 katika wilaya za Bagamoyo, Kibaha, Kilosa na Kisarawe na vijiji 18 vinavyozunguka misitu ya hifadhi Pugu na Kazimzumbwi. Kamati za Wilaya 28 zimewezeshwa kuendesha vikao vya uvunaji na kufanya doria katika misitu ya asili. Vilevile, Wizara imejenga nyumba mbili za kuishi watumishi katika Shamba la Miti Mtibwa na kutengeneza barabara zenye urefu wa jumla ya kilomita 1,120 kwenye mashamba ya miti pamoja na kujenga madaraja 10 katika shamba la miti Sao Hill.

8. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuwezesha ufugaji nyuki ambapo mizinga 602 ilitengenezwa na kutundikwa katika vituo vinne vya maonyesho vya Manyoni (174), Handeni (158), Kondoa (200) na Buha (70). Aidha, mizinga 200 imesambazwa katika maeneo ya: Sumbawanga (50), Mpanda (50) na Mbarali (100). Vilevile, wafugaji nyuki 66 katika wilaya ya Kahama wamepatiwa mafunzo kuhusu ubora na usalama wa asali.

9. Mheshimiwa Spika, Wizara ilizindua Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni na kuendelea kuhamasisha jamii kuanzisha vikundi vya utalii wa kiutamaduni. Vikundi hivyo vimeongezeka kutoka 34 mwaka 2010/11 hadi 41 mwaka 2011/12. Vikundi hivyo ni kutoka katika mikoa ya Lindi, Mara, Arusha na Dodoma. Vilevile, Wizara imefanya zoezi la kutambua na kuweka kumbukumbu za Urithi wa kihistoria uliopo majini katika kisiwa cha Mafia. Kazi nyingine za utekelezaji wa Ilani zimefafanuliwa katika aya ya 9 hadi ya 11 katika Kitabu cha Hotuba kilicho mbele yenu.

III. UTEKELEZAJI WA AHADI ZILIZOTOLEWA WAKATI WA BUNGE LA BAJETI MWAKA 2011/12

SEKTA NDOGO YA WANYAMAPORI
(i) Utekelezaji wa Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori
10. Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha 2011/12, Wizara imeendelea kutekeleza Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 kwa kukamilisha kanuni zifuatazo:- Maeneo ya Jumuiya ya Hifadhi za Wanyamapori (WMAs); Vitambulisho vya maafisa Walioidhinishwa; Uthaminishaji wa Nyara; Hati za Ufifirishaji wa Makosa (Compounding); na Amri ya kipindi Kisichokuwa cha Uwindaji. Aidha, rasimu za Kanuni tano ziko katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Kanuni hizo zimeainishwa katika aya ya 12 ya Kitabu cha Hotuba.

(ii) Ulinzi wa Wanyamapori, Maisha ya Watu na Mali Zao
11. Mheshimiwa Spika, doria-siku (patrol man-days) 75,593 zilifanyika ndani na nje ya Mapori ya Akiba ambapo watuhumiwa 1,981 wamekamatwa kwa makosa mbalimbali na kesi 1,280 zimefunguliwa. Aidha, vituo viwili vimejengwa katika Wilaya za Rombo (Ngoyoni) na Siha (Visa – West Kilimanjaro) kwa ajili ya kudhibiti wanyama wakali na waharibifu. Ujenzi wa kituo cha Nangurukuru kilichopo katika Wilaya ya Kilwa unaendelea. Vilevile, Wizara imelipa kifuta jasho na kifuta machozi kwa wananchi walioathirika na wanyamapori wakali na waharibifu. Jumla ya wananchi 1,342 wanaomiliki ekari 2,148 za mazao walilipwa Shilingi 167,672,500 ikiwa ni kifuta jasho. Aidha, jumla ya Shilingi 15,300,000 zililipwa ikiwa ni kifuta machozi kwa wananchi 42 waliojeruhiwa na wanyamapori pamoja na familia za watu wanane waliouawa na wanyama hao. Ufafanuzi zaidi kuhusu ulinzi wa wanyamapori na maisha ya watu umeoneshwa katika aya ya 13 hadi ya 15 katika Kitabu cha Hotuba.

(iii) Ushirikishaji Jamii Katika Uhifadhi wa Wanyamapori
12. Mheshimiwa Spika, mwaka 2011/12, Wizara imehamasisha jamii kuhusu uhifadhi shirikishi wa wanyamapori ambapo maeneo matano ya Jumuiya za Wanyamapori (WMAs) yameanzishwa. Aidha, WMAs 12 katika wilaya 12 zimepata jumla ya Shilingi 200,000,000 kutokana na mapato ya uwindaji wa kitalii. Kazi nyingine zilizofanyika katika kuimarisha uhifadhi wa wanyamapori zimeainishwa kwa kina katika aya ya 16 hadi 17 katika Kitabu cha Hotuba.

(iv) Maduhuli
13. Mheshimiwa Spika, mwaka 2011/12, Idara ya Wanyamapori ilikadiria kukusanya Shilingi 24,168,751,574 kutokana na vyanzo mbalimbali. Hadi Juni, 2012 Shilingi Bilioni kumi na tano, milioni sabini na nne, hamsini na tatu elfu, mia tisa sabini na mbili (15,074,053,972) sawa na asilimia 62 ya makadirio zilikuwa zimekusanywa. Vilevile, Mfuko wa Kuhifadhi Wanyamapori Tanzania ulikadiria kukusanya Shilingi 16,287,141,880. Hadi Juni, 2012 makusanyo yalifikia Shilingi 11,673,240,697 sawa na asilimia 72 ya makadirio. Fedha hizo zimeendelea kutumika kwa shughuli za kulinda wanyamapori, utafiti na mafunzo, kutoa elimu kwa umma na kukarabati miundombinu.

(v) Vyuo vya Taaluma ya Wanyamapori
14. Mheshimiwa Spika, Mwaka 2011/12, Chuo cha Wanyamapori-Mweka kimedahili wakurufunzi 502 wa kozi za muda mrefu. Aidha, Chuo kimesomesha Wakufunzi saba wa Shahada ya Uzamivu, watatu Shahada ya Uzamili na wafanyakazi wanne wa kada za Ukutubi, Uhasibu na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

15. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha miundombinu, Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi imejenga darasa moja, mabweni mawili na kukarabati nyumba tisa za watumishi. Mwaka wa masomo 2011/12, idadi ya udahili iliongezeka kutoka wakurufunzi 236 mwaka 2010/11 hadi 284. Aidha, Kituo cha Mafunzo ya Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii cha Likuyu Sekamaganga kimedahili wakurufunzi 200 ikilinganishwa na wakurufunzi 137 mwaka 2010/11.

(vi) Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI)
16. Mheshimiwa Spika, mwaka 2011/12, TAWIRI imeendelea kufanya tafiti kuhusu wanyamapori, mimea, nyuki na kupe wa nyuki katika sehemu mbalimbali nchini. Matokeo ya tafiti hizo pamoja na maeneo yaliyohusika ni kama ilivyoainishwa katika aya ya 22 hadi aya ya 25 katika Kitabu cha Hotuba.

(vi) Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
17. Mheshimiwa Spika, mwaka 2011/12 Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imekarabati barabara zenye jumla ya kilomita 420 na kununua malori manne. Aidha, Michoro ya jengo la kitega uchumi mjini Arusha imekamilika. Vilevile, Mamlaka imekamilisha ujenzi wa madarasa matatu ya Shule ya Msingi Jema na ukarabati wa majosho matatu katika maeneo ya Meshili, Olpiro na Ndiani na majosho hayo yanatumika. Ujenzi wa mabwawa matatu katika maeneo ya Ngairishi, Kaitangteng na Eltulele unaendelea.

(viii) Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA)
18. Mheshimiwa Spika, Shirika limeimarisha Idara ya Himasheria kwa kujenga vituo 11 vya askari katika hifadhi za Kitulo, Saadani, Mkomazi na Arusha. Aidha, askari 100 wameajiriwa na magari 26 yamenunuliwa kwa ajili ya shughuli za uhifadhi. Katika kuboresha miundombinu, barabara zilifanyiwa matengenezo na nyumba 21 zimejengwa katika hifadhi mbalimbali zilizo chini ya TANAPA. Kazi nyingine zilizotekelezwa na TANAPA zimeainishwa katika aya ya 28 hadi ya 30 katika Kitabu cha Hotuba.

SEKTA NDOGO YA MISITU NA NYUKI

(i) Sera na Kanuni
19. Mheshimiwa Spika, mwaka 2011/12, nakala 2,750 za kijitabu cha Tozo za Misitu zimechapishwa na kusambazwa. Aidha, Wizara imempata mtaalam mwelekezi atakayeratibu zoezi la kupitia Sera ya Ufugaji Nyuki ya mwaka 1998.

(ii)Kuendeleza Ufugaji Nyuki
20. Mheshimiwa Spika, Ili kutekeleza azma ya Serikali ya kuendeleza ufugaji nyuki, jumla ya mizinga 205 na mavazi ya kinga 90 yametengenezwa na kusambazwa kwa vikundi 20 vya ufugaji nyuki katika wilaya ya Kahama na vikundi 10 katika wilaya ya Magu. Kila kikundi kilipata mizinga nane na jozi tatu za mavazi ya kinga. Aidha, kufuatia maonesho ya Nanenane yaliyofanyika hapa Dodoma na kushindanisha wafugaji nyuki, Wizara ilitoa mizinga 100 kwa mshindi wa kwanza na 60 kwa mshindi wa pili.

(iii) Vyuo vya Taaluma ya Misitu na Ufugaji Nyuki
21. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuwezesha vyuo vya misitu na ufugaji nyuki ambapo mwaka 2011/12 jumla ya wakurufunzi 218 walidahiliwa ikilinganishwa na wakurufunzi 205 waliodahiliwa mwaka 2010/11. Wakurufunzi waliodahiliwa ni kwa ajili ya Chuo cha Misitu Olmotonyi – Arusha (150); Chuo cha Nyuki Tabora (38); na Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi (30).

22. Mheshimiwa Spika, mwaka 2011/12, Chuo cha Viwanda vya Misitu (FITI) Moshi kimekamilisha kukadiria gharama za ujenzi wa Maktaba na Maabara ambapo ujenzi utaanza mwaka 2012/13. Aidha, Ujenzi wa Bwalo la Chakula unaendelea katika Chuo cha Ufugaji Nyuki Tabora na lipo katika hatua za mwisho kukamilika.

(iv) Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)
23. Mheshimiwa Spika, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania umeanza kutekeleza majukumu ya kiutendaji yaliyokuwa yanafanywa na Idara ya Misitu na Nyuki. Majukumu yaliyotekelezwa ni pamoja na:- kutoa elimu kwa umma na uhamasishaji; kushirikisha wadau katika kuendeleza misitu; upandaji miti; kuimarisha miundombinu; kusimamia misitu ya hifadhi; na kuendeleza ufugaji nyuki. Aidha, sampuli 60 za asali zilikusanywa katika wilaya 17 kwa lengo la kuhakiki na kudhibiti viwango vya ubora wa mazao ya nyuki. Kati ya sampuli hizo, 40 zimepelekwa katika maabara teule nchini Ujerumani.

24. Mheshimiwa Spika, vituo vinne vya ufugaji nyuki viliwezeshwa kusimamia makundi ya nyuki 1,056 na kuanzisha Manzuki mbili. Kazi nyingine zilizotekelezwa katika maeneo hayo zimeainishwa katika aya ya 37 hadi aya ya 42 ya Kitabu cha Hotuba.

(v) Kuimarisha Ukusanyaji wa Maduhuli
25. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli, Wakala uliwawezesha watumishi 142 wa Halmashauri za Wilaya, Sekretarieti za Mikoa na Wizara kushiriki mafunzo kuhusu taratibu na kanuni za ukusanyaji wa maduhuli.
Hadi Juni, 2012 Shilingi Bilioni hamsini na tisa, milioni mia sita sitini na sita, sabini elfu na mia moja themanini (59,666,070,180) sawa na asilimia 151 ya lengo zimekusanywa. Aidha, Mfuko wa Misitu Tanzania umekusanya shilingi 3,338,377,101 kufikia Juni 2012, ikiwa ni asilimia 111 ya makisio ya shilingi 3,000,000,000. Kazi zilizotekelezwa na Mfuko zimeainishwa katika aya ya 45 na 46 ya Kitabu cha Hotuba.

(vi) Wakala wa Mbegu za Miti Tanzania (TTSA)
26. Mheshimiwa Spika, Wakala wa Mbegu za Miti uliendelea kuzalisha na kuuza mbegu na miche ya miti. Hadi Juni 2012, mbegu za miti zilizouzwa ndani na nje ya nchi ni kilo 9,262 kwa thamani ya Shilingi 90,612,665. Maelezo ya kina kuhusu aina za mbegu, miche ya miti na fedha zilizopatikana yamefafanuliwa katika aya ya 47 ya Kitabu cha Hotuba.

(viii) Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI)
27. Mheshimiwa Spika, mwaka 2011/12, Taasisi imeanzisha tafiti juu ya matumizi ya maji kwa miti ya mikaratusi katika maeneo ya Shinyanga, Korogwe, Lushoto na Kibaha. Aidha, Taasisi imeendelea na utafiti na uzalishaji juu ya bioteknolojia ya aina 16 za kloni za miti ya mikaratusi inayofaa kupandwa katika maeneo mbalimbali nchini. Pia, Taasisi inatafiti juu ya ukuaji wa jamii 81 za mikaratusi aina ya pellita huko Sao Hill kwa lengo la kuwapa wadau wa misitu miti yenye ubora unaotakiwa. Maelezo zaidi kuhusu tafiti zilizofanyika yanapatikana katika aya ya 49 ya Kitabu cha Hotuba.

28. Mheshimiwa Spika, kupitia Mfuko wa Misitu Tanzania, TAFORI imeanzisha mashamba darasa kwa ajili ya miti ya kuni na mkaa katika vijiji vya Lubungo na Gwata vilivyopo katika Wilaya ya Morogoro Vijijini na Kwang’andu na Kihangaiko Wilaya ya Bagamoyo.

SEKTA YA UTALII

29. Mheshimiwa Spika, Wizara imekamilisha maboresho ya Kanuni za Tozo ya Maendeleo ya Utalii na matumizi yake yataanza mwaka 2012/13. Elimu imetolewa kwa wadau kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Utalii ya mwaka 2008 hususan katika eneo la kujisajili na kulipia leseni za uendeshaji wa biashara ya utalii. Mikoa iliyohusika ni Pwani, Iringa, Rukwa, Kilimanjaro, Arusha, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Mara na Dar es Salaam ambapo jumla ya Wakala 640 wa biashara ya utalii wamepatiwa elimu.

30. Mheshimiwa Spika, mwaka 2011/12, Wizara imetoa mafunzo ya kupanga hoteli katika daraja kwa wataalamu 17 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, kati yao 15 walifaulu na kutunukiwa vyeti. Wataalamu waliofuzu wanatambulika na wanaweza kufanya zoezi la kupanga hoteli katika daraja kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha, Wizara imefungua ofisi za utalii Iringa kwa ajili ya Nyanda za Juu Kusini na Mwanza kwa ajili ya Kanda ya Ziwa. Kufunguliwa kwa ofisi hizo ni fursa ya kuchochea mpango wa kuendeleza utalii na kutangaza vivutio katika kanda hizo.

31. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Wizara kupitia Idara ya Utalii ililenga kukusanya Shilingi 3,433,872,661 kutokana na leseni mbalimbali za Wakala wa biashara ya utalii nchini. Hadi Juni, 2012, jumla ya Shilingi 3,765,959,717 zilikusanywa. Makusanyo hayo ni asilimia 109.7 ya makadirio.

(i) Bodi ya Utalii Tanzania (TTB)
32. Mheshimiwa Spika, Bodi kwa kushirikiana na wadau imetayarisha na kusambaza vielelezo mbalimbali vya utalii. Vielelezo hivyo ni pamoja na majarida ya Tan Travel, Accommodation Guide, Selling Tanzania , Conference Directory, Savor, Dar Guide, Dar life na Tanga Tourism Guide. Vilevile, Bodi ilichapisha kijitabu cha Utalii wa Utamaduni (Culture Tourism Book), DVD na CD Rom za utalii.
Jarida la “Hard venture Tourism” litakalokuwa linatolewa kila baada ya miezi minne limechapishwa ili kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo kwenye maeneo ambayo ni magumu kufikika kutokana na sababu mbalimbali. Toleo la kwanza la jarida hilo limetolewa mwezi Agosti, 2012. Kazi nyingine zilizotekelezwa na Bodi zimeainishwa katika aya ya 55 hadi 58 katika Kitabu cha Hotuba.

(ii) Wakala wa Chuo cha Taifa cha Utalii
33. Mheshimiwa Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako tukufu kuwa tarehe 10 Desemba, 2011, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua rasmi Kampasi mpya ya Wakala wa Chuo cha Taifa cha Utalii inayoitwa Bustani, Jijini Dar es Salaam. Kampasi inatarajia kujiendesha kibiashara ikiwa ni sehemu ya mafunzo. Chuo kinatoa mafunzo katika ngazi ya Astashahada na Stashahada katika tasnia ya Ukarimu na Utalii kwa viwango vya kimataifa. Utekelezaji wa majukumu ya Chuo umeainishwa katika aya ya 60 ya Kitabu cha Hotuba.
SEKTA YA MAMBO YA KALE

34. Mheshimiwa Spika, kufuatia kukamilika kwa mkakati wa kutekeleza Sera ya Taifa ya Malikale, Wizara inafanya mapitio ya Sheria Na. 10 ya Mambo ya Kale ya mwaka 1964 na marekebisho yake Na. 22 ya mwaka 1979 kwa ajili ya kuandaa Sheria mpya ya Malikale.

35. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Wizara imekamilisha Mpangokazi wa ufukuaji wa Nyayo za Laetoli. Ili kujifunza mbinu bora za uhifadhi wa nyayo zinazopatikana katika miamba iliyotokana na Volcano, Kamati ya wataalam ilifanya ziara ya kimafunzo katika nchi za China, Korea ya Kusini na Ujerumani. Aidha, maabara ya nchi ya Ujerumani imetoa fursa kwa Tanzania kutumia maabara hiyo katika masuala ya utafiti na uhifadhi wa Nyayo za Laetoli.

36. Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Shirika la Utangazaji la Taifa iliandaa na kurusha vipindi 10 vya televisheni kuhusu malikale zinazopatikana kwenye maeneo ya Tongoni, Mapango ya Amboni na maeneo mengine ya Utalii katika Mkoa wa Tanga kupitia kipindi cha Zamadamu. Vilevile, Wizara ilishiriki katika mkutano Mkuu wa Kituo cha Kimataifa cha Mafunzo ya Uhifadhi na Ukarabati wa Mali za Kiutamaduni (ICCROM) uliofanyika Roma, Italia. Tanzania ilifanikiwa kupata uenyekiti wa mkutano huo ambao utadumu kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia Novemba, 2011.

37. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Wizara iliboresha mazingira ya vituo kwa kufanya ukarabati wa ofisi katika vituo vya Magofu ya Tongoni – Tanga na Kunduchi - Dar es Salaam. Vilevile, Makumbusho ya Kaole - Bagamoyo yalifanyiwa ukarabati na kuwekwa vioneshwa. Wizara katika kuadhimisha miaka 50 ya uhuru wa Tanzania Bara ilifanya ukarabati wa Makumbusho ya Kumbukizi ya Mwalimu Nyerere iliyopo Magomeni, Jijini Dar es Salaam. Aidha, vifaa vilivyotumiwa na Mwalimu J.K.Nyerere vilikusanywa, kufanyiwa matengenezo na kuwekwa kama vioneshwa katika Makumbusho hiyo.

(i) Uhifadhi wa Mali Kale
38. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2011/12, Wizara iliendelea na ukarabati wa Gereza (Ngome ya Mreno), Kasri ya Makutani, Husuni Kubwa na Husuni Ndogo katika eneo la Kilwa Kisiwani na Magofu ya Songo Mnara. Ukarabati huo umefanyika kwa ushirikiano wa Programu ya Maeneo ya Hifadhi za Bahari na Ukanda wa Pwani (MACEMP), UNESCO, Mfuko wa Balozi wa Marekani wa Uendelezaji Urithi wa Utamaduni na ‘ World Monument Fund’.

(ii) Uchimbaji wa Urani katika Pori la Akiba la Selous
39. Mheshimiwa Spika, Katika hotuba ya Wizara yangu ya Mwaka 2011/12, ilitolewa taarifa kuhusu Serikali kupeleka ombi UNESCO kuruhusiwa kufanya mabadiliko ya mipaka kwa kuondoa eneo la Mkuju lililoko katika Pori la Akiba Selous katika urithi wa dunia ili litumike kwa uchimbaji urani. Hii ni kwa kutambua kuwa Sheria ya Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 imeruhusu uchimbaji wa madini ya urani, mafuta na gesi ndani ya Mapori ya Akiba.

40. Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa, Mkutano wa 35 wa Kamati ya Urithi wa Dunia UNESCO uliofanyika Paris, Ufaransa tarehe 19 - 29 Juni, 2011 ulijadili maombi hayo na maamuzi kutolewa katika Mkutano wa tarehe 02 Julai, 2012. Kamati ilitoa idhini ya kipekee na isiyokuwa ya kawaida (exceptional and unique approval) ya kuruhusu kufanyika marekebisho ya Mpaka wa eneo la Urithi wa Dunia kwenye Pori la Akiba Selous ili kuruhusu shughuli za uchimbaji wa madini. Eneo lililoruhusiwa ni kilometa 215 za mraba, ambalo likijumuishwa na eneo la kinga (buffer zone) ni sawa na asilimia 0.8 ya Pori la Akiba Selous.

41. Mheshimiwa Spika, pamoja na eneo hilo kuondolewa katika Urithi wa Dunia, bado limebaki kuwa eneo la Pori la Akiba Selous. Hivyo, kilichopungua ni eneo la Urithi wa Dunia na sio ukubwa wa Pori la Akiba. Sambamba na shughuli za uchimbaji urani tahadhari za kimazingira zitaendelea kuchukuliwa na taasisi husika kabla, wakati na baada ya uchimbaji.

(iii) Ukusanyaji wa Maduhuli
42. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Wizara kupitia sekta ndogo ya Malikale iliweka lengo la kukusanya shilingi 540,263,633. Mapato hayo ni kutokana na wageni wanaotembelea vituo vya Mambo ya Kale pamoja na ada za utafiti. Hadi Juni, 2012, Wizara ilikusanya shilingi 516,496,180 sawa na asilimia 95.6 ya makadirio.

(iv) Shirika la Makumbusho ya Taifa
43. Mheshimiwa Spika, Ninayo furaha kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa majengo ya Mradi wa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni yaliyogharimu takriban shilingi bilioni 11 yamekamilika. Majengo ya Mradi huu yalizinduliwa rasmi tarehe 3 Desemba, 2011 na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

44. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2011/12, Shirika limeandaa maandiko saba ya utafiti. Tafiti mbili kati ya hizo zimeanza kufanyika, ambapo utafiti wa athari za kusitishwa kwa Tawala za Jadi katika tamaduni unafanyika Iringa na utafiti kuhusu uhifadhi wa mimea ya Shubiri (Aloe) unafanyika Dar es Salaam katika kijiji cha Makumbusho. Kazi nyingine zilizofanyika zimeainishwa katika aya ya 73 hadi 75 ya Kitabu cha Hotuba.

UTAWALA NA RASILIMALI WATU

45. Mheshimiwa Spika, mwaka 2011/12, katika jitihada za kukabiliana na upungufu wa watumishi, Wizara ilipewa kibali cha kuajiri watumishi 152 na taratibu za kuajiri zinaendelea. Watumishi 124 wa kada mbalimbali walipandishwa cheo kwa kuzingatia Miundo ya Utumishi wa Umma. Aidha, watumishi 20 walithibitishwa kazini na watumishi 46 walibadilishwa cheo.

46. Mheshimiwa Spika, kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuboresha utendaji, Wizara iliwezesha watumishi 170 kuhudhuria mafunzo mbalimbali ambapo watumishi 70 walihudhuria mafunzo ya muda mfupi na 100 mafunzo ya muda mrefu. Aidha, ili kuwaimarisha watumishi kimaadili, mada kuhusu maadili zilitolewa kwa watumishi 117 katika Mkutano wa Watendaji Wakuu wa Wizara, Watumishi 305 wa Makao Makuu na kwa watumishi 230 kwenye Semina ya mafunzo ya ukusanyaji maduhuli. Mafunzo maalum ya maadili yametolewa kwa wajumbe saba wa Kamati ya Maadili ya Wizara Aprili, 2012 Mkoani Morogoro. Aidha, Wizara ina Baraza la Wafanyakazi na katika mwaka wa fedha 2011/12, imefanya vikao viwili vilivyoshirikisha wajumbe 70 kila kimoja. Maelezo kuhusu ustawi wa watumishi yako katika aya ya 78 ya Kitabu cha Hotuba.

CHANGAMOTO KATIKA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU KWA MWAKA 2011/12

47. Mheshimiwa Spika, Pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa majukumu yake, Wizara ilikabiliwa na changamoto mbalimbali kama ifuatavyo:
i. Uhaba wa watumishi, hususan katika Sekta za Wanyamapori, Misitu na Malikale;
ii. Upungufu wa nyumba na huduma duni za watumishi katika vituo vya nje vya Wizara;
iii. Uvamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa na matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali za maliasili na malikale;
iv. Mwamko mdogo wa wananchi kushiriki utalii wa ndani; na
v. Miundombinu duni katika maeneo yenye vivutio vya utalii.

48. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuchukua hatua za kukabiliana na changamoto hizo kwa kujenga uwezo wa vyuo vya Wizara wa kudahili na kupata wahitimu wenye sifa; kuomba kibali cha ajira mpya; kujenga makazi ya watumishi; kuboresha maslahi ya watumishi; na kuboresha miundombinu. Aidha, Wizara inaongeza ushiriki wa wadau katika uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali na kuhamasisha utalii wa ndani.

MPANGO WA UTEKELEZAJI NA MALENGO KWA MWAKA 2012/13

SEKTA NDOGO YA WANYAMAPORI

49. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13, Wizara itaendelea kuimarisha usimamizi wa rasilimali za wanyamapori kwa kufanya mapitio ya Kanuni zilizopo na kuandaa Kanuni mpya za kutekeleza Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Na.5 ya 2009.
50. Mheshimiwa Spika, Wizara itaanzisha Pori la Akiba Piti katika Wilaya ya Chunya pamoja na kukamilisha uanzishaji wa maeneo sita ya WMAs. Maeneo hayo yameainishwa katika aya ya 81 ya Kitabu cha Hotuba. Aidha, gawio la asilimia 25 ya fedha zitokanazo na uwindaji wa kitalii kwa Halmashauri za Wilaya 42 na WMAs 16 litaendelea kutolewa.

51. Mheshimiwa Spika, mwaka 2012/13 Wizara itakamilisha uanzishwaji wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania. Vilevile, miundombinu, vitendea kazi na huduma zitaboreshwa katika mapori ya Akiba na Kikosi Dhidi ya Ujangili pamoja na kuongeza uwezo wa kufanya doria kwenye maeneo yaliyohifadhiwa.

(i) Vyuo vya Taaluma ya Wanyamapori
52. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2012/13, vyuo vya Taaluma ya Wanyamapori vitadahili jumla ya wakurufunzi 1,074 kama ifuatavyo: Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka wakurufunzi 550; Chuo cha Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi 324; na Kituo cha Mafunzo ya Usimamizi wa Maliasili kwa Jamii - Likuyu Sekamaganga 200. Kazi nyingine zitakazotekelezwa na vyuo hivyo zimeainishwa katika Aya ya 83.

(ii) Shirika la Hifadhi za Taifa, Tanzania (TANAPA)

53. Mheshimiwa Spika, Mwaka 2012/13, Shirika litaweka kipaumbele katika kuendeleza miundombinu ya barabara katika Hifadhi za Katavi, Ruaha, Mikumi na Saadani pamoja na kununua magari 10 kwa ajili ya hifadhi mbalimbali. Vilevile, nyumba nane kwa ajili ya familia za watumishi, daraja moja na “drifts” tatu zitajengwa katika Hifadhi ya Taifa Ruaha.
54. Mheshimiwa Spika, Shirika litaendeleza utalii wa kutembea kwa miguu, kuanzisha utalii wa usiku na utalii wa tufe (baloon) katika Hifadhi za Taifa Katavi, Ruaha na Mikumi na kuendelea kutangaza vivutio vya Utalii kwa kushirikiana na wadau wengine.

(iii) Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA)
55. Mheshimiwa Spika, Mwaka 2012/13, Mamlaka itaendelea kufanya matengenezo ya barabara na ukarabati wa majosho ndani ya eneo la hifadhi, kununua magari mawili kwa ajili ya doria na kuanza ujenzi wa jengo la kitega uchumi Arusha. Ufafanuzi wa kazi zitakazofanyika umeainishwa katika Aya ya 86 ya Kitabu cha Hotuba.

(iv) Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI)
56. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/13, Taasisi itaendeleza utafiti na kuidadi wanyamapori nchini pamoja na kujenga maabara ya kisasa ya utafiti wa nyuki. Tafiti zitakazofanyika zimeainishwa katika aya ya 87 ya Kitabu cha Hotuba.

SEKTA NDOGO YA MISITU NA NYUKI

57. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/13, Wizara itaendelea kupitia Sera ya Taifa ya Ufugaji Nyuki ya mwaka 1998, kukamilisha Sera ya Taifa ya Misitu ya mwaka 1998 na kufanya maboresho kwenye vifungu vya sheria. Aidha, Wizara itapitia viwango vya ubora wa mazao ya nyuki na shughuli za ufugaji nyuki katika wilaya za Kigoma, Kibondo na Kasulu. Kazi nyingine zitakazofanyika ili kuhifadhi misitu na kuendeleza shughuli za ufugaji nyuki zimeainishwa katika aya ya 89 katika Kitabu cha Hotuba.

(i) Vyuo vya Taaluma ya Misitu na Ufugaji Nyuki
1. 58. Mheshimiwa Spika, Vyuo vya Misitu na Ufugaji Nyuki vinatarajia kudahili jumla ya wakurufunzi 251 katika mwaka 2012/13 kama ifuatavyo: Chuo cha Misitu Olmotonyi (155); Chuo cha Ufugaji Nyuki Tabora (61) na Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi (35). Wizara itaendelea kuwezesha Vyuo vya Misitu na Ufugaji Nyuki vilivyopo chini yake kutekeleza majukumu yao. Ukarabati wa baadhi ya majengo na kuweka samani na majiko katika Chuo cha Ufugaji nyuki Tabora utafanyika. Aidha, Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi kitaanza ujenzi wa Maktaba katika mwaka huu wa fedha.

(ii) Wakala wa Mbegu za Miti Tanzania (TTSA)
59. Mheshimiwa Spika, Mwaka 2012/13, Wakala utaendelea kutoa huduma kwa kuuza mbegu na miche ya miti pamoja na kutunza vyanzo 31 vya mbegu za miti ya aina mbalimbali. Ufafanuzi kuhusu kiasi cha mbegu na aina ya miche itakayozalishwa upo katika aya ya 91 ya Kitabu cha Hotuba.

(iii) Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI)
60. Mheshimiwa Spika, mwaka 2012/13, Taasisi itaendelea kufanya tafiti mbalimbali pamoja na kuboresha mazingira ya kufanyia kazi. Aidha, Taasisi itaendelea kushirikiana na wadau wa kikanda na kimataifa kwa lengo la kuhifadhi na kuongeza ubora wa miti. Maelezo ya kina kuhusu tafiti zitakazofanyika na wadau watakaohusika yako katika aya ya 92 na 93 ya Kitabu cha Hotuba.

(iv) Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)

61. Mheshimiwa Spika, Mwaka 2012/13, Wakala utaandaa mipango ya usimamizi wa hekta 453,000 za misitu katika misitu ya asili na mashamba 15 ya miti ya kupanda. Aidha, tathmini kuhusu rasilimali za misitu kupitia mradi wa National Forest Resources Monitoring and Assessment (NAFORMA) itafanyika ili kumalizia vitalu 108 vilivyobaki.

Vilevile, litafanyika zoezi la kuweka mipaka na maboya (beacons) kwenye misitu ya hifadhi na mashamba ya miti pamoja na kusafisha njia za kuzuia moto. Maelezo kuhusu kazi zitakazotekelezwa na Wakala yapo katika aya ya 95 hadi 100 katika Kitabu cha Hotuba.

SEKTA NDOGO YA UTALII

62. Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ina mpango wa kuendeleza jiji la Dar es Salaam kuwa kivutio cha Utalii. Mpango Mkakati wa miaka mitano (2012 - 2017) ambao utaanza kutekelezwa mwaka 2012/13 umeandaliwa. Aidha, Wizara itafanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 1999 ili kukidhi mahitaji ya sasa.

63. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza Sheria ya Utalii ya mwaka 2008, Kanuni za Tozo za Maendeleo ya Utalii (Tourism Development Levy) zimekamilika. Mwaka 2012/13, Wizara itahamasisha wadau kuhusu tozo hizo na kuanza kutumika rasmi. Vilevile, Wizara itafanya utafiti wa mwenendo wa biashara ya utalii nchini kwa kukusanya na kuainisha takwimu za utalii wa ndani na wa kimataifa.
BODI YA UTALII TANZANIA

64. Mheshimiwa Spika, Bodi itaanza kutekeleza Mkakati Mpya wa Miaka Mitano wa Utangazaji Utalii Kimataifa mwaka 2012/13. Aidha, Bodi itaendelea kuhamasisha uanzishwaji wa miradi ya utalii wa kiutamaduni kwa kutoa elimu ya uhamasishaji katika vikundi mbalimbali katika mikoa ya Kusini, Kanda ya Ziwa na Nyanda za juu Kusini. Vilevile, Bodi itaendelea kutangaza utalii kupitia michezo, ambapo pamoja na matangazo katika Ligi Kuu ya mpira wa miguu ya Uingereza, imeweka matangazo ya utalii katika kiwanja cha mpira wa miguu wa Kimarekani na soka kinachomilikiwa na Kampuni ya Seattle SeaHawks ya mjini Seattle nchini Marekani.

65. Mheshimiwa Spika, Bodi ya Utalii itakamilisha kazi ya kuunda utambulisho (destination brand development) baada ya kukamilisha kazi za awali za kutathmini jinsi Tanzania inavyoonekana machoni mwa wageni (image investigation) na kutafuta utambulisho (brand identity) kama hatua muhimu za kuunda utambulisho ambao utasaidia kuimarisha muonekano wa Tanzania na kutangaza nchi yetu pamoja na vivutio vyake kikamilifu.

WAKALA WA CHUO CHA TAIFA CHA UTALII

66. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/13, Chuo kitaendelea kutoa mafunzo katika fani za ukarimu na utalii ambapo udahili unatarajiwa kuongezeka kutoka wakurufunzi 229 hadi 315. Aidha, Chuo kitaanzisha mafunzo ya jioni katika fani ya Upishi na kutoa huduma ya kutembeza watalii Dar es Salaam kwa malipo. Natoa wito kwa wananchi kujiunga na chuo hiki ambacho kinatoa elimu yenye ubora na uhakika ambao utawapatia ajira katika sekta rasmi na isiyo rasmi.

SEKTA NDOGO YA MAMBO YA KALE

67. Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kufanyia marekebisho Sheria ya Mambo ya Kale ya mwaka 1964 na marekebisho yake ya mwaka 1979. Vilevile, itaanza ujenzi wa kituo cha kumbukumbu na taarifa kwenye kituo cha Mapango ya Amboni, kujenga nyumba ya mtumishi katika kituo cha Oldupai na kukarabati nyumba ya mtumishi Kaole na Magofu ya Kilwa Kisiwani. Aidha, Mkakati wa utangazaji na uendelezaji wa vituo vya malikale utaandaliwa pamoja na kuendeleza zoezi la kufukua na kuhifadhi nyayo za binadamu wa kale zilizopo kwenye eneo la Laetoli.

SHIRIKA LA MAKUMBUSHO YA TAIFA TANZANIA

68. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/13, Shirika litaendelea kuandaa na kushiriki matamasha mbalimbali pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu shughuli za makumbusho kupitia vyombo vya habari. Aidha, Shirika litaandaa michoro ya ujenzi wa Makumbusho ya Falsafa ya Mwalimu J.K. Nyerere ya Ujamaa na Kujitegemea itakayojengwa Chamwino, Dodoma.

URATIBU, UTAWALA NA MAENDELEO YA RASILIMALI WATU

69. Mheshimiwa Spika, mwaka 2012/13, Wizara itafanya mapitio ya Mpango Mkakati (2010-2013) na kuandaa Mkutano wa kisera utakaoshirikisha wadau mbalimbali. Aidha, Mpango wa Miradi ya Uwekezaji wa muda mrefu unaoainisha maeneo ya uwekezaji katika sekta za maliasili, malikale na utalii utaandaliwa.

70. Mheshimiwa Spika, jitihada za kuongeza ukusanyaji maduhuli zitaendelezwa kwa kuwezesha upatikanaji wa vitendea kazi na kuendesha mafunzo kwa watumishi. Kazi zitakazofanyika kwa lengo la kuongeza ukusanyaji maduhuli zimeainishwa katika aya ya 115 ya Kitabu cha Hotuba.
SENSA YA WATU NA MAKAZI

71. Mheshimiwa Spika, kama tunavyofahamu, Mwezi huu wa Agosti, 2012 Tanzania itaendesha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi. Kwa Wizara yangu, zoezi hili lina umuhimu wa kipekee kwa sababu changamoto nyingi zinazoikabili sekta ya Maliasili (hususan Wanyamapori na Misitu); zinatokana na shughuli za kibinadamu katika hifadhi kama vile kilimo, ujenzi wa makazi na ufugaji nyuki. Idadi ya watu na kasi ya kuongezeka kwao na jinsi wanavyojitawanya katika maeneo mbalimbali ya nchi ina athari katika uhifadhi wa Maliasili pale ambapo uhifadhi endelevu hautazingatiwa. Hivyo, uchambuzi wa taarifa zitakazotokana na zoezi hili utatoa takwimu muhimu zitakazowezesha Wizara kuboresha sera na mikakati mbalimbali inayosimamia na kutoa msaada pale inapobidi. Nawapongeza wote waliohusika na maandalizi ya zoezi hili na tunatoa wito kwa wakazi wote kujitokeza kuhesabiwa.

SHUKURANI
72. Mheshimiwa Spika, naomba kutumia fursa hii kuwashukuru kwa dhati Mheshimiwa Lazaro S. Nyalandu, Naibu Waziri na Mbunge wa Singida Kaskazini, Bibi Maimuna K. Tarishi, Katibu Mkuu na Bibi Nuru H.M Millao, Naibu Katibu Mkuu, Wakurugenzi wa Idara, Wakuu wa Vitengo na Taasisi kwa ushirikiano wao katika kuniwezesha kutekeleza jukumu la usimamizi wa Wizara. Vilevile, napenda kuwashukuru watumishi wote wa Wizara na Taasisi zake pamoja na wadau wa sekta kwa juhudi wanazoonyesha katika utekelezaji wa kazi mbalimbali za Wizara. Aidha, nichukue nafasi hii tena kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira chini ya Mwenyekiti Mheshimiwa James Daudi Lembeli (Mb) kwa ushirikiano walionipatia katika kutekeleza majukumu ya Wizara yangu.

73. Mheshimiwa Spika, Kwa namna ya pekee, napenda kuishukuru familia yangu kwa upendo na uvumilivu wao katika kuniwezesha kutekeleza majukumu yangu. Nawashukuru kwa dhati, wapigakura wangu wa Jimbo la Bukoba Mjini kwa kuniamini na kunichagua kuwa mbunge wao, naahidi kuwa nitaendelea kuwatumikia kwa uwezo wangu wote. Aidha, nawashukuru Katibu wangu, Katibu Muhtasi na Dereva ambao wamenipa ushirikiano wa karibu katika kutekeleza kazi zangu.

74. Mheshimiwa Spika, Wizara imetekeleza majukumu yake kwa ushirikiano na wadau wa maendeleo kutoka nchi na asasi mbalimbali za kitaifa na kimataifa pamoja na sekta binafsi. Nichukue fursa hii kuwashukuru wote na kutaja baadhi ya wadau kama ifuatavyo: Finland, Japan, Marekani, Sweden, Ubelgiji, Ufaransa, Ujerumani, AFD, AWF, AWHF, DANIDA, Finnida, FAO, FZS, GIZ, ICCROM, IUCN, Jumuiya ya nchi za Ulaya, KfW, NORAD, Sida, SPIDER, SNV, UNDP, UNESCO USAID, UNWTO, World Bank, WMF na WWF.

I. HITIMISHO

75. Mheshimiwa Spika, kabla sijamaliza hotuba yangu, naomba niwaombe Watanzania kushiriki, kwa mara nyingine, katika shindano jipya la maajabu saba ya asili. Shindano hili, ambalo linajulikana kama Seven Natural Wonders linaendeshwa kupitia tovuti ya http://sevennaturalwonders.org na linashindanisha vivutio vya kila bara tofauti, ili kupata maajabu saba ya asili ya dunia katika kila bara.

Kati ya vivutio 12 vinavyoshindanishwa katika Bara la Afrika, Tanzania ina vivutio vitatu ambavyo ni Mlima Kilimanjaro, Kreta ya Ngorongoro na Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Naomba kuchukua fursa hii kuwahamasisha na kuwaomba Watanzania wote kuvipigia kura vivutio vya Tanzania vilivyoingizwa katika shindano hili. Ninaamini kwamba shindano hili linaweza kuwa fursa moja nzuri kwa Tanzania kujitambulisha na kwa njia moja kuitangazia dunia kuwa Mlima Kilimanjaro, ambao ni mlima mrefu kuliko yote barani Afrika; Hifadhi ya Taifa Serengeti, ambapo tukio la kuhama wanyama hutokea kila mwaka; na Kreta ya Ngorongoro, Kreta ya pekee duniani ambayo iko kamili na yenye wanyamapori wa aina mbali mbali.

76. Mheshimiwa Spika, ili Wizara iweze kutekeleza malengo yake kwa mwaka 2012/13, naomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi 77,249,692,390. Kati ya fedha hizo, Shilingi 26,665,371,000 ni kwa ajili ya Mishahara, Shilingi 37,871,639,000 kwa Matumizi Mengineyo na Shilingi 12,712,682,390 kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo.

77. Mheshimiwa Spika, Naomba kutoa Hoja.

No comments: