Saturday, July 14, 2012

MTU MMOJA AUWAWA KWA KUKATWA NA SHOKA NYUMBANI KWAKE MKOANI DODOMA

Na. Luppy Kung’alo wa Jeshi la Polisi Dodoma
 
Mtu mmoja aliyefahamika kwan jina la Steven Mabawa umri miaka (46) Mgogo na mkulima aligundulika akiwa ameuwawa nyumbani kwake kwa kukatwa na shoka kichwani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwanadamizi wa Jeshi la Polisi Bw. Zelothe Stephen alisema tukio hilo liligundulika siku ya ijumaa tarehe 13/07/2012 majira ya saa kumi moja asubuhi katika  kijiji cha Makutupa, Wilaya ya Mpwapwa.

Akizungumzia tukio hilo Bw. Zelothe Stephen alisema Dada wa Marehemu aitwaye Elina Madabwa ndiye aliyegundua tukio hilo, baada ya kuona hamuoni kaka yake kwa muda wa siku mbili toka alipofika kijijini hapo kwa lengo la kuvuna  Mahindi na Alizeti katika shamba lake

Bw. Zelothe Stephen alisema Dada wa marehemu alienda kutoa taarifa kwa mtendaji wa kijiji Bw. Juma Matogwa ambaye kwa pamoja walikwenda katika nyumba ya marehemu na kukuta  mlango wa nyumba  ukiwa wazi, na waipoingia sebuleni wakamkuta marehemu kakatwa na shoka kichwani upande wa kulia huku shoka likiwa bado limenasia kichwani mwa marehemu.

Kamanda Zelothe Stephen alisema mwili wa marehemu umechukuliwa toka eneo la tukio na umehifadhiwa katika chumba cha maiti katika Hospitali ya Wilaya na upelelezi wa Mauaji hayo unaendelea.

Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma alito wito kwa wanakijiji wa Makutupa kupitia mkakati wake wa Polisi Jamii na Ulinzi Shirikishi kushirikiana na Jeshi la Polisi Wilayani Mpwawa kwa lengo za kutoa taarifa za mauaji hayo ili kuhakikisha watuhumiwa wa mauaji hayo wanakamatwa.
Wakati huo huo, watoto wawili Jovin Benjamini mwenye umri wa miaka mitatu na Emerisiana Benjamini mwenye umri wa mika sita wamejeruhiwa na moto baada ya nyumba waliyokuwa wanaishi kuungua na kuteketea kwa moto.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Bw, Zelothe Stephen alisema tukio hilo limetokea katika eneo la Mji Mpya Katika Wilaya  ya Mpwapwa siku ya ijumaa Tarehe 13/07/2012 muda wa saa nne na dakika kumi usiku, ambapo nyumba hiyo iliungua na kuteketea.


“Watoto hao walikuwa wamelala muda huo, wakati mama yao anayeitwa Lilian Lymo alikuwa ameenda Dukani kununua Vocha na kumuacha mfanyakazi wa ndani wa nyumba hiyo akiwa sebuleni ndipo kukatokea hitilafu ya umeme iliyosababisha glopu kupasuka na kuangukia neti iliyoshika moto wakati watoto hao wakiwa usingizini” alielezea Kamanda Zelothe

Bw. Alisema moto huo ulianzia chumbani kwa watoto hao, ambapo kulijaa moshi, baada ya kugundua hivyo wapangaji wa nyumba hiyo waliamshana na kufanikiwa kubomoa mlango wa chumba cha watoto hao na kufanikiwa kuwaokoa, lakini wao walishindwa kuokoa mali zao baada ya moto kushika kasi.

Akizungumzia hali za watoto hao, alisema mmoja ambaye ni Emerisiana Benjamini ambaye aliungua mikono ametibiwa na kuruhusiwa, wakati mwenzake Jovin Benjamini amelazwa katika hospitali hiyo ya wilaya baada ya kuungua vibaya kuanzia kiunoni kushuka chini, miguuni na katika makalio.

Kwa mujibu wa majirani  na wapangaji wa  nyumba hiyo inayomilikiwa na Bw. Samweli Baharia walidai ilikuwa  na hitilafu ya umeme kwa muda mrefu ambapo walikwishatoa taarifa kwa mmiliki huyo juu ya hitilafu hizo za umeme kuja mwingi, kujizima au kuzimika  kwa umeme katika nyumba nzima.

No comments: