Saturday, July 21, 2012

Tanzania yazindua Kampeni ya kutangaza Utalii nchini Marekani


Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Khamis Kagasheki (wa tatu kulia) akiwa na mmiliki wa Klabu ya Seattle Sounders Bw. Joe Ruth ( wa pili kushoto) kabla ya kuanza kwa mchezo baina ya Chelsea FC na Seattle Sounders FC katika uzinduzi wa matangazo ya kuhamasisha utalii katika mji wa Seattle. Wengine katika picha kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Utalii Bw. Ibrahimu Mussa, Bw. Adrian Hanauer Meneja wa Seattle Sounders FC, Bi. Mwanaidi Majaar Balozi wa Tanzania Marekani na Dk. Aloyce Nzuki Mkurugenzi Mwendeshaji wa Bodi ya Utalii nchini. (Picha na Pascal Shelutete).

Sehemu ya Matangazo ya kuvutia watalii katika uwanja wa Seattle kama yanavyoonekana wakati wa mchezo wa uzinduzi baina ya Chelsea FC na Seattle Sounders FC. (Picha na Pascal Shelutete).

Tanzania yazindua Kampeni ya kutangaza Utalii nchini Marekani
·        Uzinduzi wa matangazo washuhudiwa na mechi ya Chelsea na Seattle FC

Na Pascal Shelutete, TANAPA
Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Khamis Sued Kagasheki ameshiriki katika kampeni maalum ya kutangaza vivutio vya utalii nchini katika mji wa Seattle nchini Marekani na kuelezea matarajio yake ya kuongezeka kwa idadi ya watalii nchini katika kipindi kifupi kijacho.

Kampeni hiyo ilizinduliwa jana katika mji wa Seattle nchini Marekani na kushuhudiwa na uwepo wa matangazo yanayotangaza vivutio vya utalii nchini katika mechi ya Mabingwa wa Ulaya, Chelsea FC na wenyeji.

Balozi Kahasheki alieleza kuwa Tanzania imekuwa ikitumia mpira wa miguu kwa ajili ya kutangaza vivutio vyake katika maeneo mbalimbali laikini safari hii waligeukia soko la mji wa Seattle ambao unao wapenzi wengi wa soka na ambao kufuatia matangazo haya ya utalii wanaweza kuvutiwa na kutembelea vivutio vya utalii nchini.

Waziri Kagasheki amesema kuwa inatarajiwa matangazo ya utalii yaliyozinduliwa yatawafikia watazamaji wapatao milioni mia nane kwa mwaka kupitia vituo mbalimbali vya televisheni vinavyorusha matangazo hayo pamoja na wale wanaofika uwanjani kwa ajili ya kuangalia mechi mbalimbali katika uwanja wa Seattle Sounders.  Mji wa Seattle ni soko muhimu magharibi mwa Marekani lenye wakazi wenye kipato kizuri na wanaotembelea maeneo mbalimbali duniani kwa ajili ya shughuli za utalii.

Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Marekani Bi. Mwanaidi Maajar naye alieleza kufurahishwa kwake na kampeni hiyo ya utalii ambayo alisema anaamini kuwa imekuja kwa wakati muafaka kwa kuwa mahitaji ya Wamarekani kutembelea vivutio vya utalii nchini yamekuwa yakiongezeka kila mwaka na kwamba kampeni iliyozinduliwa itasaidia kuongeza idadi ya wageni nchini na kufikia lengo la wageni milioni moja kwa mwaka kutoka laki nane waliopo hivi sasa.

Aidha, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Bodi ya Utalii nchini Dk. Aloyce Nzuki ambaye Bodi yake inahusika na utangazaji wa vivutio vya utalii nchini alieleza kuwa Kampeni ya Utalii iliyozinduliwa ni mojawapo ya mikakati madhubuti ya bodi yake ya kuhakikisha kuwa wanatumia mbinu mbalimbali kupenya katika masoko mapya ili kuvutia wageni kutembelea nchi yetu kwa shughuli za utalii na hivyo kuongeza pato la taifa.

Katika uzinduzi wa matangazo haya Timu ya Tanzania ilipata fursa ya kuwa na banda maalum ambapo iliweza kutoa maelezo juu ya vivutio vya utalii nchini kwa wageni mbali mbali waliofika kwa ajili ya kushuhudia mchezo wa Chelsea na Seattle Sounders kwa kugawa vipeperushi mbalimbali.

No comments: