Familia ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Chama cha Madaktari Tanzania, Dk. Steven Ulimboka, imeitisha kikao cha wanandugu kwa ajili ya kujadili tukio la kutekwa na kupigwa kwa daktari huyo.
Aidha, baada ya kikao hicho, familia itatoa taarifa rasmi katika siku ambayo itapangwa kwa vyombo vya habari ili kuweka wazi kwa Watanzania juu ya mkasa uliompata daktari huyo ambaye alikuwa kiongozi wa mgomo wa madaktari.
Taarifa za wanandugu hao kuitisha kikao hicho zimekuja siku mbili tu baada ya Dk. Ulimboka kunukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akieleza kwamba anayejua mpango mzima wa kumteka, kumtesa na kumpiga ni yeye pekee.
Mmoja wa wanandugu alisema kikao hicho cha kifamilia kilifanyika juzi (Jumatano) nyumbani kwa baba yake mzazi, Dk. Ulimboka eneo la Ubungo Kibango na kuwashirikisha wanafamilia waliopo jijini Dar es Salaam na wa Mkoa wa Mbeya.
Alisema hatua ya kuitisha kikao hicho kujadili tukio lililompata mtoto wao, limetokana na kuwepo kwa taarifa zinazokinzana zinazotolewa na baadhi ya viongozi wakiwemo wa Jeshi la Polisi ambazo zinawachanganya Watanzania washindwe kujua ukweli wa tukio hilo.
Mwanafamilia huyo ambaye aliomba jina lake lisitajwe kwa kuwa si msemaji wa familia, alisema katika kikao hicho pia watajadili kama watahitaji suala la ulinzi wa Dk. Ulimboka kutoka Jeshi la Polisi pamoja na kumruhusu kuhojiwa na Polisi au la.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam, Suleiman Kova, juzi alieleza kuwa vyombo vya usalama vitamhoji Dk. Ulimboka kuhusiana na tukio lililompata.
“Unajua tangu Dk. Ulimboka akumbwe na mkasa huu na kupelekwa Afrika Kusini na kurejea nchini, kumekuwa na mambo mengi yanayozungumzwa, sasa sisi kama wanafamilia, tumeamua kukutana kujadili suala hili na baada ya hapo tutatoa tamko rasmi la tukio zima lilivyotokea,” alisema mwanafamilia huyo.
Dk. Ulimboka juzi alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akieleza kuwa Watanzania wavute subira kwani anajipa muda wa kueleza ukweli wa tukio la kutekwa kwake.
Kamanda Kova alisema hatua ya kutaka kumhoji Dk. Ulimboka, litachukuliwa ili kuondoa maneno ya uvumi ambayo yamekuwa yakielezwa ndani na nje ya nchi tangu tukio la kutekwa daktari huyo litokee Juni, mwaka huu.
Dk. Ulimboka alirejea nchini Jumapili iliyopita akitokea Afrika Kusini alikokuwa akitibiwa, na kusema kuwa yupo tayari kuendeleza mapambano na kazi baada ya kupona kabisa.
Dk. Ulimboka alikwenda Afrika Kusini Juni 30, mwaka huu kwa ajili ya matibabu baada ya kutekwa, kuteswa na kupigwa kisha kutelekezwa kwenye msitu wa Mabwepande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia Juni 27, mwaka huu.
Tukio la kutekwa Dk. Ulimboka lilitokea Juni 26, mwaka huu saa 6:00 usiku wa kuamkia siku ya Jumatano ambapo watu watatu wanaodaiwa kuwa na bunduki aina ya shotgun na bastola, walimteka katika eneo la barabara ya Tunisia, Kinondoni.
Dk. Ulimboka alitekwa na watu hao mmoja akiwa amevalia nguo za kijeshi ambao walimchukua na kumpeleka katika msitu wa Mabwepande na kisha kuanza kumpa kipigo.
Katibu wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Edwin Chitage, alidai kuwa mazingira ya kutekwa kwa Dk. Ulimboka, yalifuatia baada ya kupigiwa simu na mtu mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Abeid, aliyedaiwa kuwa alijitambulisha kutoka Ikulu na kumweleza kuwa ana maelezo ya msimamo wa serikali kuhusu mgomo wa madaktari.
Alisema kwa kuwa ilikuwa usiku, Dk. Ulimboka alimtafuta daktari mwenzake, Dk. Deo ambaye alimsindikiza hadi eneo la barabara ya Tunisia, Kinondoni ambako walikubaliana kukutana na mtu huyo aliyejitambulisha kutoka Ikulu.
Alisema Dk. Ulimboka na Dk. Deo, hawakumtilia shaka mtu huyo aliyempigia simu kwa sababu tangu mgomo uanze, alikuwa akiwapa taarifa mbalimbali ya kinachoendelea hata katika baadhi ya vikao vya serikali na madaktari alikuwepo.
Aliongeza kuwa baada ya kufika eneo hilo, walimkuta mtu huyo (Abeid), akiwa peke yake na ghafla walijitokeza watu wengine watatu kati yao wawili walikuwa na bastola na mmoja na shotgun ambao walimzonga na kumteka na kumpakiza katika gari lenye namba za IT (International Transfer).
Watu hao walimchukua Dk. Ulimboka na huku wakimuacha Dk.Deo eneo hilo.
Alisema baada ya tukio hilo, usiku huo Dk.Deo alikwenda kutoa taarifa kituo cha polisi cha Oysterbay ambako hakupata ushirikiano wowote na kuamua kwenda kuripoti tena Kituo Kikuu cha Polisi ambako alielezwa na askari waliokuwa zamu kwamba atapata taarifa za tukio hilo asubuhi.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba, alisema alipigiwa simu saa 9:00 usiku na mmoja wa madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) aliyempa taarifa kuwa Dk. Ulimboka, ametekwa na watu wasiojulikana.
Alisema baada ya kupata taarifa hizo, juhudi za kumtafuta zilianza usiku huo na ilipofika saa 12:30 asubuhi, alipata taarifa kutoka Kituo cha Polisi Bunju kwamba wakamchukue Dk. Ulimboka na kwamba hali yake ilikuwa ni mbaya sana.
No comments:
Post a Comment