Tuesday, October 9, 2012

Ripoti Za Kifo Cha Mwangosi Kuwekwa Hadharani Leo


Na: Elizabeth Edward, Mwananchi.

 SERIKALI leo inatoa hadharani ripoti ya Kamati iliyoundwa kupata taarifa kuhusu vurugu zilizotokea mkoani Iringa na kusababisha kifo cha aliyekuwa mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi. Wakati ripoti hiyo ikitarajiwa kutolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Kamati nyingine iliyoundwa na Baraza la Habari (MCT) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (Tef), nayo leo inatarajiwa kuweka hadharani ripoti yake.

 Kamati hizo ziliundwa kwa nyakati tofauti baada ya vurugu zilizotokea Septemba 2, mwaka huu katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi wakati polisi walipowatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakifungua tawi la chama hicho katika kijiji hicho. 

 Juzi, Makamu Mwenyekiti wa Kamati iliyoundwa na Dk Nchimbi, Theophil Makunga alimkabidhi waziri huyo na kusema Kamati yake ilifanya ziara Iringa na pia mahojiano na wadau mbalimbali Dar es Salaam.Kamati ya Nchimbi ilikuwa ikiongozwa na Mwenyekiti Jaji Steven Ihema, Makunga na Ofisa wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Pili Mtambalike, Kanali Wema Wapo wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) pamoja na Naibu Kamishna wa Jeshi la Polisi, Isaya Mngullu.

Tofauti na taarifa nyingine, ripoti ya mauaji ya Mwangosi inatarajiwa kutolewa hadharani ili umma uweze kuisoma, kuichambua na kutoa maoni kuhusu hatua za kuchukua ili matukio ya aina hiyo yasitokee tena. Ripoti ya MCT Katibu Mkuu wa Tef, Neville Meena alisema timu ya uchunguzi imeshamaliza kazi yake na leo itatoa rasmi ripoti kuhusiana na mazingira ya kifo cha Mwangosi.

Kamati hiyo iliundwa na watu watatu, John Mirenyi kutoka MCT, Hawra Shamte kutoka Tef na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini, Saimon Berege. “Sisi tukiwa wanahabari tuliunda Kamati yetu ili ifanye uchunguzi kuhusiana na mauaji ya mwanahabari mwenzetu, baada ya kukamilisha uchunguzi huo, sasa tupo tayari kuiwasilisha ripoti yetu hadharani,” alisema Meena. 

Chanzo:  http://www.mwananchi.co.tz

No comments: