Friday, November 2, 2012

Hali Ni Tete Dar es Salaam, Hofu Ya Maandamano Imetanda.


JIJI la Dar es Salaam leo hii limekumbwa na ukimya wa ghafla kutokana na kuwepo kwa hofu ya kufanyika kwa maandamano ya Waislamu ambayo huenda yakaanda mara baada ya Swala ya Ijumaa.
Licha ya Serikali kupitia Jeshi  la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kuwatahadharisha wananchi kutoshiriki maandamano hayo yaliyoandaliwa na Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania ili kuepusha uwezekano wa kutiwa mbaroni kwa sababu hayana kibali, lakini kuna hofu kwamba Waislamu hao wanaweza kuandamana, hali ambayo imewafanya wananchi wengi hasa wanaofanya shughuli zao katika ya Jiji kutokwenda kabisa.

Maandamano hayo yalipangwa kufanyika jana na leo kushinikiza Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Sheikh Ponda Issa Ponda, na wenzake wanaokabiliwa na mashtaka mbalimbali kupewa dhamana.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema juzi kwamba Jeshi la Polisi halitakuwa na uvumilivu wa aina yoyote kwa vitendo vya fujo na vurugu vitakavyosababishwa na watu watakaothubutu kuandamana na badala yake hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

Kova alisema kwenda mahakamani kwa maandamano ni sawa na kuingilia uhuru wa mahakama, hivyo Jeshi la Polisi litahakikisha linaimarisha ulinzi katika Mahakama ya Kisutu na kuweka utaratibu wa kiwango cha watu watakaoruhusiwa kuingia mahakamani hapo na watakaokiuka  hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

Huenda tishio hilo ndilo lililowafanya jana wasiandamane, lakini tetesi zilizopo ni kwamba, huenda wakafanya maandamani leo mchana.

No comments: