Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Khamis Kagasheki(Pichani)
na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Marekani Bwana David Hayes kwa
pamoja watazindua Kituo cha Wageni cha Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori
(Wildlife Management Area - WMA) cha Burunge Mkoani Manyara na kukikabidhi kwa wananchi. Uzinduzi huo
ambao utafanyika tarehe 5 Februari 2013 ni sehemu ya maadhimisho ya
jumuiya za WMA ambazo zilianzishwa nchini mwaka 1998 kwa mujibu wa
Sheria ya Wanyamapori.
Pia,
ni kuonyesha mafanikio ya Programu ya kuendeleza WMA ambayo
inafadhiliwa na Serikali ya Marekani. Vilevile ni ishara kuwa Serikali
ya Marekeni itaendelea kuunga mkono shughuli za uhifadhi nchini
Tanzania, hususan mapambano dhidi ya ujangili.
Kituo
cha Wageni cha Burunge ni sehemu tu ya misaada inayotolewa na Serikali
ya Marekani katika Programu ya Kuendeleza WMA nchini kote. Kwa WMA ya
Burunge misaada mingine ni ujenzi wa barabara za kufanikisha uhifadhi,
kujenga kituo cha askari wa Wanyamapori na kujenga lango kuu la
kuingilia kwenye eneo la WMA hiyo.
Jumuiya
za Hifadhi za Wanyamapori ni maeneo ya wanyamapori yanayohifadhiwa na
kulindwa na Wananchi kwa manufaa yao na taifa. Tangu zianzishwe mwaka
1998 kuna jumla ya WMA 17 nchini ambazo zimesajiliwa rasmi na wahusika
kuruhusiwa kufanya matumizi endelevu katika maeneo hayo. Aidha, kuna
maeneo 21 ambayo yako katika hatua mbalimbali za kuanzishwa WMA.
[MWISHO]
George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
4 Februari 2013
No comments:
Post a Comment