Mkutano Mkuu wa Dharura
ulioitishwa na wanachama wa Simba, Machi 17 mwaka huu na kuuondoa uongozi wa
klabu hiyo si halali kwa vile haukufuata taratibu, na Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) halitambui Kamati za Muda.
Uamuzi huo umefikiwa na
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) iliyokutana jana (Machi 24 mwaka huu) jijini Dar es Salaam chini
ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa.
Kamati imebaini kuwa kwa
mujibu wa Ibara ya 22(2) ya Katiba ya Simba, Mkutano Mkuu wa Dharura unaitishwa
na Kamati ya Utendaji baada ya wanachama wasiopungua 500 kuwasilisha ombi hilo
kwa maandishi na kujiorodhesha. Mkutano huo haukuitishwa na Kamati ya Utendaji
ya Simba.
Utaratibu huo
haukufuatwa ambapo barua ya Mkutano huo iliandikwa kwa Msajili wa Klabu na
Vyama vya Michezo badala ya Kamati ya Utendaji ya Simba ambayo ndiyo matakwa ya
Katiba ya Simba.
Kwa mujibu wa Katiba ya
Simba, Kamati ya Utendaji ndiyo inayoitisha Mkutano Mkuu wa Dharura baada ya
kuhakiki uhai na uhalali wa wanachama waliojiorodhesha kuomba mkutano huo.
Kamati imesisitiza kuwa
Katiba za wanachama wote wa TFF hazina kipengele cha kura ya kutokuwa na imani
na uongozi (vote of no confidence), ndiyo maana uko nyuma wanachama wa Yanga,
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Shinyanga (SHIREFA) na Chama cha Mpira wa
Miguu Mkoa wa Tabora (TAREFA) walipiga kura hiyo, na TFF kutotambua uamuzi wao.
Hata Katiba ya Simba
haitoi mamlaka kwa Mkutano Mkuu wa Dharura kufukuza uongozi uliochaguliwa.
Katiba za wanachama wote
wa TFF zimezingatia katiba mfano za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu
(FIFA) ambazo zinasema kiongozi ataingia madarakani kwa uchaguzi, na si
kuteuliwa (Kamati ya Muda).
Pia Kamati imesema
endapo wanachama wa Simba wangefuata taratibu na uongozi ukakataa kuitisha
mkutano, wanachama wangetuma ombi hilo TFF kupitia Kamati ya Sheria ili kutoa
mwongozo kwa uongozi wa Simba .
No comments:
Post a Comment