Na: Albert Sanga- Iringa
Nawasalimu
wasomaji wote, pia ninawapongeza na kuwashukuru wale wote ambao
wamekuwa wakiwasiliana nami. Mbarikiwe. Itakumbukwa kuwa huko nyuma
nimepata kuandika makala iliyokuwa na kichwa, "Naiona Afrika ikiinuka
tena". Katika makala ile nilieleza kwa sehemu namna Afrika ilivyoanza
kuzinduka na leo katika makala haya (na zitakazofuata kila
nitakapopatwasaa wa kuchambua uchumi wa Afrika) nitaeleza namna Afrika
ilivyoanza kutembea katika mstari wa mafanikio ya kiuchumi, kijeshi na
kijamii pasipo kuwategemea akina "bwana mkubwa" kutoka ng'ambo.Nauona
umuhimu wa...SOMA ZAIDI
kuyachambua haya ili kwamba Waafrika wote tujitambue, kujikubali, na
kisha tujenge ari ya matumaini na fikra za ushindi sasa na kwa vizazi
vijavyo. Tumejikunyata vya kutosha, na sasa ni wakati wetu kutamba
duniani!
Kwa miaka
mingi sasa kila neon Afrika linapotajwa huwa linaunganishwa na migogoro
ya kivita, mabaa ya njaa na magonjwa, umbumbumbu na ulafi wa watawala,
umasikini na ufukara uliopindukia, mikosi, laana, kuonewa pamoja na
harufu ya jehanamu.
Waafrika
wengi tulijiona katika picha hiyo (nab ado wengi wanajiona hivyo),
lakini vile vile dunia imekuwa ikiiona Afrika kwa jinsi hiyo hiyo. Mengi
yameandikwa sana kuhusu Afrika, mengi yamesemwa, mikakati mingi kutoka
nje ya Afrika imekuwa ikifanyika (kwa madai) ya kuliokoa bara hili
ambalo wakati fulani wazungu waliliita kuwa ni bara la giza.
Wanazuoni
mahiri kutoka duniani waliibuka na nadharia na falsafa kedekede
zinazoonesha kuwa Afrika imefika katika hali mbaya kwa ajili ya ukoloni.
Namkumbuka Walter Roodney namna alivyoandika kitabu kiitwacho, “How
Europe underdeveloped Afrika” ambapo katika kitabu hicho ameeleza namna
Ulaya ilivyocheza karata zake kuimaliza Afrika. Wengine wakaja na mwanya
wa kisayansi wakieleza kibaiolojia.
Hawa
wakadai kuwa Waafrika wana genetiki zilizoumbwa kushindwa (unsuccessful
genetic codes). Hawa wanamaanisha kuwa umasikini na matatizo ya Waafrika
ni matokeo ya kukosewa kuumbwa! Yaani waafrika waliumbwa kushindwa
(Programmed to fail). Haiishii hapo; kwani wapo wachambuzi wa Biblia
ambao husema kuwa Waafrika ni kizazi kilicholaaniwa na Mungu ndio maana,
kila kitu hakifanikiwi ndani ya Afrika.
Hizo ni
sababu chache kati ya nyingi zilizoelezwa na kuendelea kuaminika kwa
miaka mingi. Kimsingi kila nadharia, falsafa na sababu inayoelezwa
kuhusu kukwama kwa Afrika inaonekana kuwa na usadifu Fulani wenye
mashiko; kiasi kwamba kila nadharia imejipatia wafuasi wengi. Bahati
mbaya ni kuwa nadharia na falsafa zote zinaua uwezo wa Mwafrika
kujikwamua na zinaendelea kuwafanya Waafrika waamini kuwa wao sio sehemu
ya wanadamu kamili katika hii dunia.
Hata hivo
wale tunaoifuatilia historia ya Afrika kwa macho ya uchanya, tunaona
sababu za Afrika kupita ilikopitia lakini pia tunaona Afrika
inakoelekea. Ni kweli kuwa Afrika imepita katika mkondo wa vita,
umasikini, majanga, kutengwa, kuonewa na kudharauliwa; lakini wasaa wa
Afrika kujikwamua umewadia nao unaendelea kutokea. Afrika inaumbika kwa
upya!
Ninaposema
Afrika inaumbika upya, ni vema tujikumbushe historia ya nguvu za
mataifa katika dunia. Kimsingi mataifa tajiri na yenye nguvu yamekuwa
yakipanda na kushuka huku nafasi zao zikichukuliwa na mataifa
yanayoibuka. Ukiyachunguza mataifa ambayo huibuka na kuyapiku yale
mataifa makubwa; mara zote huwa yametoka ama yamepitia kwenye matatizo
makubwa, ikiwemo umasikini mkubwa, vita ya wenyewe kwa wenyewe, kuonewa
na mengine niliyoyataja hapo juu.
Tunapoitazama
China tunaona kuwa kwa miaka zaidi ya 20 ilikuwa ikielea katika ujamaa
ulioonekana kama umepoteza mwelekeo lakini baada ya hapo imeibuka kwa
kasi sana kiasi kwamba sasa inaitishia nafasi ya Marekani kiuchumi na
kijeshi.
Nchi ya
India nayo kwa miaka mingi ilihaha kwa umasikini mkubwa lakini ndani ya
miaka 4 hadi 10 neema ikaitembelea na sasa uchumi wake unastawi kwa kasi
mno. Hata Brazil huko zamani ilikuwa ikiogelea katika lindi la
umasikini lakini kwa sasa ni moja ya nchi zinazopanda kwa kasi katika
ustawi wa viwanda duniani.
Zamani
yale mataifa saba tajiri (Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani,
Italia, Canada na Japan) yalijiona kama miungu mtu duniani,
yakajiandikia haki ya kuitawala dunia katia kila jambo kuanzia uchumi,
nguvu za kijeshi na kijamii.
Siku
zilivyokuwa zinaenda yakabaini kuwa wanachoamini ni “kujilisha upepo”
kwani kuna maaifa ambayo yanapanda kiasi kwamba ustawi wa chumi zake ni
mzuri kuliko wao wanaojiita G-7. Hapana shaka kwamba nchi hizi zilikuwa
zikijionea haya kujiita tajiri wa matajiri ilihali kuna matajiri
wakubwa kupita wao
Baada ya
mvutano na mjadala mwingi; kwa shingo upande yakasalimu kujibadilisha
jina kutoka G-7 hadi G-8 ambapo walilazimika kuliongeza taifa la Urusi.
Haikuishia hapo kwani mataifa haya yakabaini kuwa matatizo ya kiuchumi
ya dunia hayawezi kumalizwa na wao pekee hivyo wakaona ni wasaa wa
kutengeneza umoja utakaoyatabua mataifa mengine ambayo yanazidi
kuongezeka kila kona. Hii ikawa ndio sababu ya dunia kupata kinachoitwa
G-20.
Ukiacha
ngazi ya uchumi wa mataifa, tunaporudi katika chumi za mtu mmoja mmoja
(micro economics) tunaona pia mambo yakibadilika. Kwa miaka nenda rudi
taifa la Marekani ndilo limekuwa likitoa binadamu tajiri kuliko wote
duniani. Lakini miaka ya karibuni binadamu tajiri kuliko wote ametokea
taifa la Mexico, taifa ambalo miaka kadhaa nyuma lilikuwa kwenye orodha
ya nchi za ulimwengu wa tatu
Nini
maana ya mambo haya? Ni hivi: mambo yanabadilika na yanabadilika kwa
kasi sana. Taifa lenye nguvu leo haimaanishi kuwa litakuwa na nguvu
milele. Matajiri kwa sasa wanapatikana kutoka nchi zote, za ulimwengu wa
kwanza na za ulimwengu wa tatu.
Pia
ukweli ni kuwa mataifa mengi yanaanguka moja kwa moja na nafasi zao
zinazidi kuchukuliwa na yale mataifa ambayo yalidhaniwa kuwa ni madogo
na manyonge kabisa. Mataifa makubwa sasa yanatoa jasho!
Haya
mabadiliko yanayoipata dunia hayajaliacha nyuma bara la Afrika. Mwanga
wa matumaini unazidi kuonekana Afrika. Afrika imeanza kujitambua,
imeanza kuamka, imeanza kusimama na kimsingi itasimama moja kwa moja na
kuitawala dunia, kiuchumi, kijeshi na kijamii.
Hili
jambo sio “habari ya maono ya rohoni” isipokuwa ni mtiririko (trends) na
mahesabu yajayo (forecast) kutokana na yale yaliyotokea Afrika,
yanayoendelea kutokea na Afrika inavyojipachika (reposition) katika
“mdundo wa mabadiliko”.
Kabla ya
mwaka 1950 Karibu Afrika nzima ilikuwa ikitawaliwa na makoloni isipokuwa
nchi chache tu. Baada ya mwaka 1950 bara la Afrika lilipatwa na mfumuko
wa ukombozi, ambapo makumi ya nchi zilianza kujipatia uhuru wake miaka
ya 60 hadi 80.
Ifahamike
kuwa kilichofanya nchi nyingi za Ulaya ziachie makoloni ni kuyumba kwa
chumi zao kiasi kwamba wakawa hawana tena jeuri ya kuendesa makoloni
hasa baada ya vita ya pili ya dunia. Mataifa haya ni kwamba yalilazimika
kuyaachia makoloni kwa shingo upande.
Msomaji
napenda ushike hapa: Afrika haikupata Uhuru kwa bahati mbaya ama kwa
hiari ya walioitawala; isipokuwa ilipata uhuru kwa sababu ya kuyumba kwa
chumi za walioitawala”. Kisosholojia na kiimani tunasema uhuru wa
Afrika ulikuwa kama ujio wa nguvu za Mungu kwa Afrika baada ya
kutawaliwa kwa miongo mingi. (First God’s Visitation to Africa).
Bahati
mbaya ninaweza kusema kwamba Afrika iliuchezea ujio wa mara ya kwanza wa
Mungu! Hii ni kwa sababu baada ya nchi nyingi kujipatia Uhuru, wale
viongozi wa kwanza na wapigania uhuru wengi wao walijisahau. Badala ya
kuwatumikia wananchi wakajikuta wanalewa madaraka, wakawa walafi na
mafisadi na idadi ya kutosha wakageuka kuwa madikteta ghafla.
Huzuni
ilitanda upya Afrika pale ambapo, viongozi kutoka mataifa mengi
yaliyopata uhuru; waliporudi kuwapigia magoti wakoloni. Badala ya kubuni
mikakati ya kujitegemea wakawa kiguu na njia kwenda kuomba misaada kwa
wale wale waliowatawala. Mataifa mengi yakageuka kuwa tegemezi na mengi
yao hadi leo hayana jeuri ya kujitegemea asilimia mia moja kiuchumi,
kijeshi na kijamii. Hata hivyo hali haijabaki vivyo hivyo hadi sasa;
kwani mambo yanabadilika mno Afrika.
Tuonane wiki ijayo katika sehemu ya pili ya makala haya. Waafrika ni wakati wetu wa kung’aa kiuchumi
No comments:
Post a Comment