Mkuu wa mkoa wa Singida Dk.Parseko Vicent Kone akitoa taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo kwenye picha) juu ya ujio wa Mwenge wa uhuru mkoani Singida kesho Agosti 9 mwaka huu. Uongozi wa mkoa wa Simiyu utakabidhi Mwenge huo wa uhuru kwa uongozi wa mkoa wa Singida kwenye kijiji cha Nyahaa tarafa ya Kirumi wilaya ya Mkalama.Kushoto ni katibu tawala mkoa wa Singida, Liana Hassan.(Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.
Mwenge wa uhuru unatarajiwa kuzindua, kufungua, kuweka mawe ya msingi na kutembelea jumla ya miradi 62 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 25.6, wakati wa mbio zake za mwaka huu zinazotarajiwa kuanza kesho asubuhi mkoani Singida.
Akitoa taarifa ya ujio wa mwenge huo mkoani Singida, Mkuu wa mkoa Dkt. Parseko Vicent Kone amesema mwenge huo wa uhuru unatarajiwa kupokelewa kesho asubuhi katika kijiji cha Nyahaa kata ya Mpambala tarafa ya Kirumi wilaya ya Mkalama.
Amesema kuwa uongozi wa mkoa wa Simiyu wanatarajia kukabidhi mwenge huo wa uhuru kwa uongozi wa mkoa wa Singida kwenye kijiji hicho cha Nyahaa.
Baada ya kukimbizwa katika wilaya ya Mkalama, siku inayofuata utakimbizwa wilaya ya Iramba.
Agosti 11 wilaya ya Iramba utakabidhi mwenge huo kwa uongozi wa halmashauri ya manispaa ambao nao kesho yake, watakabidhi kwa uongozi wa halmashauri ya Singida.
LM
Dkt. Kone amesema mwenge wa uhuru unatarajiwa kumaliza mbio zake mkoani Singida Agosti 14 mwaka huu katika wilaya ya Manyoni, ambapo Agosti 15 uongozi wa mkoa wa Singida utakabidhi mwenge huo kwa uongozi wa mkoa wa Dodoma katika kijiji cha Mpedoo cha mkoa wa Dodoma.
Mkuu huyo wa mkoa, ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika maeneo yote ambayo mwenge wa uhuru utapitia.
Dkt Kone amesema "Mwenge wa uhuru uwe ni chachu ya maendeleo yetu, miradi yote itakayozinduliwa au kufunguliwa, tushirikiane kuitunza ili idumu na kutuletea maendeleo tarajiwa.
Miradi yote ambayo itawekwa mawe ya msingi tushirikiane pia katika kuikamilisha ndani ya muda mfupi na vyema iwe kabla ya mbio za mwenge wa uhuru wa mwakani".
No comments:
Post a Comment