Wednesday, August 7, 2013

Moto wazuka kwenye Uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta, Kenya

 
 
Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta nchini Kenya umefungwa kwa muda baada ya moto mkubwa kuwaka saa 11 alfajiri ya leo. Idara ya kupambana na majanga ya moto inajitahidi kuzima moto huo, na watu waliokuwa katika eneo hilo wameondolewa. Moto huo umeharibu vibaya eneo la kuingia na kupokea wageni. Mamlaka ya uwanja wa ndege ya Kenya imesema, operesheni za uwanja huo zimesitishwa, huku ndege zinazoingia zikielekezwa kutua katika viwanja vingine nchini Kenya na pia viwanja vya ndege vya nchi jirani vya Entebe, Dar es Salam, na Kigali.
Rais Uhuru Kenyatta ametembelea eneo hilo kukagua hasara iliyosababishwa na moto huo. Mkurugenzi wa Shirika la ndege la Kenya Airway, Titus Naikuni amesema, abiria wote wanaingia na kutoka wako salama.
Wakati huohuo, mkuu wa polisi nchini Kenya David Kimaiyo amesema, hakuna watu waliofariki katika tukio hilo. Uwanja wa kimataifa wa Jomo kenyatta ni uwanja mkubwa katika kanda ya Afrika mashariki unaotumiwa na wasafiri wanaoelekea katika nchi nyingine za Afrika, Ulaya na hata Mashariki ya Kati.

Uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta nchini kenye waripuku


Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta umefungwa baada ya moto mkubwa kutokea katika uwanja huo mjini Nairobi. Kwa sasa moto huo umeweza kudhibitiwa

Rais Uhuru Kenyatta amewasili katika uwanja huo na anatarajiwa kuhutubia waandishi wa habari baadaye. Hadi kufikia sasa hakuna ripoti zozote za majeruhi .

Mwandishi wa BBC katika uwanja huo amesema kuwa kulikuwa na moshi mkubwa uliotoka katika eneo la kuondokea na kuingilia wageni.

Mamlaka ya uwanja huo imesema kuwa tayari watu waliokuwa katika eneo hilo wameondolewa.

Imesema kuwa baadhi ya operesheni za uwanja huo zimekatizwa huku ndege zinazoingia katika uwanja huo zikielekezwa kutua katika viwanja vingine ndege kama vile Entebe, Dar es Salam ,Kigali, Mombasa na kwingineko nchini Kenya.

Baadhi ya safari za ndege kutoka uwanja huo pia zimeahirishwa.

Mwishoni mwa wiki jana baadhi ya wenye maduka ya Duty Free katika uwanja huo walifurushwa baada ya serikali kusema kuwa leseni za wenye maduka zilikuwa zimepitwa na muda.

Hata hivyo chanzo cha moto bado hakijabainika.
 


No comments: