Saturday, March 24, 2012

Lowassa aigawa CCM Arumeru  Send to a friend
Saturday, 24 March 2012 09:08
0digg
Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa
ADAIWA KUPIGWA 'STOP' ASISHIRIKI,ASEMA NI UZUSHI WA KIPUUZI, CHADEMA WALIA
Waandishi Wetu, Arumeru na Dar
 USHIRIKI wa Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa kwenye kampeni za uchaguzi mdogo wa Ubunge Arumeru Mashariki unadaiwa kuigawa timu ya kampeni ya CCM inayomnadi mgombea wa chama hicho, Sioi Sumari.Lowassa ambaye yuko mkoani Arusha tangu Machi 20, mwaka huu, amekuwa akitajwa kwamba atamnadi Sioi lakini tofauti na makada wengine, hadi sasa hakuna ratiba yoyote ndani ya CCM inayoonyesha ni lini mbunge huyo wa Monduli atapanda jukwaani.

Habari zilizopatikana jana kutoka Arumeru na Dar es Salaam zinasema baadhi ya viongozi wa CCM na timu inayoongoza kampeni za uchaguzi huo wamegawanyika kuhusu Lowassa kupanda jukwaani, huku wengine wakipinga.

Kumekuwepo na kundi ambalo linaona kwamba Lowassa akiingia kwenye kampeni hizo anaweza kuzua mazingira  ambayo yataipa ugumu CCM kushinda kutokana na kumbukumbu kuwa alijiuzulu kutokana na kashfa ya utoaji wa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura iliyotolewa kwa kampuni tata ya Richmond Development LCC.

Chadema tayari kimetangaza kuwa endapo Lowassa atajitokeza kwenye kampeni hizo kumnadi mgombea wa CCM, watamuumbua kwa kile wanachodai wataweka hadharani tuhuma kinazodai zinamhusu.

Jana, mmoja wa viongozi wa chama hicho alisema: “Hatapanda jukwaani (Lowassa), wala hatothubutu kufanya hivyo kwani tayari ameambiwa aache na huyo aliyemwambia nadhani anamsikiliza, hawezi kukiuka.”

Kauli ya kiongozi huyo inafanana na ile iliyotolewa na mmoja wa makada wakongwe wa CCM anayeshiriki kampeni za Arumeru Mashariki ambaye Machi 20 mwaka huu akiwa Usa River alsikika akisema: "Lowassa hana umuhimu wowote” kwenye kampeni hizo.

Kiongozi huyo alikuwa akichangia mjadala usio rasmi uliokuwa ukiwahusisha makada kadhaa wakongwe wa CCM, walipokuwa wakisubiri kuanza kwa msafara wa kwenda kwenye moja ya mikutano ya kampeni.

Lowassa ajibu
Akizungumza kwa simu kuhusu madai hayo jana, Lowassa aliziita taarifa za kukatazwa kwake kupanda jukwaani kumnadi Sioi kuwa ni “uzushi usiokuwa na msingi.”

Hata hivyo, hakuwa tayari kuweka bayana aina ya ushiriki wake kwenye kampeni hizo zinazoelekea ukingoni, huku CCM kikikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mahasimu wao Chadema ambacho kimemsimamisha, Joshua Nassari.

“Kwani kuna nini, hakuna haja ya kuwa na haraka, kwani vyovyote itakavyokuwa mtajua tu,” alisema Lowassa.

Mapema jana asubuhi alipotafutwa kwa simu, Lowassa alisema asingeweza kuzungumza kwani alikuwa kwenye kikao. “Nipigie majira ya mchana kama saa tisa hivi, maana sasa niko kwenye kikao,” alisema.

Hata hivyo, watu walio karibu na kiongozi huyo walisema Lowassa atapanda jukwaani kesho na kwamba tayari ameanza kampeni za kumnadi Sioi kwa kufanya vikao vya ndani na kwamba kikao cha jana ni moja ya vikao hivyo.

“Hizo taarifa kwamba amezuiwa siyo za kweli, mimi nimehakikishiwa kwamba atapanda jukwaani kuanzia Jumapili (kesho) na ninavyofahamu tayari ameanza vikao vya ndani,” alisema mmoja wa watu wa karibu na Lowassa.

Mwana CCM mwingine aliye karibu na kiongozi huyo alisema: “Ni kweli walikuwa wakihaha kumzuia, eti wandai kwamba ushindi ukipatikana itaonekana kwamba ni mafanikio yake, lakini wameshindwa maana hadi sasa tuna uhakika Mzee (Lowassa) atapanda jukwaani."

Habari zaidi zinasema kuwa Mratibu wa Kampenzi za CCM katika uchaguzi huo, Mwigulu Nchemba juzi jioni alikutana na Lowassa kuweka mambo sawa kabla ya kiongozi huyo kupanda jukwaani kesho.

Timu ya kampeni
Tangu kuanza kwa kampeni hizo,inadaiwa kwamba kumekuwapo na hali ya kutokuaminiana ndani ya timu hiyo kunakotokana na kile kilichojiri wakati wa mchakato wa kura za maoni zilizompa ushindi Sioi.

“Tatizo kubwa hapa kwetu ni hilo, hawa wapambe wa mgombea hawaamini kwamba sisi wengine tumekuja kwa ajili ya kutafuta ushindi wa chama, wanatufikiria vinginevyo ndiyo maana unaweza kuona kama tuko makundi tofauti,” alisema mmoja wa makada waliopo Arumeru ambao wanashiriki kampeni hizo.

Kada huyo alisema awali ni kama kulikuwa na timu mbili za kampeni ambazo ni ile ya chama inayoongozwa na Nchemba na timu ya pili ni ile inayoongozwa na wapambe wa mgombea ambao walikuwa na wasiwasi kwamba mgombea wao anaweza kuhujumiwa.

“Lakini sasa naona kama imani inarejea taratibu, wanatuona tunavyochapa kazi na kumpigia kampeni mgombea wetu. Wasichofahamu ni kwamba msuguano huwa kwenye vikao tu, lakini mtu akishateuliwa hakuna haja ya kumpinga kwani kufanya hivyo ni kukiua chama chetu,” alisema kada huyo.

Hata hivyo, kada huyo alisema pamoja na misukosuko ya hapa na pale, kampeni zao zimekuwa zikiimarika kila kukicha na kwamba wana uhakika wa kushinda kiti hicho cha ubunge ambacho kiko wazi kutokana na kifo cha aliyekuwa mbunge wake, Jeremia Sumari.

Chadema walia
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa jana alilalamikia kile alichodai kuwa ni kuchezewa mchezo mchafu na makada wa CCM.

Malalamiko ya Dk Slaa yanatokana na  kusambazwa barua yenye nembo ya Chadema ambayo ina maneno ya kashfa dhidi ya Meneja Mwenza wa kampeni wa chama hicho, Vincent Nyerere.

Akizungumza kwenye mikutano ya hadhara katika Vijiji vya Nkoanekoli, Kata ya Nkoaranga, Kikwe na Akheri, Dk Slaa alisema amesikitishwa na barua hiyo iliyosambazwa usiku wa manane maeneo ya Tengeru na Leganga.

“Barua hii inaonyesha kama imeandikwa na Naibu Katibu Mkuu wa  Chadema, Zitto Kabwe lakini cha ajabu jina langu limekosewa limeandikwa Silaha wakati siitwi hivyo na imeghushiwa nembo na kumbukumbu ya chama changu. Huu ni wizi ambao haukubaliki hata kisheria,” alisema Dk Slaa.

Akinukuu barua hiyo, Dk Slaa alisema maneno yake yanamshauri kuachana na Vicent Nyerere kwa sababu amemchafua Mkapa, anayeheshimika Meru na nchi nzima, hivyo hali hiyo itasababisha kukosa kura Meru.

“Sisi tumechukua barua hizi na nakala tumepeleka polisi na namtaka Isaya Mngulu amtafute mhusika wa barua hii ili ashughulikiwe kwa sababu kughushi nembo ni kosa kisheria na njia za kumpata ni rahisi sababu anatafutwa hata kwa njia ya kompyuta,” alisema.

Dk Slaa alisema kuwa ugomvi wake siyo kukosewa jina lake wala kumchafua Nyerere, sababu watake wasitake Nyerere ni mtoto wa baba mkubwa wa marehemu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, hivyo hakuna uhusiano na uchaguzi huo.

Alisema ugomvi wake ni kughushi nembo hiyo ya chama na amegundua imeghushiwa baada ya kuwasiliana na Zitto ambaye alikana kuandika barua hiyo wala kuifahamu.

Zitto akizungumza kwenye mkutano wa hadhara jana pia alikana kuitambua barua hiyo.

No comments: