Na Mohammed Kuyunga
MCHORO wa mfano unaoonesha jinsi kifo cha msanii wa filamu nchini, Steven Charles Kanumba alivyokufa kutokana na tatizo la kutikisika kwa ubongo wake unawekwa hadharani kwa mara ya kwanza na Amani.
Kwa mujibu wa mchoro huo unaopatikana katika mtandao, unaonesha kitaalamu hatua kwa hatua jinsi ubongo unavyotikisika hadi binadamu kufikia hatua ya kukata roho.
TATIZO LA KANUMBA
Kitaalamu, tatizo lililompata marehemu Kanumba linaitwa ‘Brain Concussion’ ambapo ubongo ulihama kutoka kwenye makazi yake na hivyo kusababisha mfumo wa kupumua kushindwa kufanya kazi inavyotakiwa.
KINACHOSABABISHA
Kwa mujibu wa maelezo ya kitaalamu, mara nyingi hali hiyo husababishwa na mtu kuangukia kichwa, hasa sehemu ya nyuma kama siyo kula au kunywa kitu chenye madhara mwilini.
Wataalamu wanasema binadamu anapotokewa na hali hiyo hushindwa kuingiza hewa ya oksijeni (cardio-respiratory failure).
Cha kwanza, kwa mujibu wa madaktari, mara baada ya mtu kukutwa na hali hiyo, kucha zake hubadilika rangi na kuwa za bluu huku mapafu yakivilia damu na kuonekana kama maini.
Hatua nyingine ni mhusika kutokwa na povu kinywani muda mfupi kabla ya tukio la kukata roho kumfika.
Kwa kawaida,watalaamu wanasema, ili kujiridhisha kama tatizo ni hilo, madaktari hukagua ubongo ili kuona kama umevimba au kushukia kwenye uti wa mgongo jambo ambalo linadaiwa kutokea kwa marehemu Kanumba.
UCHUNGUZI UNAENDELEA KWA MKEMIA MKUU
Habari zaidi zinasema kuwa, madaktari waliomfanyia uchunguzi wa saa 3 Kanumba, walichukua sehemu ya maini na majimaji ya machoni na kuvipeleka kwa mkemia mkuu wa serikali ili kubaini endapo marehemu alikula kitu chenye sumu.
WADAU WASUBIRI KWA HAMU MAJIBU
Huku mkemia mkuu wa serikali akiendelea na uchunguzi huo, mitaani wadau na wapenzi wa marehemu wamekaa mkao wa kula wakisubiri kwa hamu majibu hayo, hasa kutokana na ukweli kwamba bado maneno ya mitaani yanapishana kuhusu ukweli wa kifo hicho.
Licha ya kwamba kesi ipo mahakamani lakini baadhi ya watu wanasema serikali ichunguze kwa undani sakata hilo kwa vile kuna uwezekano mkubwa kifo cha Kanumba kikawa na mikono mingi.
Kanumba alifariki dunia Aprili 7, mwaka huu nyumbani kwake Sinza ya Vatican City Hotel kwa kile kilichoelezwa kutokana na ugomvi baina yake na mpenzi wake, Elizabeth Michael ‘Lulu’.
Marehemu alizikwa Aprili 10, 2012 katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Lulu alikamatwa na kuhojiwa na askari wa Kituo cha Polisi cha Oysterbay jijini Dar kutokana na kifo hicho na baadaye kupandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Kisutu, Dar ambapo alisomewa mashitaka.
Kesi yake itatajwa tena Aprili 23, mwaka huu katika mahakama hiyo na yuko mahabusu ya Segerea.
No comments:
Post a Comment