Saturday, April 14, 2012

Mkapa awa mbogo




Rais mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa
NI BAADA YA WASOMI KUMKOSOA KWA SERA ZAKE ZA UBINAFSISHAJI, AWAJIA JUU, AHOJI TANGU 2005 KUNA KIWANDA KIPYA?
Waandishi Wetu
RAIS mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa jana alijikuta katika wakati mgumu baada ya kubanwa na wasomi waliokosoa hadharani sera zake za ubinafsishaji kwa maelezo kwamba hazijaonesha mafanikio, badala yake zimechangia kudorora kwa uchumi wa nchi.Sakata la Mkapa na wasomi hao lilibuka jana katika Kongamano la Kigoda cha Mwalimu Nyerere lililofanyika kwenye ukumbi wa Nkrumah katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuibua msisimko wa aina yake kwa watu waliohudhuria.

Katika mjadala huo uliochukua takribani saa mbili, washiriki hao wengi wao wakiwa wasomi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), walihoji sababu za Rais huyo mstaafu kupigia debe sera zake za uwekezaji kwamba zingekuwa suluhisho lakini hadi sasa hali ya uchumi wan chi imezidi kudorora.

Hata hivyo, Mkapa alipinga vikali hoja za wasomi hao na kuwahoji  akitaka wamtajie, tangu mwaka 2005 alipoondoka madarakani, ni viwanda vingapi vipya vimejengwa? 
'Mnanilaumu kwa sera ya ubinafsishaji lakini niambieni viwanda vingapi vipya vimejengwa tangu mwaka 2005?" Alihoji Mkapa ambaye aliongoza Tanzania kuanzia mwaka 1995 hadi 2005.

Mkapa alitetea sera za ubinafsishaji na kueleza kwamba kimsingi hazikushindwa lakini zimeonekana kuwa na kasoro kwenye utekelezaji wake kutokana na matatizo ya uongozi na kwamba aliamua kubinafsisha baadhi ya vitega uchumi kwani vilifilisika.
“Ili uendesha kiwanda unahitaji mitaji, uongozi bora na soko pamoja na ujuzi, sisi tulibinafisha baada ya kukosa mitaji na uwezo wa kuviendesha, tulishindwa kuviendesha, tulikuwa na viwanda vitano vya nguo… vyote vilikwenda hovyo hovyo,”alisema Mkapa.
Aliilaumu mamlaka iliyohusika na uwekezaji wakati wa utawala wake, kwa kile alichodai,  kushindwa kuueleza umma ukweli uliosababisha Serikali yake kuchukua uamuzi wa kubinafisha mashirika na viwanda mbalimbali.

“Tulibinafsisha mashirika na viwanda 330, kati yake 180 walikabidhiwa Watanzania na 23 wageni, vilivyobaki vilimilikiwa kwa ubia kati ya Watanzania na wageni, kwanini watu hawahoji sababu za hata wenyeji  kushindwa kuviendeleza? Twende tufanye utafiti tupate sababu za kushindwa,”alisizitiza Mkapa.

Aliongeza kuwa mbali ya  kuwapo matatizo katika sekta ya uchumi wa nchi, baadhi ya viwanda vilivyobinafisishwa vinafanya vizuri huku akitolea mfano kile cha Sukari cha Kilombero mkoani Morogoro.

Mkapa alitoa wito kwa watanzania kujituma kwa bidii kutafuata maendelea badala ya kuendelea kujadili masuala yasiyo na tija kwa maendeleo ya taifa.
Akizungumza kwenye mjadala huo, Profesa Issa Shivji, alisema ubinafsishaji uliofanywa nchini uliuza njia kuu za uchumi zikiwemo benki na Shirika la Bima na kuifanya Serikali kushindwa kusimamia na kulinda uchumi wa nchi.

Shivji alitofautiana na mtazamo wa Mkapa aliyedai kuwa ubinafishaji ulifanywa kwenye viwanda vilivyoshindwa kujiendesha kwa kukosa mitaji akisema:

“Viwanda tulivyobinafisha ni vile vilivyokuwa vinatoa faida, tatizo tulilofanya tulibinafisha njia kuu zote za uchumi hali iliyosababisha Serikali kushindwa kusimamia uchumi wa nchi.”

Msomi huyo alibainisha kuwa hata nchi zilizoendelea, ikiwamo China, ziko kwenye ubinafishaji lakini zinatenga maeneo ya kubinafisha.
Kwa upande wake Dk Ng'wanza Kamata ambaye ndiye aliyechokoza mada katika mdahalo huo, alihoji kama Afrika inaweza kutimiza ndoto ya kuwa kitovu cha uchumi duniani kwa kutumia sera na mfumo uliopo ambao unatoka mataifa ya Ulaya.

“Katika hotuba yako uliyoitoa Afrika ya Kusini umesema Afrika inaweza kuwa kitovu cha uchumi wa dunia kutokana na wingi wa raslimali zilipo, je ni kweli tunaweza kufika huko kwa kutumia mifumo na sera zilizopo? Alihoji Dk Kamata na kuongeza:

“Wazungu wanajua kuwa Afrika ina utajiri wa rasilimali tangu mkutano wa Berlin”.
Dk Kamata alisema mfumo wa utandawazi  unaonekana kama umejileta wenyewe ambao ndani yake watu wa Ulaya wanatafuta mahali pa kupeleka mitaji yao ili waweze kupata faida.

“Zipo kampuni 600 zinazoshika uchumi wa dunia, lengo lao siyo kusadia wananchi katika nchi husika bali kutengeneza faida kwa maslahi yao,”alisema.

Kuhusu udhaifu wa Serikali wadau hao walisema mikakati mingi ya maendeleo inashindwa kutekelezeka kutokana na tatizo la viongozi kutowashirikisha wananchi katika kuandaa miradi ya maendeleo.

“Kama viongozi serikalini wangewashirikisha wananchi katika kujadili miradi ya maendeleo mikakati mingi ingefanikiwa,”alisema Maselina Charles kutoka Morogoro.

Historia ya ubinafsishaji
Ubinafsishaji wa Mashirika ya umma hapa nchini ulianza tangu mwaka 1993 na ulikuwa unaratibiwa na Tume ya Rais ya Kurekebisha  Mashirika ya Umma (PSRC) iliyopewa mamlaka ya kusimamia
na kuongoza shughuli zote za ubinafsishaji.

Hata hivyo shughuli za tume hiyo zilisitishwa Desemba 2007 baada ya kukamilisha  ubinafsishaji wa mashirika mengi ambayo yalikuwa yametengwa.

Mashirika ya Umma 34 ambayo yalikuwa kwenye hatua za ubinafsishwaji yalihamishiwa katika Shirika Hodhi la Mali za Makampuni yaliyobinafsishwa kutoka PSRC kuanzia kuanzia Januari 2008.

Januari 2008 Shirika Hodhi la Mali za
Makampuni Yaliyobinafsishwa lilipewa majukumu ya kuendesha shughuli za kampuni zilizokuwa kwenye makakati wa kubinafsishwa.

Matatizo kwenye Ubinafsishaji
Kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (SAG)mashirika yaliyotengwa kawa ajili ya kubinafsishwa, yalikuwa yamezuiwa kupanuka zaidi kwa sababu hayawezi kuandaa na kutekeleza mipango mikakati au kuwekeza.

Pia wafanyakazi wa mashirika hayo wanakuwa hawana morali wa kufanya kazi au kutimiza wajibu wao kwa sababu ya kutokujua hatima ya ajira yao na ya mwajiri wao.

Uchakavu wa mali na raslimali za mashirika yaliyotengwa unakuwa ni wa kiasi cha juu kutokana na kukosa fedha kwa ajili ya ukarabati au urudishwaji wa mali zilizoharibika unakuwa mgumu.

No comments: