Daniel Mjema, Dodoma
OFISI ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), imeingilia kati mgogoro wa ununuzi wa kahawa mbivu (cherry) mkoani Mbeya na kutengua zuio la ununuzi wa aina hiyo ya kahawa.
Hivi karibuni, watu waliojiita ni wadau wa zao la kahawa walipitisha azimio la kupiga marufuku ununuzi wa kahawa mbivu wakidai unawanyonya wakulima na kutaka wauze kahawa yao kwenye vikundi pekee.
Walikuwa wakijenga msingi wao kwa kuoanisha bei anayopata mkulima anayeuza kahawa yake ya maganda au kwenye mnada, wakitaka ifanane na ile anayopata anapouza kahawa mbivu kabla haijamenywa.
Takwimu zinaonyesha ili kupata kilo moja ya maganda, mkulima analazimika kumenya kilo tano za kahawa hiyo, hivyo dhana kuwa mkulima aliyekuwa anauza kahawa mbivu anapunjwa ilikuwa siyo sahihi.
Baadhi ya viongozi wa mkoa huo walitajwa kuwa na maslahi binafsi katika mpango huo, kwa vile walikuwa wakimiliki vikundi vilivyojiita ni vya wakulima, hivyo kutaka ndivyo vinunue kahawa.
Hata hivyo, katika barua yake ya Aprili 10, Waziri mkuu kupitia Tamisemi ameagiza kuondolewa kwa zuio hilo na kuziagiza halmashauri zote za mkoa huo
“Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi imesikitishwa na zuio la ununuzi wa kahawa mbivu Mkoa wa Mbeya lililotolewa na halmashauri za mkoa huo, hivyo ofisi ya Waziri mkuu imeondoa zuio hilo kuanzia leo,” inasomeka sehemu ya barua hiyo.
Barua hiyo iliyotiwa saini na D.I Bandisa kwa niaba ya Katibu Mkuu Tamisemi, imemwagiza Katibu Tawala wa Mkoa (Ras) kuwajulisha wakuu wote wa wilaya za mkoa huo kuhusu kuondolewa kwa zuio hilo
No comments:
Post a Comment